FAUSTINE KAPAMA,
MAGRETH KINABO
JAJI Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 26 Juni, 2024 amezindua Kongamano la Kimataifa la Mahakama kuhusu Haki Miliki, Alama za Biashara na Usimamizi wa Mashauri kujadili mada mbalimbali zinazolenga kuwajengea uwezo Majaji na Mahakimu katika kushughulikia mashauri yanayohusu miliki bunifu.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akitoa hotuba yake leo tarehe 26 Juni, 2024 ya ufunguzi wa kongamano la kimataifa la miliki bunifu na usimamizi wa mashauri la siku mbili linalofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto)akizungumza jambo picha ya juu na Naibu Jaji wa Mahakama Kuu ya Uingereza, Mhe.Daniel Alexander(kushoto), (kulia) ni Afisa Sheria wa Shirika la Kimataifa na Miliki Bunifu Duniani(WIPO), Bi. Ines Fernandez Ulate, picha ya chini na kulia picha juu ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma(katikati) akiwa katika kongamano hilo na majaji wengine, (wa pili kulia) ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo, (wa pili kushoto) ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani, (wa kwanza kulia) ni Naibu Jaji wa Mahakama Kuu ya Uingereza, Mhe.Daniel Alexander na (wa kwanza kushoto)Afisa Sheria wa Shirika la Kimataifa na Miliki Bunifu Duniani(WIPO), Bi. Ines Fernandez Ulate.
Kongamano hilo ambalo la siku mbili linalofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam, ambalo limeandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Miliki Bunifu Duniani (WIPO), linawaleta pamoja Majaji wa Tanzania, Majaji kutoka Mahakama ya Uingereza na Kenya, Naibu Wasajili na Mahakimu wa Mahakama ya Tanzania.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kongamano hilo, Mhe. Prof. Juma aliwataka Majaji na Mahakimu kusimamia masuala ya haki miliki kwa ufanisi, haki na uthabiti katika robo ya pili ya karne ya 21.
"Sote tunakubali kwamba Karne ya 21 inakwenda kwa kasi,na mipaka mingi mipya inayohitaji Mahakama kushika kasi. Hakuna shaka kwamba, katika miaka ijayo, mashauri ya haki miliki yataendelea kuvuka mipaka mipya,” alisema.
Jaji Mkuu alisema kwamba kutokana na mabadiliko ya haraka ya teknolojia ya kisasa na akili bandia, robo ya pili ya Karne ya 21 itashuhudia ubunifu na uvumbuzi wa kuvuka mipaka.
Mhe. Prof. Juma alisema kuwa Mahakama zitazidi kutegemewa kulinda haki miliki za wabunifu na wavumbuzi. Alikubaliana na wale, kama Francelina Perdomo Klukosky, ambaye anasisitiza kwamba kulinda haki miliki ni ndoto ya lazima katika karne ya 21.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya akitoa neno la utangulizi kwenye kongamano hilo.
Baadhi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Majaji ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Naibu Wasajili na Mahakimu wakiwa katika kongamano hilo.
Baadhi ya wageni waalikwa, Naibu Wasajili na Mahakimu wakiwa katika kongamano hilo.
Jaji Mkuu alieleza kuwa wakati Tanzania inaelekea kwenye hadhi ya kipato cha kati, hitaji la ulinzi thabiti zaidi wa haki miliki linaongezeka.
"Mahakama imeshuhudia ongezeko kubwa la mizozo inayohusiana na miliki bunifu, inayoonyesha uelewa unaokua na utumiaji wa haki za miliki bunifu. Mwenendo huu unasisitiza haja ya Majaji, Mahakimu, na mfumo wa Mahakama ambao unaweza kujibu kwa haraka na kwa haki mashauri ya ukiukaji wa miliki bunifu,” alisema.
Mhe. Prof. Juma alifurahishwa na Majaji na Mahakimu waliofuzu kwa Kozi ya Jumla ya Mafunzo ya Masafa kuhusu Miliki Bunifu inayotolewa na Chuo cha WIPO wanashiriki katika kongamano hilo.
Kwa mfano, alisema, Chuo cha WIPO kilimsajili Jaji Stephen Murimi Magoiga katika Kozi ya Jumla ya Mafunzo ya Masafa kuhusu Miliki Bunifu kwa Majaji kuanzia tarehe 12 Septemba 2023 hadi 06 Novemba 2023.
“Jaji Dk. Paul Kihwelo wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Mhe. Upendo Ngitiri awmekuwa wakinifahamisha kila mara kuhusu mahudhurio ya Majaji na Mahakimu wa Tanzania katika semina za Mahakama kuhusu hakimiliki, alama za biashara na utatuzi mbadala wa migogoro, ambazo WIPO ilitoa," alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushot, (IJA), Mhe. Dkt. Paul Kihwelo, alitoa shukrani kwa WIPO kwa kujitolea kwao na kuwakutanisha majaji kutoka Uingereza, Kenya na Tanzania pamoja na Naibu Wasajili na Mahakimu kutoka Mahakama ya Tanzania.
Mhe. Dk Kihwelo ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, alisema wamekuwa wakifanya hivyo kwa muda mrefu, kwani kuna mafunzo yalifanyika nchini Tanzania na kuna mengine ya masafa ambayo Tanzania ni ya pili Duniani kushiriki katika kozi za kujifunza masafa za WIPO, wakati nchi ya kwanza ni Misri.
"Tumekuwa tukifanya mengi katika mafunzo kwa njia ya mtandaoni nchini Tanzania na Majaji na Mahakimu wamekuwa wakishiriki kikamilifu. Mafunzo ya kwanza yalihusu miliki bunifu, ambapo Majaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Dkt.Theodora Nemboyao Mwenegoha na Mhe. Dk Ubena John Agatho walikuwa miongoni mwa wawezeshaji,” Mhe. Dk.Kihwelo alisema.
Mkurugenzi Msaidizi wa WIPO, Bw. Marco Aleman akizungumza katika kongamano hilo kwa kutumia mkutano mtandao.
Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo, akizungumza katika kongamano hilo.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na meza kuu, wengine (wa pili kulia) ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo, (wa pili kushoto) ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani, (wa kwanza kulia) ni Naibu Jaji wa Mahakama Kuu ya Uingereza, Mhe.Daniel Alexander na (wa kwanza kushoto)Afisa Sheria wa Shirika la Kimataifa na Miliki Bunifu Duniani(WIPO), Bi. Ines Fernandez Ulate.
Meza Kuu ikiwa katika picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania.
Meza Kuu ikiwa katika picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Meza Kuu ikiwa katika picha ya pamoja na Naibu Wasajili.
Akizungumza baada ya uzinduzi huo, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya, alieleza kuwa Mahakama ya Tanzania na Shirika la Miliki Bunifu Duniani (WIPO) kwa pamoja walisaini hati ya makubaliano tarehe 5 Machi, 2021 kwa madhumuni ya kushirikiana katika maeneo mbalimbali yaliyolenga kuboresha utoaji haki kwenye eneo la miliki bunifu “Intellectual Property” na usuluhishi wa migogoro mahakamani.
“WIPO imekuwa ikishirikina na Mahakama ya Tanzania katika maeneo mbalimbali ambayo yamelenga kuboresha utoaji haki katika eneo la miliki bunifu kwa zaidi ya miaka mitano. Kwa mwaka huu wa 2024 ,WIPO kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania imeandaa kongamno hili la Kimataifa la Mahakama kuhusu miliki bunifu na Usimamizi wa Mashauri,” amesema.
Msajili Mkuu amesema kuwa kufanyika kwa Kongamano hilo ni sehemu ya utekelezaji wa Hati ya Makubaliano hayo. Amesema kuwa katika kipindi hiki cha siku mbili za Kongamano, mada mbalimbali zaitawasilishwa na wawezeshaji mahiri waliobobea katika maeneo hayo, ikiwemo Hali ya uendeshaji wa mashauri ya Miliki Bunifu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Picha ya juu na chini ni meza kuu ikiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu.
Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo akiwasilisha mada katika kongamano hilo.
Mratibu wa WIPO Tanzania, Mhe. Upendo Ngitiri akiwasilisha mada.
Mada nyingine ni anuni za Ulinzi wa Alama za Biashara; Uvunjifu wa Alama za Biashara; Kanuni za Ulinzi wa Haki Miliki; Uvunjifu wa Haki Miliki; Mahitaji ya Kiushahidi; Ushahidi wa Kidijitali katika Mashauri ya Alama za Biashara; Hatua za Nafuu za Dharura na Mbinu za Usimamizi wa Mashauri ya Miliki Bunifu.
Mhe.Nkya alitaja mada nyingine kama namna ya Kuharakisha Usikilizaji wa Mashauri ya Miliki Bunifu kwa kuangalia nchi zinazofanya vizuri kama Uingereza na Fursa na Changamoto katika Kuimarisha Usimamizi wa Mashauri ya Miliki Bunifu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.