Jela miaka 50 kwa kubaka, utakatishaji fedha

LINDI-Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi, imewahukumu kwenda jela miaka 30 kwa kosa la ubakaji na miaka 20 kwa kosa la utakatishaji fedha pamoja na kulipa fedha shilingi milioni 35 walizoiba na pia Mahakama imeamuru kutaifishwa kwa mali zao.
Waliohukumiwa ni Kazil Hamis maarufu kama Kaftanyi (43) mkazi wa Dar es Salaam na John Mkondo maarufu kama Kikwete (51) mkazi wa Morogoro.

Hukumu hiyo imetolewa Mei 31, 2024 na Hakimu Mkazi Mfawidhi Consolata Singano wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutolewa hukumu.

Awali jopo la mawakili wa serikali likiongozwa Wakili Godfrey Mramba alidai kuwa,walikuwa na mashahidi 32 na vielelezo 35 vilivyowatia hatiani washtakiwa wote.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka kumi na sita.

Iliendelea kudai kuwa, katika shtaka la kwanza la kula njama ya kutenda kosa la wizi washtakiwa wote walikutwa hawana hatia.

Katika shtaka la pili na la tatu ni kubaka, ilidaiwa kuwa mnamo Machi 1,2022 katika Hoteli ya White Pearl iliyoko mtaa wa Mikumbi katika Wilaya na Mkoa wa Lindi, pasipo na ridhaa washtakiwa waliwabaka mhanga wa kwanza na wa pili (majina yamehifadhiwa) wakiwa katika hali ya kutokujitambua.

Kosa la nne, tano, sita ni wizi ilidaiwa kuwa mnamo Machi 1, 2022 katika Hoteli ya White Pearl iliyoko mtaa wa Mikumbi katika wilaya na mkoa wa Lindi, waliiba pete ya dhahabu yenye uzito wa gramu 12, yenye thamani ya shilingi 1,800,000,

Simu moja ya mkononi aina ya Samsung S7 Edge yenye thamani ya shilingi 1,500,000, kadi ya benki ya CRDB yenye namba 0152....kadi ya benki ya NMB yenye namba za akaunti 20.....na pesa shilingi 300,000 vitu vyote vikiwa na thamani ya shilingi 3,600,000 mali ya mhanga wa kwanza (jina limehifadhiwa).

Pia kati ya Machi Mosi, 2022 katika Hoteli ya White Pearl iliyoko mtaa wa Mikumbi katika Wilaya na Mkoa wa Lindi, waliiba saa moja aina Oriflame, yenye thamani ya shilingi 180,000,

Simu moja ya mkononi aina ya Infinix Hot 11 yenye thamanai ya shilingi 510,000, pesa taslimu shilingi 120,000 vitu vyote vikiwa na thamani ya shilingi 810,000 mali ya mhanga wa pili (jina limehifadhiwa).

Pia iliendelea kudai kuwa kati ya Machi Mosi, 2022 na Machi 02, 2022 katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Lindi na Mtwara, waliiba fedha taslimu kiasi cha shilingi 35,000,000 kwenye akaunti ya benki ya CRDB yenye namba 0152... na Akaunti ya benki ya NMB yenye namba za 2010240.... mali ya Mhanga wa kwanza (jina limehifadhiwa).

Kati ya tarehe zilezile na maeoneo yaleyale washtakiwa kwa pamoja waliiba fedha taslimu kiasi cha shilingi 120,000 kwenye laini ya simu ya Tigo namba.....mali ya mhanga wa pili (jina limehifadhiwa).

Kosa la nane na tisa ni kughushi, ilidai kuwa Mnamo Machi 2, 2022 eneo Mangaka katika Wilaya ya Masasi, Mkoa wa Mtwara, akiwa na nia ya kuhadaa alighushi nyaraka ya uongo ikiwa ni fomu ya kutolea fedha ya benki ya CRDB yenye jina la mhanga wa kwanza ikiwa imejazwa kiasi cha shilingi 4,000,000 akiaminisha kuwa ni ya kweli na ilikua imejazwa na nhanga wa kwanza (jina limehifadhiwa).

Ilidaiwa kuwa tarehe na maeneo yaleyale washtakiwa wote wakiwa na nia ya kuhadaa walighushi nyaraka ya uongo ikiwa ni fomu ya kutolea fedha ya benki ya NMB yenye jina la Mhanga wa kwanza ikiwa imejazwa kiasi cha shilingi 3,000,000 wakiaminisha kuwa ni ya kweli na ilikua imejazwa na Mhanga wa kwanza (jina limehifadhiwa).

Kosa la kumi ni kuwasilisha nyaraka ya uongo, mnamo Machi 2 2022 eneo Masasi katika Wilaya ya Masasi, Mkoa wa Mtwara, kwa makusudi na wakiwa na nia ya kuhadaa waliwasilisha nyaraka ya uongo ikiwa ni fomu ya kutolea fedha ya benki ya NMB yenye jina la Mhanga wa kwanza ikiwa imejazwa kiasi cha shilingi 3,000,000 kwa JASMINI ALLY MOKIWA Wakala wa NMB wakiaminisha kuwa ni nyaraka ya kweli ya kutolea kiasi cha fedha kilizojazwa huku wakijua kitendo hicho si cha si cha kweli.

Pia iliendelea kudai kuwa eneo na tarehe hiyo hiyo washtakiwa kwa makusudi na wakiwa na nia ya kuhadaa waliwasilisha nyaraka ya uongo ikiwa ni fomu ya kutolea fedha ya benki ya NMB yenye jina la Mhanga wa kwanza ikiwa imejazwa kiasi cha Sh 4,000,000 kwa NASSORO SAID SELEMANI wakala wa NMB akiaminisha kuwa ni nyaraka ya kweli ya kutolea kiasi cha fedha kilizojazwa huku akijua kitendo hicho si cha si cha kweli.

Kosa la 12,13,14 ni kutumia laini ya simu iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine, ilidaiwa kuwa KAZIL HAMIS (KAFTANYI) Mnamo Juni 30, 2022 eneo Tegeta Wilaya ya Kinondoni, Mkoa wa Dar es Salaam alitumia laini ya simu yenye namba 07... iliyosajiliwa kwa jina la SHARIFA JONAS HYERA pasipokumjulisha mtoa huduma.

Vilevile alitumia laini ya mtu mwingine inayotambulika kwa jina la JACOB ATUPELE MWANDUMBYA pasipokumjulisha mtoa huduma.

Pia alitumia laini ya simu yenye usajili wa PAULINA ATHANAS MAGANGA pasipokumjulisha mtoa huduma.

Katika kosa la kumi na tano, kutakatisha fedha, ilidaiwa kuwa kabla au baada ya Juni 30, 2022 eneo lisilofahamika katika Mkoa wa Dar es salaam, kwa nia ya kuficha chanzo halisi alitakatisha fedha kiasi cha shilingi millioni 35,000,000 kwa kununulia gari aina ya Toyota Aphard Na. 548 DZQ huku akifahamu fedha hizo ni mazalia ya uhalifu wa wizi.

Kosa la kumi na sita kutakatisha fedha, ilidaiwa kuwa washtakiwa wote kwa pamoja tarehe tofauti kati ya Machi mosi 2022 na Machi 2,2022 maeneo mbalimbali ya mkoa wa Lindi na Mtwara, walijipatia fedha kiasi cha shilingi milioni 35,000,000 huku wakifahamu fedha hizo ni mazalia ya uhalifu wa wizi.

Sambamba na hayo Mahakama imeamuru mshtakiwa wa kwanza na wa pili kuwalipa Mhanga wa kwanza na wa pili fidia ya shilingi millioni tano kwa kila mmoja. Pia kurudisha kiasi cha shilingi milioni 35 kwa mhanga.

Aidha, magari matatu yametaifishwa na kuwa mali ya Serikali ambayo ni TOYOTA ALPHARD T. 548 DZQ, NISSAN DUALIS T. 141 DWA na TOYOTA IST T. 978 DJD, amri imetolewa ya ushahidi kuthibitisha kuwa magari hayo yalitokana na zao la uhalifu.

Vilevile simu na mali zingine walizokutwa nazo washtakiwa zimetaifishwa na kuwa mali ya Serikali.

Pia gari moja TOYOTA IST T531 DVA Mahakama imeamuru lirudishwe kwa mwenyewe (mmiliki) ambaye hakuwa mshtakiwa katika shauri hilo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news