Kamati ya Bunge yatoa saluti kwa NHC utekelezaji wa Samia Housing Scheme, Morocco Square na 7/11

NA GODFREY NNKO

WAJUMBE wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii wameridhishwa na utekelezaji wa miradi ya Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) ambayo ipo katika hatua za umaliziaji na mingine ikiendelea kujengwa jijini Dar es Salaam.
Kutokana na ufanisi wa miradi hiyo ambayo inajumuisha Samia Housing Scheme uliopo Tanganyika Packers Kawe, Mradi wa 7/11 uliopo Kawe na Morocco Square, kamati imesema ni hatua muhimu kwa ustawi wa shirika na Taifa kwa ujumla.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo,Timotheo Mzava ameyasema hayo leo Juni 30,2024 baada ya kamati hiyo kutembelea miradi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.

"Sisi kama Kamati ya Bunge tumefurahi na tumeridhishwa na utekelezaji wa miradi hii. Na katika hii miradi mitatu, kuna mradi mmoja muhimu sana wa Samia Housing Scheme ambao unakwenda kuacha legacy kwa Rais wa Awamu ya Sita, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.

"Kama mnavyokumbuka katika hii miradi miwili kwa maana ya Morocco Square na 7/11 ilikuwa imekwama."

Mheshimiwa Mzava amesema, baada ya Mheshimiwa Rais Dkt.Samia kuona tatizo hilo alitoa kibali ili shirika lipate fedha liweze kuikwamua miradi hiyo na matokeo mazuri yameonekana, kwani miradi hiyo ipo katika hatua nzuri huku Morocco Square ukiwa umeanza kutoa huduma kwa baadhi ya maeneo.

"Kwa hiyo, kama kamati tumeridhika, lakini tumebaini kazi hii isingefanyika vizuri kama siyo nia, kama siyo moyo,kama siyo mtazamo na maono aliyonayo Mheshimiwa Rais hasa kwa kutoa kibali kwa Shirika la Nyumba kupata fedha ili kukamilisha miradi hii.
"Kwa hiyo, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kazi yake nzuri na kwa kuliruhusu shirika liweze kupata fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi hii, vile vile nilipongeze Shirika la Nyumba kwa usimamizi mzuri wa miradi hii."

Mheshimiwa Pinda

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Geophrey Pinda amesema, wanamahukuru Rais Dkt.Samia kwa kuridhia miradi hiyo kuendelea kwani hapo awali ilisimama kwa muda kupisha mambo ya kiserikali, lakini sasa mambo ni mazuri.

"Tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuridhia miradi hii kuendelea, na kwa sasa, jengo la Morocco Square limekamilika."

Amesema, eneo la Morocco ambalo lilikuwa linakaliwa na watu watatu, baada ya uwekezaji huo wa NHC, eneo hilo sasa litakuwa na makazi mengi ikiwemo vitega uchumi vya kutosha.

Pia, amesema wataendelea kusimamia maelekezo ya Rais Dkt.Samia ili kuhakikisha miradi hiyo inamalizika kwa wakati na kuhakikisha inaleta tija kwa wananchi, shirika na Taifa kwa ujumla.

NHC

Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah amesema, shirika linaendelea na mpango wa ujenzi wa nyumba 5,000 za gharama ya kati na chini kupitia mradi wa Samia Housing Scheme (SHS) ambao utekelezaji wake unaendelea.
Mradi huu wa nyumba za kuuza na kupangisha unakusudia kuenzi kazi nzuri anazofanya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo kuwezesha upatikanaji wa nyumba bora nchini.

"Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amekuja kulikwamua Shirika la Taifa la Nyumba, miradi hii ilikuwa imekwama. Moja ya miradi iliyokuwa imekwama au miwili tunayoitembelea leo, mmoja ni 7/11 na Mradi wa Morroco Square.

"Sisi kama Shirika la Nyumba la Taifa tumesema, sasa Rais wetu tunamuachia legacy kivipi kwa kazi nzuri ambayo ameifanya kwa shirika, tukasema sisi kama shirika tutajenga nyumba 5,000 nchini za Samia Housing Scheme."

Amesema,asilimia 50 ya nyumba hizo zitajengwa katika Mkoa wa Dar es Salaam, asilimia 20 katika mkoa wa Dodoma na asilimia 30 zitajengwa katika mikoa mingine nchini.

Pia, amesema mradi huu utakaokuwa na nyumba 5,000 unaotekelezwa kwa awamu, utagharimu shilingi bilioni 466 sawa na Dola za Kimarekani milioni 200.

"Katika kuendeleza mradi huu, maandalizi ya ujenzi wa Mradi wa Samia Housing Scheme wenye nyumba 100 jijini Dodoma na nyumba 560 eneo la Kawe awamu ya pili yanaendelea kukamilishwa.

"Nyumba 560 zinaendelea kujengwa katika eneo hili la Kawe, Dar es Salaam ambapo hadi kufikia leo Juni 30, 2024, ujenzi umefikia asilimia 65.

"Mradi huu wa Kawe utagharimu shilingi bilioni 48.27 na hadi sasa shilingi bilioni 21.88 zimeshatumika."

Mkurugenzi Mkuu huyo amesema, mauzo ya mradi huo yamefikia asilimia 100 na shirika limeshapokea malipo ya awali ya kiasi cha shilingi bilioni 31.2 na kiasi kilichobakia cha shilingi bilioni 45.5 kinaendelea kukusanywa.
Kuhusu, Mradi wa Morocco Square, Mkurugenzi Mkuu wa NHC amesema, umeshakamilika kwa asilimia 99 na shughuli za upangishaji wa eneo la hoteli yenye vyumba 81 umekamilika na eneo la ofisi na biashara upangishaji unaendelea kukamilishwa.

"Aidha, jengo lenye nyumba za makazi 100, tayari nyumba 71 zimeshauzwa na mauzo ya nyumba zilizobakia yanaendelea."

Amesema,katika nyumba za makazi na biashara zilizouzwa, shirika hilo limekusanya shilingi bilioni 30 na kiasi cha shilingi bilioni 35.9 kinaendelea kukusanywa.

"Eneo la maduka (mall) limeshapangishwa kwa asilimia 98 na kwa sasa upangaji wa bidhaa unaendelea ili kufungua maduka hayo mwezi Julai, 2024."

Vile vile, kwa upande wa mradi wa 7/11 amesema, mradi huo wenye nyumba 422 pamoja sehemu ya biashara wa Kawe 7/11 ulianza Novemba 2014 na ulisimama 2018.

Amesema,mkandarasi alirejea kuendelea na ujenzi Januari, 2024 ambaye ni Estim Construction Company Limited kwa gharama ya shilingi bilioni 169.9 na kwa sasa ujenzi umefikia asilimia 40.

"Mradi unatarajiwa kukamilika mwezi Aprili, 2026. Mauzo ya nyumba katika mradi huu yanaendelea ambapo shirika limekusanya shilingi bilioni 2.9 na litazindua rasmi mauzo ya mradi huu Julai, 2024."

Hata hivyo, amewataka Watanzania kuchangamkia fursa za manunuzi ya nyumba hizo kwani, anayefanya malipo mapema ndiye anapata nafuu kubwa kuliko anayesubiria mradi ukamilike.

DC Kinondoni

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mheshimiwa Saad Mtambule amelipongeza Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) kwa uwekezaji huo ambao amesema, licha ya kupendezesha mandhari ya wilaya hiyo pia, imefungua fursa nyingi za ajira, makazi bora, vitega uchumi, vyanzo vya mapato kwa Serikali, watoa huduma na shirika kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news