●Atembelea migodi midogo ya uzalishaji na uchenjuaji dhahabu
●Apokea changamoto za wachimbaji wadogo.
MBEYA-Katibu Mkuu Wizara ya Madini,Kheri Mahimbali Juni 9, 2024 amekamilisha ziara yake katika Mkoa wa Kimadini Chunya kwa kutembelea migodi ya wachimbaji wadogo wa dhahabu wilayani Chunya mkoani Mbeya.
Katika ziara hiyo Katibu Mkuu Mahimbali amekamilisha kwa kutembelea migodi mbalimbali ya uchimbaji pamoja na kuona jinsi uchenjuaji wa madini ya dhahabu unavyofanyika katika eneo la Makongolosi na Itumbi.
Sambamba na ziara hiyo, Mahimbali amepokea Taarifa ya Uchimbaji na Uchenjuaji wa Madini ya Dhahabu pamoja na Hali ya Ushirikishwaji wa Jamii kutoka katika kampuni ya Apex Resources Ltd na Xepa Resources Ltd zinazojishughulisha na uchimbaji wa madini ya dhahabu katika eneo la Itumbi wilayani Chunya.
Katika ziara hiyo, Mahimbali amepata fursa ya kuzungumza na wachimbaji wadogo katika eneo la Itumbi na kupokea changamoto mbalimbali zinazowakabili katika shughuli zao za uchimbaji madini.
Ziara hiyo maalum yenye lengo la kutembelea maeneo mbalimbali ya uchimbaji na uchenjuaji imejumuhisha watendaji kutoka Wizara ya Madini na Taasisi zake.