DODOMA-Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri amewataka wahandisi washauri wa mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda katika Jiji la Dodoma kuhakikisha wanazingatia weledi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Agizo hilo amelitoa leo katika kikao cha maandalizi ya Upembuzi Yakinifu, Usanifu wa Kina wa mradi na Uandaaji wa Makabrasha ya zabuni kilichofanyika jijini Dodoma katika ofisi za wizara zilizoko Mji wa Serikali Mtumba.
Amesema, wananchi wa Dodoma wamesubiri kwa muda mrefu utekelezaji wa mradi huo, sasa ni muda muafaka wa kuanza kuona matunda ya Serikali ambayo kwa muda wote imejipambanua kama serikali ya wananchi.
Amesema, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameelekeza wizara kuhakikisha mradi huo unaanza ili kuondoa kabisa changamoto ya huduma ya maji katika Jiji la Dodoma ambalo ni makao makuu ya nchi.
Aidha, amesisitiza ushirikishwaji wa kutosha wa wataalamu wa wizara ili kuongeza maarifa na uelewa wa kutosha wa miradi mikubwa ya maji.
Wataalamu washauri waliopewa jukumu la mradi wa ziwa Victoria kweda Dodoma ni Dong Myeong Engineering Consultants kutoka Korea Kusini pamoja na kampuni za Tanzania ambazo ni Don Consult LTD na Supelit Consulting LTD.