Kigoma wahimizwa kujitokeza kwa wingi uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura nchini

KIGOMA-Wananchi mkoani Kigoma wamehimizwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao wakati wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linalotarajiwa kuzinduliwa mkoani humo tarehe 01 Julai, 2024.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele wakati akifungua mkutano wa wadau wa uchaguzi wa mkoa wa Kigoma uliofanyika leo tarehe 19 Juni, 2024 katika Halmashauri ya Kigoma Ujiji.
Jaji Mwambegele amewapongeza wadau wa uchaguzi na wananchi kwa ujumla kwenye mkoa wa Kigoma kwa mkoa wao kuteuliwa kuwa sehemu ya uzinduzi wa uboreshaji huo ambao utafanyika kwenye uwanja wa Kawawa uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB).

“Uboreshaji wa daftari utazinduliwa hapa mkoani Kigoma tarehe 01 Julai, 2024 na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB). Tayari Tume imeamua kwamba uzinduzi huo ufanyike katika uwanja wa Kawawa uliopo hapa kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji,” amesema Mhe. Mwambegele.
Ameongeza kuwa,Tume ilifikia uamuzi wa kufanya uzinduzi huo kwenye mkoa wa Kigoma baada ya kuzingatia mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa mwamko mkubwa wa wananchi kujitokeza kwenye uboreshaji wa Daftari uliofanyika mwaka 2019/20.

“Ni matarajio ya Tume kuwa mtakuwa mabalozi wazuri wa kusambaza taarifa na kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao ili kuendeleza sifa hii ya mwamko wa wananchi kujitokeza kwa wingi,” amewaambia wadau hao.

Amesema, uzinduzi wa uboreshaji wa Daftari utatanguliwa na shughuli mbalimbali za uhamasishaji ikiwa ni pamoja na matangazo na tamasha la uborshaji wa Daftari ambalo litafanyika siku ya Ijumaa tarehe 28 Juni, 2024 kwenye uwanja wa Kawawa.

Wakati akiwasilisha mada, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima, R. K amesema uboreshaji kwa awamu hii ya kwanza utafanyika kwenye mizunguko 13 na kuongeza kwamba baada ya mkoa wa Kigoma uboreshaji utaendelea kwenye mikoa ya Katavi na Tabora.
“Zoezi hili litaendeshwa kwa siku saba kwenye kila kituo cha kuandikisha wapiga kura. Tunatarajia zoezi litakamilika Machi, 2025,” amesema Bw. Kailima.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news