NA GODREY NNKO
SERIKALI imesema, mwaka 2023, Pato ghafi la Taifa (kwa bei za mwaka husika) lilikuwa shilingi bilioni 188,588.05 ikilinganishwa na shilingi bilioni 170,820.03 mwaka 2022.
Aidha, Tanzania Bara ilikuwa na wastani wa watu 61,718,700 mwaka 2023 ikilinganishwa na watu 59,851,347 mwaka 2022.
Hivyo, Pato la Taifa kwa Mtu (GDP per capita) mwaka 2023 lilikuwa wastani wa shilingi 3,055,606 ikilinganishwa na shilingi 2,854,072 mwaka 2022, sawa na ongezeko la asilimia 7.1.
Kiasi hicho ni sawa na dola za Marekani 1,275.5 kwa mtu mwaka 2023 ikilinganishwa na dola za Marekani 1,233.1 kwa mtu mwaka 2022.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Alexander Mkumbo ameyasema hayo leo Juni 13, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya uchumi wa nchi kwa mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2024/25.
Amesema, mwaka 2023, ukuaji wa shughuli za kilimo ambazo zinajumuisha kilimo cha mazao, mifugo, misitu na uvuvi ulikuwa asilimia 4.2 ikilinganishwa na asilimia 3.3 mwaka 2022.
Waziri Prof.Mkumbo amesema,ongezeko hilo lilitokana na Serikali kutoa ruzuku ya mbolea na hivyo kuwezesha wakulima kupata mbolea kwa bei nafuu pamoja na upatikanaji wa mvua za kutosha na za wakati katika maeneo mengi ya uzalishaji.
Pia, shughuli za mifugo zilikuwa na kiwango kikubwa cha ukuaji cha asilimia 5.0 ikifuatiwa na misitu asilimia 4.3, uzalishaji mazao asilimia 4.2 na uvuvi asilimia 1.4 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 5.0, asilimia 3.1, asilimia 2.7 na asilimia 1.9 mtawalia mwaka 2022.
"Mwaka 2023, shughuli za kilimo sehemu ya kuuza ilikuwa na ukuaji wa asilimia 4.2 na sehemu isiyo ya kuuza asilimia 4.5 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 3.3 kwa sehemu ya kuuza na asilimia 3.5 sehemu isiyo ya kuuza mwaka 2022.
"Aidha, sehemu ya kuuza kwa shughuli za mifugo ilikua kwa asilimia 5.0, misitu asilimia 4.3, uzalishaji mazao asilimia 4.2 na uvuvi asilimia 1.4 kama ilivyokuwa kwa sehemu isiyo ya kuuza."
Mwaka 2023, mchango wa shughuli za kilimo, Waziri Prof.Mkumbo amesema, katika Pato la Taifa ulikuwa asilimia 26.5 ikilinganishwa na asilimia 26.2 mwaka 2022.
Huku shughuli ndogo za mazao zilichangia asilimia 16.1 katika Pato la Taifa, mifugo asilimia 6.2, misitu asilimia 2.5 na uvuvi asilimia 1.7 mwaka 2023 ikilinganishwa na mchango wa asilimia 15.0, asilimia 6.7, asilimia 2.7 na asilimia 1.8 mtawalia mwaka 2022.
Waziri Prof.Mkumbo amebainisha kuwa, mwaka 2023, kiwango cha ukuaji wa shughuli za uchimbaji madini na mawe kilikuwa asilimia 11.3 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 10.8 mwaka 2022.
"Ukuaji huo ulitokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa madini, hususan makaa ya mawe, jasi, chumvi, almasi, mawe ya chokaa na shaba.
"Aidha, mchango wa shughuli za uchimbaji madini na mawe kwenye Pato la Taifa ulikuwa asilimia 9.0 mwaka 2023 kama ilivyokuwa mwaka 2022."
Mwaka 2023, kiwango cha ukuaji wa shughuli za uzalishaji bidhaa viwandani kilikuwa asilimia 4.3 ikilinganishwa na asilimia 4.2 mwaka 2022.
Ukuaji huo ulichangiwa na kuongezeka kwa mahitaji ya bidhaa za viwandani hususan katika soko la ndani kufuatia mwitikio wa wananchi kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini.
Aidha, mchango wa shughuli za uzalishaji bidhaa viwandani katika Pato la Taifa ulikuwa asilimia 7.0 mwaka 2023 ikilinganishwa na asilimia 7.1 mwaka 2022.
Mheshimiwa Waziri Prof.Mkumbo amesema, mwaka 2023, kiwango cha ukuaji wa shughuli za ufuaji, usafirishaji na usambazaji umeme kilikuwa asilimia 3.9 ikilinganishwa na asilimia 7.6 mwaka 2022.
"Kupungua kwa kasi ya ukuaji kulitokana na uchakavu wa njia za kusambaza umeme zilizosababisha upotevu wa umeme wakati wa usafirishaji pamoja na kuzimwa kwa baadhi ya mitambo ili kupisha ukarabati wa miundombinu ya usafirishaji.
"Mchango wa shughuli za umeme kwenye Pato la Taifa ulikuwa asilimia 0.02 ikilinganishwa na asilimia 0.15 mwaka 2022.
"Mwaka 2023, kiwango cha ukuaji wa shughuli za usambazaji maji na udhibiti majitaka kilikuwa asilimia 2.5 ikilinganishwa na asilimia 5.5 mwaka 2022.
"Hii ilichangiwa na uharibifu wa miundombinu ya maji kutokana na mabadiliko ya tabianchi yaliyosababisha mvua zilizozidi wastani katika baadhi ya maeneo."
Kwa upande wa mchango wa shughuli za usambazaji maji na udhibiti majitaka katika Pato la Taifa ulikuwa asilimia 0.5 mwaka 2023 kama ilivyokuwa mwaka 2022.
Aidha, shughuli za usambazaji maji na udhibiti wa majitaka kwa sehemu 5 inayouzika na isiyouzika zilikua kwa asilimia 2.5 mwaka 2023 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 5.5 mwaka 2022.
Mwaka 2023, amesema shughuli za ujenzi zilikua kwa asilimia 3.5 ikilinganishwa na asilimia 3.9 mwaka 2022.
Ukuaji huo, Mheshimiwa Waziri Pro.Mkumbo amesema, ulichangiwa na kuendelea kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya barabara, madaraja, viwanja vya ndege, reli, ofisi za Serikali, madarasa, vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na nyumba za makazi na biashara.
Kwa upande mwingine, shughuli za ujenzi sehemu inayouzika ilikua kwa asilimia 3.7 na sehemu isiyouzika ilikuwa na ukuaji hasi wa asilimia 1.6 mwaka 2023.
Pamoja na kasi ndogo ya ukuaji, shughuli za ujenzi ni za pili kwa kuwa na mchango mkubwa katika Pato la Taifa wa asilimia 13.2 mwaka 2023 ikilinganishwa na asilimia 13.7 mwaka 2022.
"Mwaka 2023, kiwango cha ukuaji wa shughuli za biashara na matengenezo kilikuwa asilimia 4.2 ikilinganishwa na asilimia 3.9 mwaka 2022.
"Ukuaji huo ulichangiwa na kuendelea kuboreshwa kwa mazingira ya ufanyaji biashara nchini, kuimarika kwa upatikanaji wa mikopo kwa sekta binafsi pamoja na kuimarika kwa biashara za kikanda baada ya kulegezwa kwa vikwazo vya kibiashara.
"Aidha, mchango wa shughuli za biashara na matengenezo katika Pato la Taifa ulikuwa asilimia 8.3 mwaka 2023 ikilinganishwa na asilimia 8.2 mwaka 2022.
"Mwaka 2023, shughuli za huduma za malazi na chakula zilikua kwa asilimia 8.3 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 9.0 mwaka 2022.
"Ukuaji huo ulichangiwa na kuendelea kuimarika kwa shughuli za kiuchumi, hususan utalii kufuatia hatua zilizoendelea kuchukuliwa na Serikali ikiwemo utangazaji wa utalii kupitia Programu ya Tanzania-The Royal Tour na uboreshwaji wa miundombinu ya utalii.
"Aidha, mchango wa shughuli za huduma za malazi na chakula katika Pato la Taifa ulikuwa asilimia 1.2 mwaka 2023 ikilinganishwa na asilimia 1.1 mwaka 2022."
Amesema, mwaka 2023, shughuli za usafirishaji na uhifadhi mizigo zilikua kwa asilimia 4.1 ikilinganishwa na asilimia 3.8 mwaka 2022.
Ukuaji huo ulitokana na kuongezeka kwa usafirishaji wa abiria na shehena za mizigo iliyohudumiwa katika bandari na kusafirishwa kwa njia ya barabara, reli na anga.
Mchango wa shughuli hizo katika Pato la Taifa uliongezeka na kufikia asilimia 7.2 mwaka 2023 ikilinganishwa na asilimia 6.7 mwaka 2022.
Vile vile, shughuli za habari na mawasiliano ambazo zinajumuisha huduma za utayarishaji, uchapishaji na usambazaji wa taarifa mbalimbali kupitia vyombo vya habari kama vile radio, magazeti, runinga, tovuti pamoja na huduma za mawasiliano kwa njia ya simu zilionesha ukuaji.
"Mwaka 2023, shughuli hizo zilikua kwa asilimia 7.6 ikilinganishwa na asilimia 7.4 mwaka 2022.
"Ukuaji huu ulitokana na kuongezeka kwa matumizi ya huduma za simu za viganjani na mitandao ya kijamii nchini katika kuwasiliana na kupata habari na matukio mbalimbali."
Amesema, kuongezeka kwa matumizi ya njia za mitandao katika kufanya mikutano, pamoja na kuongezeka kwa idadi ya wateja waliopata huduma za fedha kupitia mitandao ya simu na huduma za utangazaji na inteneti ni sehemu ya mafanikio.
Aidha, mchango wa shughuli hizo katika Pato la Taifa, Waziri Prof.Mkumbo amesema, ulikuwa asilimia 1.4 mwaka 2023 ikilinganishwa na asilimia 1.5 mwaka 2022.
Kwa mwaka 2023, shughuli za huduma za fedha na bima zilikua kwa asilimia 12.2 ikilinganishwa na asilimia 9.2 mwaka 2022.
Waziri Mkumbo amesema, ongezeko hilo lilitokana na kuongezeka kwa kiwango cha amana na mikopo kwa sekta binafsi.
Pia, kupungua kwa mikopo chechefu, kupanuka kwa huduma za shughuli za bima pamoja na kuimarika kwa shughuli za kiuchumi kulikochangia kuongezeka mahitaji ya huduma za fedha.
"Mchango wa shughuli za huduma za fedha na bima katika Pato la Taifa ulikuwa asilimia 4.5 mwaka 2023 ikilinganishwa na asilimia 3.7 mwaka 2022."
Wakati huo huo, Waziri amesema, mwaka 2023, shughuli za upangishaji majengo zilikua kwa asilimia 4.3 ikilinganishwa na asilimia 4.4 mwaka 2022.
Amesema, ukuaji huo ulitokana na kuendelea kuongezeka kwa mahitaji ya nyumba kwa ajili ya makazi, biashara na ofisi, hususan maeneo ya mijini.
Aidha, shughuli za upangishaji majengo kwa sehemu inayouzika na sehemu isiyouzika zilikua kwa asilimia 4.3 mwaka 2023.
Vile vile, mchango wa shughuli hizo katika Pato la Taifa ulikuwa asilimia 2.7 mwaka 2023 ikilinganishwa na asilimia 2.8 mwaka 2022.
"Mwaka 2023, shughuli za utawala wa umma na ulinzi zilikua kwa asilimia 5.5 ikilinganishwa na asilimia 5.4 mwaka 2022.
"Ukuaji huo ulitokana na kuongezeka kwa ulipaji wa malimbikizo ya madai ya wafanyakazi, utekelezaji wa kazi za ulinzi na usalama na uendeshaji wa shughuli za Serikali.
"Hata hivyo, mchango wa shughuli hizo katika Pato la Taifa ulipungua kufikia wastani wa asilimia 3.5 mwaka 2023 ikilinganishwa na asilimia 3.7 mwaka 2022."
Amesema, mwaka 2023, ukuaji wa shughuli za huduma za utawala na usaidizi ulikuwa asilimia 5.0 ikilinganishwa na asilimia 4.6 mwaka 2022.
Shughuli hizo zinajumuisha ukodishaji wa vifaa, mashine na mitambo, utafutaji wa ajira, huduma za utalii, utoaji huduma ofisini, uwakala wa kampuni za usafiri na haki ya kutumia matokeo ya kitaaluma.
Mchango wa shughuli hizo katika Pato la Taifa ulikuwa asilimia 2.6 mwaka 2023 ikilinganishwa na asilimia 2.5 mwaka 2022.
"Mwaka 2023, ukuaji wa shughuli za utoaji huduma za elimu ulikuwa asilimia 6.2 ikilinganishwa na asilimia 5.3 mwaka 2022.
"Ukuaji huo ulitokana na juhudi za Serikali kwa kushirikiana na wadau katika kuboresha miundombinu ya elimu, kuongezeka kwa udahili wa wanafunzi katika shule za msingi na sekondari pamoja na kuajiri waalimu.
"Aidha, shughuli za huduma za elimu zilichangia asilimia 2.2 katika Pato la Taifa mwaka 2023 kama ilivyokuwa mwaka 2022."
Kwa upande mwingine, Waziri Prof.Mkumbo amesema, shughuli za kitaaluma, sayansi na ufundi zilikua kwa asilimia 5.5 mwaka 2023 ikilinganishwa na asilimia 5.8 mwaka 2022.
Vile vile, mchango wa shughuli hizo katika Pato la Taifa ulikuwa asilimia 0.7 mwaka 2023 kama ilivyokuwa mwaka 2022.
"Shughuli za huduma za afya na maendeleo ya jamii zilikua kwa asilimia 6.0 mwaka 2023 ikilinganishwa na asilimia 5.4 mwaka 2022.
"Ukuaji huo ulitokana na kuendelea kuboreshwa kwa utoaji wa huduma za afya kwa jamii katika ngazi zote za kutolea huduma.
"Aidha, mchango wa shughuli za huduma za afya na maendeleo ya jamii katika Pato la Taifa ulikuwa asilimia 1.4 mwaka 2023 kama ilivyokuwa mwaka 2022.
"Mwaka 2023, shughuli za sanaa na burudani ndizo zilikuwa na kiwango kikubwa cha ukuaji wa asilimia 17.7 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 19.0 mwaka 2022.
"Ukuaji huo ulitokana na kuendelea kuimarika kwa mauzo ya bidhaa za kitamaduni kwa watalii na kuboreshwa kwa mazingira ya biashara ya tasnia ya burudani."
Aidha, mchango wa shughuli hizo katika Pato la Taifa, Waziri Prof.Mkumbo amesema, ulikuwa kwa asilimia 0.4 mwaka 2023 kama ilivyokuwa mwaka 2022.
"Mwaka 2023, ukuaji wa shughuli za kaya binafsi katika kuajiri ulikuwa asilimia 3.1 kama ilivyokuwa mwaka 2022."
Aidha, mchango wa shughuli hizo katika Pato la Taifa ulikuwa asilimia 0.2 kama ilivyokuwa mwaka 2022.
Kwa upande mwingine, shughuli za huduma nyingine zilikua kwa asilimia 6.7 mwaka 2023 ikilinganishwa na asilimia 5.7 mwaka 2022.
"Mchango wa shughuli hizo katika Pato la Taifa ulikuwa asilimia 0.8 mwaka 2023 ikilinganishwa na asilimia 0.9 mwaka 2022."