Kukopa jambo la heri

NA LWAGA MWAMBANDE

KWA mujibu wa mtaalamu wa masuala ya Elimu ya Fedha, Uwekezaji na Ushauri wa Kibiashara, Kumbuael Kaaya kupitia maandiko yake mitandaoni anabainisha kuwa,mkopo ni fedha ambayo taasisi za fedha au za mikopo zinatoa kwa wateja wake ili kukidhi mahitaji ya msingi au mtaji na kwa ajili ya kuboresha biashara au kutekeleza miradi.
Picha na freshbooks.

Vile vile anabainisha kuwa,pia ni fedha ambayo mkopaji anaweza kuitumia katika kipindi cha muda mfupi au ndani ya kipindi cha muda fulani, ambapo atatakiwa kufanya marejesho kulingana na riba au gharama waliyokubaliana na mkopeshaji.

Ikumbukwe, fedha hii ni mkopo wa amana na hisa za wateja katika kutoa huduma ya fedha. Kwa hiyo mkopo una gharama zake kupitia riba na gharama za uandaaji.

Mkopo si mali ya benki bali ni mali ya wateja wa benki ambapo benki inasimamia fedha za wateja na kuwa mdhamini kwa wateja wanaoomba mikopo.

Mkopeshaji anaweza kuwa taasisi za Kimataifa,benki,taasisi za mikopo au mtu binafsi.

Sababu za kuchukua mkopo ni pamoja na kuutumia katika uwekezaji, kushughulikia ama kutatua mambo ya dharura ikiwemo utekelezaji wa miradi mbalimbali.

Zingatia kuwa, kukopa sio tatizo wala sio roho ya umasikini. Matajiri wengi wanakopa na kutumia hela za wengine kuzalisha. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa,kwa maendeleo bora, kukopa ni jambo la heri. Endelea;

1.Maskini huwa hakopi, hana kitu cha kulipa,
Tusijione wafupi, vile tunakopakopa,
Tuna mali si makapi, tunakopa na kulipa.
Kwa maendeleo bora, kukopa jambo la heri.

2.Inafanywa tathmini, kama twataka kukopa,
Tena ni kwa umakini, kwamba twaweza kulipa,
Tukiujua undani, kwa raha zetu twakopa,
Kwa maendeleo bora, kukopa jambo la heri.

3.Nenda kote duniani, wanaoweza kukopa,
Ni wale wenye madini, wanakopesheka hapa,
Lakini walio duni, kukopa shida kulipa,
Kwa maendeleo bora, kukopa jambo la heri.

4.Nchi zinakopa sana, kiuchumi zinalipa,
Za maendeleo sana, wanakopa wanalipa,
Hapo hakuna hiana, wamejiwekea chapa,
Kwa maendeleo bora, kukopa jambo la heri.

5.Nchi kama Marekani, tajiri sana kukopa,
Japo kama i angani, uchumi unavyolipa,
Ndivyo kote duniani, nchi zinakopakopa,
Kwa maendeleo bora, kukopa jambo la heri.

6.Japani Ujerumani, tajiri ila zakopa,
Ni mtindo duniani, ambao kweli walipa,
Ni nchi zilizo duni, vigumu sana kukopa,
Kwa maendeleo bora, kukopa jambo la heri.

7.Si Kenya au Uganda, hata Rwanda wanakopa,
Kukopa siyo kupinda, limradi utalipa.
Ili uchumi kupanda, harakisha kwa kukopa,
Kwa maendeleo bora, kukopa jambo la heri.

8.Vivyo hata Tanzania, tunaiona yakopa,
Yafanya hivyo kwa nia, vile yaweza kulipa,
Fedha hizo yatumia, miradi inayolipa,
Kwa maendeleo bora, kukopa jambo la heri.

9.Deni likiongezeka, kwa sababu tunakopa,
Wala tusijeteseka, bora liwe lalipika,
Na fedha zikatumika, miradi inayolipa,
Kwa maendeleo bora, kukopa jambo la heri.

10.Hapa tuna kazi nyingi, ngumu kuvunja mfupa,
Bila kuupiga mwingi, kwa kuamua kukopa,
Tusingejenga msingi, kesho yetu iwe supa,
Kwa maendeleo bora, kukopa jambo la heri.

11.Hii reli mwendokasi, yajengeka kwa kukopa,
Jambo chanya siyo hasi, tunaona hapahapa,
Safari za mwendokasi, zimekwishafika hapa,
Kwa maendeleo bora, kukopa jambo la heri.

12.Toka Dare tu Dodoma, saa tatu zinalipa,
Kama mtu ajituma, kwa haraka atachupa,
Kazi azifanye vema, zile kwake zinalipa,
Kwa maendeleo bora, kukopa jambo la heri.

13.Bwawa kubwa la umeme, limeshaanza kulipa,
Hayo mambo tuyasome, tusilalame kukopa,
Acha uchumi uvume, tuzalishe tutalipa,
Kwa maendeleo bora, kukopa jambo la heri.

14.Muhimu uhimilivu, mikopo tunayojopa,
Matumizi endelevu, yale yatayotulipa,
Huo hasa ni werevu, sawa kuvunja mfupa,
Kwa maendeleo bora, kukopa jambo la heri.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news