DODOMA-Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametoa wito kwa Idara na Vitengo vya Mazingira katika wizara na taasisi za Serikali kuendelea kutekeleza majukumu yao ya msingi yanayolenga kuleta suluhisho la athari za mazingira nchini.

“Nataka nisisitize jambo hili muhimu sana kila wizara ina Kitengo cha Mazingira ni bahati mbaya kumbe kuna wakati vitengo hivi katika wizara na taasisi vimewekwa watu ambao wanadhani ni kama hawana shughuli ya kufanya, hawatengewi bajeti na hivyo hakuna shughuli ya kufanya, kazi hii imeachwa kwenye Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira pekee.
“Imefika mahali ukitaka kujua kuhusu mazingira basi umuone Waziri wa Mazingira peke yake wakati kila wizara ina Kitengo cha Mazingira na wajibu wake ni kuhakikisha kwamba mazingira yanahifadhiwa hata hapa kwenye uzinduzi wa mabanda ya maonesho vitengo vya baadhi ya wizara na taasisi havipo hapa wanadhani wana majukumu kuliko mazingira.”

Pia, Dkt. Biteko amesema kuwa kutunza mazingira si kupanda miti tu bali kulinda na kuhifadhi ni jambo muhimu na lenye gharama zaidi. Aidha, ametoa wito kwa watendaji wa wizara ambao Vitengo vyao vya Mazingira havikushiriki Maonesho hayo ya Wiki ya Mazingira vijulikane ili vielezwe namna ya kutekeleza majukumu yao.
Vilevile, Dkt. Biteko ametoa rai kwa Watanzania kushiriki kwa wingi katika kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Mazingira kitakachofanyika Juni 5, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete uliopo jijini Dodoma ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Dkt. Philip Isdory Mpango.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule amesema kuwa mkoa wake umeendelea kutekeleza maagizo na shughuli mbalimbali zinazolenga kutunza mazingira na kuwa waliweka azimio la kuhakikisha wanatenga maeneo ya kuuza hewa ya ukaa na tayari Wilaya ya Mpwapwa imefanikiwa kukidhi vigezo vilivyowekwa katika kufanya biashara hiyo ikiwa ni sehemu ya utunzaji wa mazingira.