MOROGORO-Idara ya Ukaguzi na Biashara ya Madini imetakiwa kufanya kazi kwa uwajibikaji na ushirikiano.
Akifungua kikao kazi cha kuwajengea uwezo Watumishi wa Kurugenzi ya Ukaguzi na Biashara ya Madini mkoani Morogoro, Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini, Andrew Mgaya amesema, lengo ni kukutana ili kujengeana uwezo ili kuwa wabunifu katika kuongeza makusanyo na kufikia lengo la shilingi bilioni 999 kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Amesema, nia ya kuwepo kwa kikao hiki ni kuboresha utendaji kazi wa Idara pamoja na kujengeana uwezo katika masuala mbalimbali hasa utekelezaji wa mpango kazi wa sehemu kwa mwaka wa fedha 2023/2024 na mpango kazi kwa mwaka 2024/2025.
“Kikao hiki kiwe ni chachu ya kufika mbali ki Idara tuwajibike katika kazi zetu, tushirikiane kwa pamoja na kufanya kazi kwa weledi ili tufikie lengo tulilojiwekea ,”amesema Mgaya.
Pia, amewaomba Watumishi wa Idara ya Ukaguzi na Biashara ya Madini kusikiliza kwa umakini mada na mafunzo ili kuleta matokeo chanya kwa mwaka ujao wa fedha.