Mahakama Musoma yavuka mwaka 2023 bila mrundikano wa mashauri

NA FAUSTINE KAPAMA

MAHAKAMA ya Tanzania, Kanda ya Musoma imefanikiwa kusikiliza mashauri yote ya muda mrefu na kuvuka mwaka 2023 bila mrundikano, hivyo kutekeleza kwa vitendo jukumu la utoaji haki kwa wakati kwa wananchi.
Hayo yamebainishwa na Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Salome Abubakar Mshasha alipokuwa anaongea na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania, Ndg. Gerald Chami alipofanya ziara hivi karibuni.

“Tumefanikiwa kuendesha vikao tisa kati ya 10 vilivyopangwa kufanyika katika mwaka wa fedha 2023/2024. Hadi kufikia mwezi Mei 2024 kilikuwa kimebaki kikao kimoja tu kinachotarajiwa kufanyika mwezi Juni 2024. Pia tumesikiliza mashauri yote ya muda mrefu, hivyo kuvuka mwaka 2023 bila mlundikano,” alisema.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Hamidu Mtulya akizungumza na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania, Ndg. Gerald Chami (katikati picha ya chini) alipokuwa ofisini kwake kwa ziara fupi aliyoifanya hivi karibuni. Kulia ni Mtendaji wa Mahakama, Kanda ya Musoma, Bw. Leonard John Maufi.

Akizungumzia usikilizaji wa mashauri kwa Kanda nzima kwa ujumla, Mhe. Salome alieleza kuwa Mahakama katika ngazi zote kuanzia Mahakama za Mwanzo hadi Mahakama Kuu zilivuka mwaka 2022 na jumla ya mashauri 2,792, yaliyosajiliwa mwaka 2023 yalikuwa 14,646, mashauri yaliyoamuriwa yalikuwa 14,561 na yale yaliyobaki ni 2,877.
Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Salome Abubakar Mshasha (katikati) akiwa na pacha wake, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Mhe. Monica Onesmo Ndyekobera (wa kwanza kushoto) ndani ya ofisini kwa Jaji Mfawidhi.

Akifafanua zaidi, Naibu Msajili Mfawidhi alieleza kuwa Mahakama Kuu ilivuka mwaka 2022 na mashauri 297, yaliyosajiliwa mwaka 2023 yalikuwa 1,254, mashauri 1,305 yaliamuliwa na yaliyobaki yalikuwa 246.

Kwa upande wa Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mhe. Salome ambaye aliambatana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu katika Kanda hiyo, Mhe. Monica Onesmo Ndyekobera, alieleza pia kuwa kulikuwa na mashauri 58 yaliyovuka mwaka 2022, yaliyosajiliwa mwaka 2023 yalikuwa 231, yaliyoamuriwa yalikuwa 201 na mashauri yaliyobaki ni 88.
Akizungumzia upande wa Mahakama za Wilaya, Naibu Msajili Mfawidhi alieleza kuwa mashauri 1,142 yalivuka mwaka 2022, yaliyosajiliwa mwaka 2023 yalikuwa 1,626, yaliyoamuriwa ni 1,680 na yaliyobaki yalikuwa mashauri 1,088.

Kwa upande wa Mahakama za Mwanzo, jumla ya mashauri 1,295 yalivuka mwaka 2022, mashauri 11,535 yakapokelewa mwaka 2023, yaliyoamuriwa yalikuwa 11,375 na mashauri yaliyobaki yalikuwa 1,455 pekee.
Mtendaji wa Mahakama, Kanda ya Musoma, Bw. Leonard John Maufi akifafanua jambo.

Naye Mtendaji wa Mahakama, Kanda ya Musoma, Bw. Leonard John Maufi, alieleza kuwa mwaka 2023 ulikuwa wa mafanikio makubwa katika utendaji kazi na kumekuwepo na juhudi mbalimbali ili kuwezesha shughuli za kimahakama kufanyika.

“Tumeweka mtandao wa dharura (mbadala) katika jengo la Mahakama Kuu Musoma kwa ajili ya matumizi pale mtandao wa Mahakama unapokata ili kutokwamisha shughuli za kimahakama.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Hamidu Mtulya akiagana na Mkuu wa Kitengo cha Haberi, Elimu na Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania, Ndg. Gerald Chami baada ya mazungumzo mafupi.

"Pia tumewezesha laini za simu za kampuni ya TIGO katika Magereza matatu (Tarime, Musoma na Serengeti) na Mahakama za Wilaya zote ndani ya Kanda hii ili kurahisisha uendeshaji wa mashauri pale inapotokea changamoto ya mtandao (Internet),” alisema.
Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Salome Abubakar Mshasha.

Mafanikio mengine ni kufanyika kwa ukarabati mkubwa wa majengo ya Mahakama za Mwanzo Kiagata, Ngoreme, Mtana, Kenkombyo, Nansimo na Musoma Mjini na kuanzishwa kwa Mahakama mbili za Mwanzo ambazo ni Mahakama ya Mwanzo Mukendo iliyoko Musoma na Mahakama ya Mwanzo Ingri iliyoko Rorya, hivyo kusogeza huduma za Mahakama karibu na wananchi.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma, Mhe. Monica Onesmo Ndyekobera.

Bw. Maufi alieleza pia kuwa wameendeleza ushirikiano mwema kati ya Mahakama na wadau wake wa Taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali na kushiriki katika matendo ya huruma kwenye jamii kwa kutoa misaada kwa wahitaji kama vile vituo vya kulelea watoto yatima Musoma Children Home pamoja na Magereza ya Wilaya Musoma, Tarime, Seregeti na Bunda.
Muonekano kwa mbele wa jengo la Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma.

Alitaja mafanikio mengine kama ununuzi wa vifaa vya TEHAMA na Samani za ofisi, hasa katika Mahakama za Wilaya ili kuwezesha shughuli za uendeshaji wa Mahakama, kuwezesha Mahakama zote za Mwanzo katika Kanda Musoma kufanya kazi na upandaji wa miti katika Mahakama za Mwanzo zote ili kutunza mazingira na kulinda mipaka ya maeneo ya Mahakama.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Hamidu Mtulya (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Haberi,Elimu na Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania, Ndg. Gerald Chami (wa pili kulia). Wengine katika picha (juu na chini) ni Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Salome Abubakar Mshasha (wa pili kushoto), Naibu Msajili wa Mahakama Kuu katika Kanda hiyo, Mhe. Monica Onesmo Ndyekobera (wa kwanza kushoto) na Mtendaji wa Mahakama, Kanda ya Musoma, Bw. Leonard John Maufi (wa kwanza kulia).

Kabla ya kuzungumza na viongozi hao wa Mahakama, Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano alikutana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Hamidu Mtulya na kufanya naye mazungumzo mafupi kabla ya kuendelea na ziara yake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news