Mahakama, wadau wakubaliana kumaliza mrundikano wa mashauri Pwani

NA EUNICE LUGIANA
Mhakama Pwani

HAKIMU Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi pamoja na wadau wa haki jinai wamefanya kikao cha kusukuma mashauri katika Mahakama hiyo na kuazimia kuwa mashauri yaliyo katika mrundikano kufikia Septemba, mwaka huu yawe yamemalizika.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wadau wa Haki Jinai Mkoa wa Pwani mara baada ya kumaliza kuzungumza na wafungwa na mahabusu katika Gereza la Mkuza (wa pili kulia) ni Mkuu wa Upelelezi, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Victor Samata. Kulia kwa Mhe. Mkhoi ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha, Mhe. Emmael Lukuma pamoja na wadau wengine.

Katika kikao hicho kilichofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, walikubaliana pia kuhakikisha mashahidi wanafika kwa wakati na kwa mashauri ambayo upelelezi haujakamilika kufika Septemba upelelezi uwe umekamilika.

Hata hivyo ilielezwa kuwa,  katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani hakuna mashauri ya mlundikano kwa kuwa yaliopo ni ya miezi mitatu kushuka chini.

Waliongeza kwa kukumbushana kuwa, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mashauri yachukue muda wa miezi sita ikizidi hapo inakuwa imepitwa na wakati. 

“Katika hili wadau wote wa haki jinai wamefanikiwa kuondosha mlundikano kwa njia hiyo na kwa sasa kesi zilizo na miezi mitatu kufikia septemba ziwe zimeisha,” alisema Mhe. Mkhoi.
Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Kipolisi Mlandizi, Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Thomas Kilakoi akitoa maoni yake katika kikao cha kusukuma mashauri katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani kilichofanyika hivi karibuni.

Akizungumza katika kikao hicho, Mfawidhi huyo alimpongeza Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Kisarawe, Mrakibu Msaidizi wa Polisi Joseph Matui kwa kufanya upelelezi kwa wakati na hivyo kuwezesha kuondosha mlundikano.

Naye Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Kipolisi Mlandizi, Mrakibu Msaidizi wa Polisi Thomas Kilakoi ameomba wakati wa mwisho wa wiki awepo Hakimu ambaye atasaini fomu za uchunguzi wa miili iliyopatikana kwa sababu inakuwa changamoto kama maiti imepatikana ikiwa katika hali ya kuharibika inakuwa ni changamoto kusubiri mpaka Jumatatu.
Baadhi ya Wadau wa Haki Jinai wakiwa katika kikao cha kusukuma mashauri kilichofanyika Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani kilichofanyika hivi karibuni.

“Awepo Hakimu anayepatikana mwisho wa wiki ili inapotokea dharura fomu ijazwe kwa wakati na uchunguzi uendelee ili ndugu wachukue mwili wakazike maana Pwani ni Mkoa uliopo njiani ajali ni nyingi hivyo tunaomba kama itawezekana awepo Hakimu wakati wote ikitokea hali kama hiyo,” alisema Mrakibu Kilakoi.

Kabla ya kikao hicho, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo pamoja na wadau wa Haki Jinai walitembelea Gereza la Mkuza ili kusikiliza changamoto na maoni ya wafungwa na mahabusu walioko katika Gereza hilo.

Akisikiliza risala iliyosomwa na Mhabusu kutoka Gereza hilo, Bw. Peter Modest Mbala aliiomba Mahakama kusimamia na kutoa haki na pale wanapoona ushahidi unalega uamuzi utolewe na mshtakiwa aachiwe huru.
Baadhi ya Wadau wa Haki Jinai wakiwa katika kikao cha kusukuma mashauri kilichofanyika Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani kilichofanyika hivi karibuni.

Akijibu hoja hiyo, Mhe. Mkhoi alisema Mahakama inazingatia sheria na inatoa haki kwa mujibu wa sheria hivyo, alitoa wito pia kwa wadau wote wa haki jinai kuisaidia Mahakama kufikia utoaji wa uamuzi sahihi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news