NA MARY GWERA
Mahakama Dodoma
MTENDAJI Mkuu Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza bajeti ya Mahakama kutoka Shilingi bilioni 155 kwa mwaka wa fedha 2020/2021 hadi kufikia shilingi bilioni 241.6 kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza na Waandishi wa Habari leo tarehe 05 Juni, 2024 katika ukumbi wa Mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) kuhusu Miaka Mitatu ya Uongozi wa Rais wa Awamu ya Sita wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo tarehe 05 Juni, 2024 katika ukumbi wa Mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma kuhusu Miaka Mitatu ya Uongozi wa Mhe.Dkt.Samia ilivyogusa Mahakama ya Tanzania, Prof.Ole Gabriel amesema kuwa, hatua hiyo inaonesha ni kwa namna gani ambavyo Serikali inathamini na kutambua majukumu yanayofanywa mhimili huo.
Sehemu ya Waandishi wa Habari wakifuatilia kwa makini taarifa ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (hayupo katika picha) wakati wa Mkutano uliofanyika leo tarehe 05 Juni, 2024.
“Mwaka ule 2021 wakati Rais Samia anaingia madarakani bajeti ya Mahakama na sio siri unaposema bajeti hili ni jambo limepitishwa na Bunge, bajeti ya Mahakama ilikuwa Shilingi bilioni 155, mwaka ujao wa fedha bajeti iliyopitishwa ni Shilingi bilioni 241.6 maana yake kuna ongezeko la shilingi bilioni 86.6 sawa na asilimia 55.5,” amesema Mtendaji Mkuu.
Amesema, hatua hiyo inaonesha ushirikiano ambao Serikali inaendelea kuutoa kwa Mahakama katika kuiwezesha kutekeleza ipasavyo majukumu yake.
Sehemu ya Waandishi wa Habari wakifuatilia kwa makini taarifa ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (hayupo katika picha) wakati wa Mkutano uliofanyika leo tarehe 05 Juni, 2024.
Mbali na ongezeko la bajeti, Prof. Ole Gabriel amebainisha maboresho kadhaa ya Mahakama ambayo yamepatikana ndani ya miaka mitatu ya Uongozi wa Mhe. Dkt. Samia ambayo ni pamoja na Matumizi ya TEHAMA, Ujenzi wa majengo ya Mahakama ikiwemo Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki (IJCs), Ongezeko la Majaji na Ajira kwa watumishi wapya na kadhalika.
Akizungumzia kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na Habari (TEHAMA), Mtendaji huyo amesema kwamba, yamerahisisha utendaji kazi wa Mahakama lakini pia yameondoa usumbufu kwa wananchi kuhudhuria mahakamani kwa shughuli mbalimbali.
“Mahakama ni Taasisi ya kwanza ya umma ambayo ina matumizi ya hali ya juu ya mtandao, hivi sasa tunayo mifumo ambayo inarahisisha utendaji kazi kwa mfano tunao Mfumo wa Ofisi Mtandao ambao unawezesha watu kufanya kazi zao hata wakiwa nje au ndani ya Nchi, Mfumo wa Mkutano Mtandao ‘Video Conference’ ambapo Mashauri mengi sasa yanaendeshwa kwa njia ya mtandao,” alisema Prof. Ole Gabriel.
Afisa Utumishi Mkuu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Bi. Lucy Timba akifanya utambulisho wa Wawakilishi kutoka Ofisi hiyo pamoja na Waandishi wa Habari waliohudhuria katika Mkutano wa 'Mitatu Dodoma na Samia' kilichofanyika leo tarehe 05 Junj, 2024 katika ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma.
Akizungumzia kuhusu Mfumo wa Taarifa za Sheria na Maamuzi Tanzania (TanzLII), Mtendaji ameeleza kuwa, Mfumo huo unatembelewa kwa zaidi ya asilimia 82.4 huku akibainisha kuwa Nchi inayofuatia yenye Mfumo kama huo inatembelewa na wadau kwa asilimia 2.7.
Akizungumzia kuhusu mafanikio yaliyopatikana kwa upande wa miundombinu ya majengo ya Mahakama, Mtendaji Mkuu ameeleza kuwa, wakati Rais Samia alipoingia madarakani alizindua jumla ya Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki (IJCs) sita (6) ambavyo ni pamoja na Kituo cha Dodoma ambacho Mkutano huo umefanyikia leo.
Mwandishi wa Habari kutoka Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Bw. Asher Thomas akiuliza swali wakati wa Mkutano huo.
“Kadhalika, kuna ujenzi wa Vituo Jumuishi tisa (9) ikiwemo Pemba ambavyo tayari vimeanza kujengwa na ujezi wake utachukua miezi tisa. Kituo cha mwisho kinatarajiwa kukamilika tarehe 23 Februari, 2025. Sambasamba na hili ujenzi wa Mahakama za Mwanzo 60 mikataba yake imesainiwa (leo) tarehe 05 Juni, 2024,” amefafanua Prof. Ole Gabriel.
Kadhalika, Mtendaji Mkuu amezungumzia kuhusu Mafunzo ya muda mfupi yaliyotolewa kwa Watumishi na Wadau wa Mahakama ambapo ameeleza kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu ya Uongozi wa Rais Samia, Mahakama ya Tanzania imefanikiwa kutoa Mafunzo kwa jumla ya Watumishi na Wadau 8,701 akieleza kuwa, Watumishi walionufaika na Mafunzo hayo ni pamoja na Majaji, Mahakimu pamoja na Watumishi wasio Mahakimu.Mwandishi wa Habari kutoka Gazeti la Majira, Bi. Joyce Kasiki akiuliza swali mara baada ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama kutoa wasilisho lake.
Ameongeza kwa kuzungumzia kuhusu ongezeko la Majaji wa Mahakama ya Rufani kutoka 16 hadi 35 na wa Mahakama kuu kutoka 75 hadi 105 sambamba na kutoa nafasi za 762 za ajira kwa Watumishi wapya wakiwemo Mahakimu Wakazi 78 na Watumishi wasio Mahakimu 684.
Mkuu wa Vipindi na Maudhui kutoka Manyunyu TV na Balozi wa Kuutangaza Mkoa wa Dodoma, Dkt. Kennedy Festo akizungumza jambo wakati wa Mkutano huo.
Prof. Ole Gabriel ametoa rai kwa Wananchi kuendelea kutumia Mahakama kwa kuwa maboresho yote yanayofanyika yanawalenga wao. Aliongeza, “hatusemi tunajenga majengo au kuboresha matumizi ya TEHAMA kwa mantiki ya kujisifu la hasha bali yote haya yanafanyika lengo likiwa ni kuboresha huduma ya utoaji haki kwa wananchi.”
Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mtendaji wa Mahakama ya Rufani (T), Bw. Victor Kategere (kushoto) na Mtendaji wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma, Bw. Sumera Manoti (kulia) wakati wa Mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika IJC Dodoma leo tarehe 05 Juni, 2024.(Picha na Mary Gwera, Mahakama).
Mkutano huo wa ‘Mitatu Dodoma na Samia’ wenye Kauli Mbiu isemayo; “Kero yako, Wajibu Wangu Dodoma Fahari ya Watanzania. Wekeza Dodoma, Stawisha Dodoma,” umeratibiwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma lengo likiwa ni kutoa fursa kwa Wizara na Taasisi mbalimbali kuuhabarisha umma kuhusu mafanikio mbalimbali yaliyofikiwa na Taasisi husika katika kipindi cha Miaka mitatu ya Uongozi wa Awamu ya Sita wa Rais Samia.