□Majaji, Wasajili na Mahakimu wastajabisha mashabiki walivyolisakata kabumbu
NA MARY GWERA
Mahakama
TIMU ya Mahakama ya Tanzania iliyohusisha Majaji, Wasajili na Mahakimu imeibuka bingwa katika mchezo wa mpira wa miguu iliyocheza dhidi ya Timu ya Bunge la Tanzania katika mashindano ya Bunge ‘Grand Bonanza’ baada ya mchuano mkali wa dakika 90 uliohitimishwa kwa bao moja kwa moja na baadae Mahakama kunyakua ushindi kwa mikwaju ya penati ya goli nne kwa tatu.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa na Kapteni wa Timu inayoundwa na Majaji, Wasajili na Mahakimu, Mhe. Said kalunde (aliyeshika kombe) akipokea kombe la ushindi kutoka kwa Mgeni Rasmi Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla (katikati) mara baada ya Timu hiyo Kuibuka na ushindi katika mashindano ya Bunge 'Grand Bonanza' kwa Mpira wa Miguu tarehe 22 Juni, 2024 katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Mechi hiyo iliyochezwa leo tarehe 22 Juni, 2024 katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma ilianza majira ya saa 2.55 asubuhi ambapo Timu ya Mahakama iliweza kupata goli la kuongoza ndani ya dakika ya 28 katika kipindi cha kwanza cha mchezo huo ambapo mpaka wanaenda mapumziko Mahakama ilikuwa ikiongoza.
Aidha, ndani ya kipindi cha pili Bunge nao walifanikiwa kurudisha goli na mchezo kusomeka moja moja, hata hivyo, mpaka mechi ilipomalizika Timu zote zilitoka sare kwa bao moja kwa moja.
Mara baada ya dakika 90 za mchezo kukamilika bila mshindi kupatikana, mechi ilibidi iamuliwe kwa mikwaju ya penati ambapo Timu ya Mahakama ilibuka mshindi kwa kuinyuka Timu Bunge mikwaju minne kwa mitatu.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa na Kapteni wa Timu inayoundwa na Majaji, Wasajili na Mahakimu, Mhe. Said kalunde (aliyeshika kombe) akifurahia kombe la ushindi wa Mahakama kutoka kwa Mgeni Rasmi Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla (katikati) mara baada ya Timu hiyo Kuibuka na ushindi katika mashindano ya Bunge 'Grand Bonanza' kwa Mpira wa Miguu tarehe 22 Juni, 2024 katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Timu ya Mahakama imefanikiwa kufanya kile kilichokusudiwa kwa kukonga nyoyo za watu hasa watumishi wa Mahakama kwa kuibuka na ushindi huo.
Akitoa salaam za pongezi mara baada ya mashindano hayo kwa niaba ya Jaji Mkuu, Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani amelishukuru Bunge la Tanzania kwa kuialika Mahakama na kuomba kuwa, awamu nyingine watakapoialika Mahakama wawashirikishe katika michezo mbalimbali badala ya mchezo wa mpira wa miguu pekee.
“Mbali na kutoa haki, Mahakama inashiriki pia katika michezo, hivyo ni ombi langu katika Bonanza zijazo tupangiwe michezo mingi badala ya mmoja pekee ili tuoneshe uwezo zaidi,” amesema Mhe. Siyani.
Kocha wa Timu ya Majaji, Wasajili na Mahakimu, Bw. Spear Dunia Mbwembwe akiwa amebeba kombe la ushindi baada ya kutwaa kombe hilo tarehe 22 Juni, 2024.
Naye Spika wa Bunge la Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson amesema kwamba lengo la Bonanza hilo ni kujenga mahusiano kati ya Watumishi wa Mhimili pamoja na Wadau.
“Moja ya malengo ya Bonanza hili ni kuleta ushirikiano sambamba na kujenga afya njema,” amesema Mhe. Dkt. Tulia.
Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maendeleo kadhaa ikiwa ni pamoja na maendeleo ya Sekta ya michezo.
Shangwe za ushindi; sehemu ya Wachezaji na watumishi wengine wa Mahakama wakishangilia ushindi wa mpira wa miguu katika mashindano ya Bunge 'Grand Bonanza' yaliyofanyika tarehe 22 Juni, 2024 katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Mgeni Rasmi katika Bonanza hilo lililodhaminiwa na Benki ya CRDB, alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ambaye amemuakilisha Rais wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Akizungumza mara baada ya hitimisho la mashindano hayo yaliyohusisha michezo mbalimbali, Mhe. Abdulla amelipongeza Bunge la Tanzania pamoja na Benki ya CRDB kwa kuja na Bonanza hilo kwakuwa sio tu linajenga ushirikiano bali linajenga afya za washiriki.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla (wa tatu kushoto) pamoja na Viongozi wengine wakifuatilia mechi ya mpira wa miguu iliyokuwa ikichezwa kati ya Timu ya Mahakama na ya Bunge katika mashindano ya Bunge 'Grand Bonanza' yaliyofanyika leo tarehe 22 Juni, 2024 katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. Wa nne kulia ni Spika wa Bunge la Tanzania na Rais wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, wa tatu kulia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani, wa kwanza kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo, wa pili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe.Rosemary Senyamule na Viongozi wengine.
Furaha ya Jaji Mtulya baada ya ushindi wa Timu ya Mpira wa miguu ya Mahakama ambayo naye ameshiriki kucheza.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Manyara na Rais wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT), Mhe. John Kahyoza (kushoto) na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo na washiriki wengine wakifanya mazoezi ya viungo katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Matembezi ya uzinduzi wa Bunge 'Grand Bonanza'.
Sehemu ya Watumishi (kushoto) wa Mahakama wakifanya mazoezi kwenye Bunge 'Grand Bonanza'.
“Nimefarijika sana kushiriki pamoja na Wabunge na wadau wengine katika Bonanza hili, rai yangu ni kumuomba kila mmoja kushiriki katika michezo mbalimbali pamoja na kuendelea na utaratibu huo,” amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB na Mdhamini wa Bonanza hilo, Bw. Abdulmagid Nsekela amesema kwamba, michezo pia hutumika kama njia ya kutoa elimu kwa wananchi.
Bonanza hilo lilitanguliwa na matembezi maalum yaliyoanza majira ya saa 12.30 alfajiri na yalianzia katika Viwanja vya Bunge hadi Uwanja wa Jamhuri. Matembezi hayo yaliongozwa na Mgeni Rasmi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ambaye amemuakilisha Rais wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Sehemu yaWatumishi wa Mahakama walioshiriki katika mashindano ya Bunge'Grand Bonanza' lililofanyika katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Washiriki mbalimbali wakiwepo watumishi wa Mahakama, Bunge na wengine wakiwa katika Bunge 'Grand Bonanza' lililofanyika tarehe 22 Juni, 2024 jijini Dodoma.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ambaye amemuakilisha Rais wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Washiriki katika Bonanza hilo.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambae pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani Mhe. Dkt. Tulia Ackson akihutubia katika Bonanza hilo.
Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Mustapher Mohamed Siyani akihutubia katika Bonanza mara baada ya Timu hiyo Kuibuka na ushindi wa Bunge Grand Bonanza kwa Mpira wa Miguu tarehe 22 Juni, 2024.
Viongozi wengine walioshiriki ni Naibu Waziri Mkuu, Mhe. Dotto Biteko, Spika wa Bunge, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na baadhi ya Watumishi wa Mahakama na washiriki wengine.
Michezo mingine iliyochezwa katika Bonanza hilo ni pamoja na mbio, netiboli, mpira wa kikapu, kukimbiza kuku, kukimbia kwa magunia, mchezo wa bao, mpira wa wavu, kuvuta Kamba, mpira wa meza, kutembea haraka, mpira wa kikapu na mingine.
Tags
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Habari
Judiciary of Tanzania
Mahakama ya Tanzania
Michezo