Makatibu EAC wafanya mashauriano uanzishwaji vituo vya umahiri

ARUSHA-Makatibu Wakuu wa sekta ya afya kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamekutana tarehe 14 Juni, 2024, jijini Arusha kwa kikao cha mashauriano.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe akiwasilisha hotuba ya ufunguzi katika kikao cha Mashauriano cha Makatibu Wakuu kilichofanyika jijini Arusha, tarehe 14 Juni, 2024.

Kikao hicho ni maandalizi ya Mkutano wa 7 wa Dharura wa Baraza la Kisekta la Mawaziri, unaotarajiwa kuitishwa katika tarehe itakayopangwa baada ya kukamilika kwa mashauriano hayo.

Mashauriano haya yanafanyika kufuatia wasilisho la pendekezo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kuanzisha vituo vya umahiri, ambavyo ni Kituo cha Umahiri cha Sayansi ya Afya ya Kinywa chini ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), na Kituo cha Umahiri cha Upandikizaji Uloto na Sayansi ya Matibabu ya Magonjwa ya Damu chini ya Hospitali ya Benjamin Mkapa.
Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania ukifuatilia majadiliano.


Ujumbe wa Tanzania.

Akihutubia katika ufunguzi wa Mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, ameeleza kuwa kuanzishwa kwa vituo hivyo vya kikanda kutasaidia kuinua uwezo katika matibabu ya kibingwa, mafunzo ya kibobezi, utafiti, na utoaji wa huduma maalum za afya.
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Miundombinu ya Kiuchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhandisi Abdillah Mataka akifuatilia majadiliano katika kikao cha Makatibu Wakuu.

Aidha, amefafanua kuwa kuanzishwa kwa vituo hivyo ni ushahidi wa nia ya dhati ya kukuza ushirikiano wa kikanda, hususan katika masuala ya afya na elimu. Vilevile, vituo hivyo vitatumika kama maeneo ya kukuza ubunifu, vipaji, na utaalamu wa kikanda na katika maeneo mengine.

Naye Mwenyekiti wa kikao hicho, Katibu Mkuu wa Afya wa Jamhuri ya Sudan Kusini, Dkt. Ader Macar Aclek ambaye alishiriki mashauriano kwa njia ya mtandao ameipongeza Tanzania kwa jitihada zake za kufanikisha kuwasilisha andiko dhana la kuanzishwa kwa vituo vya umahiri. 

Pia, ameonyesha umuhimu wa kushirikiana katika kupambana na changamoto za kidunia, hususan mabadiliko ya tabia nchi ambayo yamekuwa yakileta mlipuko wa magonjwa mbalimbali yanayohitaji jitihada za pamoja kukabiliana nayo.
Kutoka kushoto Mwenyekiti wa kikao wa Wataalam kutoka Jamhuri ya Sudan Kusini, Mhandisi Ring Rut ambaye Mkurugenzi wa Sekta ya Jamii kutoka Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Irene Isaka na Mkuu wa Idara ya Afya katika Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Eric Nzeyimana wakiongoza majadiliano ya kikao hicho.

Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Sekta ya Jamii kutoka Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Irene Isaka kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu, Sekta za Miundombinu, Uzalishaji, Jamii na Siasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki alitumia wasaa huo wa ufunguzi wa kikao kuwaeleza wajumbe kuwa ana matumaini majadiliano ya kikao hicho yatafanyika kwa tija na masilahi mapana ya kikanda.

Kadhalika, alishauri kuwa ni vyema Nchi Wanachama zikatoa ushirikiano katika uanzishwaji wa vituo hivyo vipya ili viweze kufikia malengo ya utendaji yanayotarajiwa katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiafya zinazoendelea kikanda na ulimwenguni kwa ujumla.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe (kulia) na Makamu Mkuu wa Chuo cha Afya Shirikishi cha Muhimbili, Prof. Bruno Sunguya wakifuatilia majadiliano ya kikao.
Ujumbe wa Tanzania ukifuatilia majadiliano.

Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huu wa Makatibu Wakuu umeongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, ambaye ameambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. James Mdoe, pamoja na maafisa waandamizi kutoka wizara na taasisi za afya na elimu nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news