ZANZIBAR-Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mama Maryam Mwinyi amekabidhi mkono wa Eid kwa watoto yatima pamoja na wasiojiweza zaidi ya 50 waliopo katika Nyumba ya Wema Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Msaada huo ambao ni fedha taslimu amekabidhi Juni 17,2024 ikiwa ni zawadi maalum kwa watoto hao kwa ajili ya Sikukuu ya Eid Al Adha.
Akizungumza na watoto hao amewataka kuendeleza bidii katika masomo ya dini ili kuweza kuwa viongozi watakoendeleza vyema Taifa bora la baadae.
Aidha,amesema kuwa lengo la kutoa msaada kwa watoto hao ni kuweza kuunganisha pamoja watu wa hali zote katika kipindi hiki cha kusherehekea sikukuu ya Eid AlAdha.
Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Zanzibar, Mhe. Riziki Pembe Juma amemshukuru Mama Maryam Mwinyi kwa kukadidhi fedha hizo kwa watoto hao ambapo amesema,msaada huo utawasaidia katika matumizi mbalimbali ndani ya kipindi hiki cha sherehe za sikukuu.
Watoto hao kutoka maeneo mbalimbali ambao wapo katika Nyumba ya Wema Micheweni hawakusita kumuombea dua Mama Maryam Mwinyi pamoja na kuiombea Zanzibar kwa ujumla.