DAR-Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA),Dkt.Erasmus Kipesha leo Juni 3, 2024 amesaini makubaliano maalum na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Utangazaji cha EATV Limited,Regina Mengi kushirikiana katika kuendesha Kampeni ya Namthamini.
Kampeni ambayo inalenga kuboresha mazingira ya watoto mashuleni hasa watoto wa kike, hafla iliyofanyika Mikocheni katika ofisi za EATV jijini Dar es Salaam.
Namthamini ni kampeni iliyoanzishwa na kituo utangazaji cha EATV Limited mwaka 2017 kwa ajili ya kuchangisha taulo za kike kwa wanafunzi wenye uhitaji mashuleni ambapo, kampeni hii ilikuja baada ya tafiti kuonyesha kuwa wasichana wengi hupata changamoto katika siku zao za hedhi kwa kushindwa kununua taulo za kike, hivyo kupelekea kukosa masomo kwa takribani siku 3 mpaka 7 kwa mwezi.
Katika kampeni hii, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) itahamasisha uchangiaji wa rasilimali fedha na vifaa kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo na upatikanaji wa maji safi na salama ili kuwasaidia watoto wa kike kuwa na uhakika wa kubaki wasafi katika mazingira ya shule wawapo katika siku za hedhi.
Akizungumza katika hafla hiyo,Dkt.Kipesha amesema, TEA imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali kwa ajili ya kutafuta rasilimali fedha na vifaa kwa ajili ya kufadhili miradi ya elimu.
Lengo ni kusaidia jitihada za Serikali za kuboresha mazingira ya kujifunza na kufundishia, hivyo anaamini kampeni ya Namthamini ambayo mwaka huu itaendeshwa kwa ushirikiano baina ya EATV na Mfuko wa Elimu wa Taifa unaosimamiwa na TEA itawaibua wadau wengi zaidi kuchangia ili kumpa mtoto wa kike tabasamu siku zote akiwa shuleni.
Aidha, Dkt. Kipesha aliongeza kuwa, wachangiaji wa sekta ya elimu kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa watanufaika kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na; Kupata Hati ya Utambuzi wa Uchangiaji wa Elimu (Certificate of Educational Appreciation).
Hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa Kifungu cha 12 cha Sheria ya Mfuko wa Elimu ya mwaka 2001; Kuweza kutumia Hati ya Utambuzi wa Uchangiaji wa Elimu (Certificate of Educational Appreciation) kuombea nafuu ya kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa mujibu wa Kifungu cha 16 (1) cha Sheria ya Kodi ya Mapato Sura 332 marejeo ya mwaka 2019; Kutangazwa na kutambuliwa kitaifa, ambapo mchangiaji huandikwa katika rejesta ya kudumu ya wachangiaji wa elimu.