TANGA-Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amesema rasilimali watu yenye elimu, ujuzi, weledi na maarifa ndio msingi wa kujenga uchumi shindani na endelevu.
Mhe. Majaliwa amesema hayo Mei 31, 2024 jijini Tanga wakati akizungumza katika kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu akisema kuwa Serikali inalenga kuongeza mikakati na hamasa ya kukuza elimu, ujuzi, na matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu (STU) kama nyenzo za kusaidia kutatua changamoto za kiuchumi na kijamii pamoja na kuchagiza maendeleo ya nchi kwa ujumla.
"Serikali inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuendeleza elimu ngazi zote msingi, elimu ya ufundi, Elimu ya Juu pamoja na shughuli za utafiti na ubunifu," amesema Mhe Majaliwa.
Amepongeza maandalizi ya Maadhimisho hayo kuwa ya viwango vya juu na kuagiza kutangazwa pia kimataifa huku akifurahishwa na ushiriki wa wadau mbalimbali katika kuendeleza sekta ya Elimu Sayansi na Teknolojia kupitia Wizara na Taasisi zake.
"Nimefurahi sana kuona ushiriki wa Wadau wa Maendeleo na Sekta Binafsi kupitia mradi niliouzindua wa Smart Wasomi mnaotekekeza kwa ushirikiano, Serikali itaendelea na kazi ya kuvutia fedha na rasilimali nyingine kutoka kwa Wadau wa Maendeleo na Sekta Binafsi ili kuongeza fursa za utoaji Elimu uendelezaji ujuzi na kuimarisha matumizi ya teknolojia,’’ amesema Majaliwa.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema katika kuongeza mchango wa sayansi, teknolojia na ubunifu, Wizara inaendelea kutekeleza juhudi mbalimbali ikiwemo kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia yanayolenga kuiboresha na kuihuisha kuwa Sera ya Taifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu.
"Kuna bunifu na teknolojia zenye sifa na zinajibu changamoto za kiuchumi na kijamii, hivyo, Wizara itaendelea kuchukua hatua zinazolenga kuziendeleza na kuzibiasharisha," amebainisha Mkenda.