DAR-Mawaziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Utamaduni na Michezo kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamekutana Juni 22, 2024 jijini Dar es Salaam kushiriki Mkutano wa Kisekta wa 19 wa EAC.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb.) ameshiriki mkutano huo na kubainisha kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesisitiza umuhimu wa matumizi ya lugha ya Kiswahili katika vikao vya sekta hiyo na vikao vya Jumuiya ya Afrika Mashariki na hatimaye waweze kuikuza na kuipeleka hoja kwa Mataifa.


Aidha, ameeleza kuwa wameongelea uwepo wa mashindano makubwa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027 ambapo amesema wao kama Tanzania kwa kushirikiana na Kenya, Uganda watakuwa wenyeji kwenye mashindano hayo.
Mwisho amesema nchi zingine zote za jumuiya ya Afrika Mashariki wafahamu kwamba wao pia watakuwa wenyeji kwa namna moja ama nyingine kwenye mashindano hayo.
Kwa upande wake Waziri wa Jinsia, tamaduni, sana na torati za Taifa katika nchi ya Kenya, Mhe. Aisha Juma, amesema kwa mwaka huu wao ndio wanaandaa siku ya ulimwengu ya kiswahili ambayo itaadhimishwa Julai 7, 2024.
Amesema,maandalizi yako tayari ikiwemo kuwaalika wanajumuiya wote kwa ajili ya kusherehekea siku hiyo muhimu.
Ameeleza kuwa, Kiswahili ni lugha inayotumika sana ulimwenguni ambapo takribani watu milioni 500 wanazungumza lugha ya kiswahili pia inasaidia kukuza uchumi.
