Mheshimiwa Rais Dkt.Samia endelea kuwawajibisha-Mwinjilisti Temba

DAR-Muhubiri na Mwinjilisti wa Kimataifa, Alphonce Temba amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuingilia kati sakata la Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dkt. Yahaya Ismaili Nawanda.
Juni 11, 2024 Rais Dkt. Samia alitengua utenguzi wa Dkt. Nawanda ikiwa ni siku moja baada ya taarifa kusambaa katika mitandao ya kijamii na vyombo mbalimbali vya habari kuwa anatuhumiwa kumuingilia kinyume na maumbile (kulawiti) binti mwenye umri wa miaka 21 ambaye ni mwanafunzi wa chuo kikuu jijini Mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari Juni 12, 2024 jijini Dar es Salaam Mwinjilisti Temba, alisema hatua hiyo ya Rais Dkt. Samia ni uamuzi mzuri, mgumu na wenye busara kwa Mkuu wa Mkoa ambaye ametuhumiwa kwa kitendo hicho cha kikatili na taarifa kusambaa katika vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii ndani na nje ya nchi na kuligawa Taifa na Serikali.

"Tabia anazotuhumiwa nazo ni za ajabu na hazitegemewi kufanywa na kiongozi mkubwa kama huyo kama zilivyoripotiwa, iwe alisingiziwa ama alifanya, lakini kwasababu ya uovu huo mbaya na Mama amekuwa mstari wa mbele kupinga kwa nguvu kubwa mambo haya ambayo yamekuwa yakionekana yakizungumzwa zungumzwa yakitokea nchi za Ulaya na Mataifa mengine ya Magharibi," alisema Mwinjilisti Temba na kuongeza,

"Kwa mambo kama haya ambayo amekuwa akishutumiwa moja kwa moja ilikuwa ni suala la hekima na busara Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani kumuweka pembeni,".
Mwinjilisti Temba ametaka hatua hiyo iwe ni onyo kwa Wakuu wa Mikoa na wateule wengine wa Rais kwamba pale watakaposhutumiwa kwa nguvu katika kashfa kubwa ni vizuri wakapisha wenyewe ili Serikali iweze kuongozwa na viongozi ambao wananchi watakuwa na imani nao ikizingatiwa kuwa mwaka huu 2024 na mwaka kesho 2025 ni wakati ambao unakwenda kufanyika Uchaguzi Mkuu ambapo Watanzania watachangua viongozi mbalimbali.

"Hivyo ilikuwa ni jambo la busara na nawaambia Watanzania ni vizuri tukampongeza mama kwa kuwa hakusubiri taarifa mbalimbali na kelele za watu kuchukua hatua, kwasababu hayo hakutumwa (Mkuu wa Mkoa) akayafanyie kazi, na siku zote Mhe. Rais amekuwa akiwateua baadhi na kuwatengua, na pale ambapo anawapa nafasi bila kupepesa macho amekuwa akiwapa maelekezo ya nini wakafanye, nje ya kiapo chao wanachoapa na majukumu yao ya kila siku, amekuwa akikazia wananchi wakatendewe haki, wananchi watatuliwe matatizo yao, wapambane wakalete vitu vipya kuboresha maeneo waliyopo na kama watahitaji misaada yake waendelee kuwasiliana naye na atawasaidia," amebainisha Mwinjilisti Temba.

Hivyo ameeleza kuwa kutokana na kadhia hiyo Viongozi wa Dini wamesikitishwa na kitendo hicho cha kinyama, kipuuzi na kijinga ambacho hakikutegemewa wala kudhaniwa kama kinaweza kufanywa na kiongozi mwenye mamlaka makubwa kama hiyo.

“Hivyo pongezi hizi ni za dhati, lazima tuzizungumzie na kukemea wale waovu wote wanaoingia katika Serikali na sehemu nyingine mbalimbali nchini na kuleta udhalilishaji mkubwa wa hivi, kwababu itakuwa ni kazi ya bure.

"Wazungu hawa tunawalaumu bure juu ya mambo haya ya ushoga na usagaji halifu ikajulikana wako baadhi ya viongozi wanaowafanyia wananchi tena kwa kuwarubuni na kuwatengenezea mazingira mabovu katika vizazi vyao kwasababu ya madaraka waliyobeba.

"Hivyo basi kwa kunyang’anywa nafasi hiyo, naendelea kusema tunakupongeza sana Mhe. Rais, sisi tunakuombea usonge mbele na Watanzania wako nyuma yako,” amesisitiza Mwinjlisti Temba.

Hata hivyo Mwinjilisti Temba ametumia fursa hiyo kumshauri Rais Dkt. Samia, kwamba umefika wakati sasa na Viongozi wa Dini wawe sehemu ya kufanya kazi za Serikali na kufafanua kuwa hakuna zuio lolote katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoeleza kwamba kiongozi wa Dini hawezi kuteuliwa na kuwa kiongozi Serikalini.

Kwamba tumeshaona viongozi mbalimbali wa dini wakiwa viongozi Serikalini akitolea mfano Getrude Rwakatare ambaye alikuwa ni Mbunge huku akiwa ni Mchungaji, Mchungaji Peter Msigwa na watumishi wengine wengi.

Hivyo amesema ni wakati wa Wakuu wa Mikoa, Wilaya na baadhi ya viongozi wengine hususan wa kuteuliwa, Rais ateue viongozi wa Dini wenye weledi na uwezo ili kuwasiadia wananchi na Taifa kwa ujumla.

Kwamba sio kwa Tanzania tu, bali hata nchi mbalimbali ikiwemo Zambia imekuwa na viongozi kama mawaziri ambao ni viongozi wa dini huku kwa Malawi Rais wa sasa wa Nchi hiyo, Dkt. Lazarus Chakwera akiwa ni Mchungaji na Askofu wa makanisa ya Assemblies Of God kadhalika na nchi nyingine mbalimbali kama vile Iran, Sudan.

Mwinjilisti Temba amesisitiza kwa kumuomba Rais Dkt. Samia kuchagua na kuwapa nafasi viongozi wa dini, kwamba watamsaidia kwani tayari wanazo karama zao za kutenda haki na sio kosa kwa wao kupata nafasi ndani ya Serikali. Amesema kuwa kwa sasa Watanzania wanahitaji viongozi wakweli na wenye hofu ya Mungu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news