Mheshimiwa Sagini afanya mazungumzo na Jaji Mkuu

DAR-Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Jumanne Abdallah Sagini tarehe 20 Juni, 2024 amemtembelea Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ofisini kwake kwa lengo la kufanya naye mazungumzo mafupi na kujifunza mambo mbalimbali ya kiutendaji.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Jumanne Abdallah Sagini (kushoto) akikaribishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alipomtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam tarehe 20 Juni, 2024.

Mhe. Sagini aliwasili katika ofisi ya Jaji Mkuu iliyopo kwenye jengo la Mahakama ya Rufani ya Tanzania jijini Dar es Salaam saa 4.15 asubuhi na kupokelewa na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya na Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. George Hillary Herbert kabla ya kukutana na Jaji Mkuu.

Baada ya utambulisho mfupi, Naibu Waziri ambaye aliambatana na Msaidizi wake, Bw. Amani Manyaga, alionesha kufurahishwa na maboresho makubwa yaliyofanywa na Mahakama ya Tanzania katika maeneo mbalimbali, ikiwemo miundombinu ya majengo na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (juu na chini) akisisitiza jambo alipokuwa anaongea na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Jumanne Abdallah Sagini.

Kufuatia hali hiyo, Mhe. Sagini akaomba kujua siri iliyouwezesha Mhimili huo wa Dola kufikia maendeleo makubwa ambayo yanachagiza kwa kiasi kikubwa na kwa haraka jukumu la utoaji haki kwa wananchi.
Mazungumzo yakiendelea.

Jaji Mkuu alimweleza mgeni wake historia ndefu na chimbuko la maboresho ndani ya Mahakama tangu mwaka 2010, lililoanza na mipango na mikakati iliyoandaliwa ili kuleta mageuzi chanya ndani ya Mahakama ya Tanzania ambayo yamekuwa mfano wa kuigwa na Taasisi nyingine Tanzania.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Jumanne Abdallah Sagini (juu na chini) akisisitiza jambo alipokuwa anaongea na Jaji Mkuu (hayupo katika picha).

“Kabla ya maboresho ya Mahakama, wote tulikuwa tunategemea maboresho yaliyokuwa yanaongozwa na Serikali Kuu, kupitia Wizara ya Katiba na Sheria na Utumishi wa Umma. Baada ya muda, tukaona changamoto za Mahakama zilikuwa nyingi ajabu, ukizitatua kwenye maboresho ambayo yanafanywa kwa wote unaweza usifanikiwe.

“Tuliamua kuwa na maboresho yanayoongozwa na Mahakama, iwe ni sehemu ya maboresho ndani ya Serikali, lakini tutengeneze barabara yetu ambayo itahusu matatizo halisi ya utoaji wa haki kupitia Mahakama.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya akitoa utambulisho wa Viongozi mbalimbali.

"Tuliangalia pia ukubwa wa nchi yetu, tulikuwa na muda wa kufikiri na kujadiliana, tukaja na Mpango Mkakati wa Mahakama wa miaka mitano mitano, kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo,” alisema.

Mhe. Prof. Juma alimweleza Naibu Waziri kitu kingine kilichosaidia kwa Mahakama kuja na maboresho hayo ni utafiti uliofanywa na Taasisi ya Repoa ambayo ilipita katika maeneo mbalimbali nchini kuwauliza wananchi wanataka Mahakama ifanye nini ili iweze kutekeleza haki.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Jumanne Abdallah Sagini (juu na chini) akisisitiza jambo alipokuwa anaongea na Jaji Mkuu (hayupo katika picha).

Alisema kuwa, taarifa ya Repoa iliainisha changamoto nyingi ambazo Mahakama ilikuwa nazo na matarajio ya wananchi, mambo ambayo yalijumuishwa kwenye Mpango Mkakati na kufanyiwa kazi na hivyo kuleta matokeo chanya na maboresho yanayoonekana hivi sasa.
Viongozi wa Mahakama ya Tanzania walioshiriki katika mazungumzo hayo. Kutoka kulia ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. George Hillary Herbert, Katibu wa Jaji Mkuu na Naibu Msajili, Mhe. Venance Mlingi na Katibu wa Msajili Mkuu na Naibu Msajili, Mhe. Dkt. Jovin Bishanga.

“Hata nyinyi Wizara kama mtataka kufanya maboresho, siyo vibaya mkaomba Taasisi ya nje ili iwaangalie. Unajua ukijiangalia mwenyewe ni ngumu, huwezi kuona mapungufu yako mwenyewe. Lakini mtu wa nje akikuangalia kutoka katika macho ya wananchi anaweza kukusaidia sana,” alimweleza Naibu Waziri.

Kadhalika, alimweleza kuwa utawala bora umekuwa pia siri ya usimamizi bora wa mageuzi na maboresho makubwa ndani ya Mahakama ya Tanzania yanaonekana kwa sasa. “Utawala bora siyo wa Viongozi, ni mfumo. Jaji Mkuu haingilii mambo ya miradi, kuna Mtendaji Mkuu wa Mahakama ambaye anaangalia mambo ya fedha, manunuzi na rasilimali watu,” alisema.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Jumanne Abdallah Sagini (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma. Picha chini, wakiwa na Viongozi wa Mahakama, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya (wa kwanza kushoto) na Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. George Hillary Herbert (wa kwanza kulia).
Jaji Mkuu alibainisha kuwa hatua hiyo imesaidia kujenga uaminifu kwa Benki ya Dunia ambao nao huwa wanakuja kila mara kukagua miradi ya majengo na watu wao ni sehemu ya usimamizi ili kuhakikisha utekelezaji unafanyika kwa ufanisi.

Viongozi wengine wa Mahakama ya Tanzania walioshiriki katika mazungumzo hayo ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. George Hillary Herbert, Katibu wa Jaji Mkuu na Naibu Msajili, Mhe. Venance Mlingi na Katibu wa Msajili Mkuu na Naibu Msajili, Mhe. Dkt. Jovin Bishanga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news