DAR-Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC),Dkt. Sophia Kongela amesema, miradi yote inayotekelezwa na shirika hilo nchini watahakikisha inatekelezwa kwa viwango vya Kimataifa.
Dkt.Kongela ameyasema hayo leo Juni 27,2024 jijini Dar es Salaam baada ya bodi hiyo kufanya ziara katika miradi ya shirika jijini humo.
"Tunajivunia juhudi zinazofanywa na timu yetu ya ujenzi na tunahakikisha kwamba miradi yote inatekelezwa kwa viwango vya kimataifa," amesema Dkt.Kongela.
Leo Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) imefanya ziara katika miradi mbalimbali ya shirika hilo iliyopo jijini Dar es Salaam kwa lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi.
Ziara hiyo iliyofanyika leo, ilianza saa nne asubuhi na kuwajumuisha wajumbe wote wa Bodi pamoja na viongozi waandamizi wa Shirika.
Katika ziara hiyo, Bodi ilipata fursa ya kutembelea miradi ya Kawe 711, Morocco Square, Samia Housing na eneo la NHC Urafiki ambayo inajumuisha ujenzi wa nyumba za makazi na biashara.
Viongozi wa NHC waliokuwepo katika ziara hiyo waliweza kutoa maelezo ya kina kuhusu changamoto zinazojitokeza katika ujenzi na hatua ambazo zimechukuliwa ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotarajiwa.
Bodi inaendelea na ziara katika miradi ya Samia, Morocco Square na Eneo la NHC Urafiki kufuatilia utekelezaji wa maelekezo na miongozo yake.
Ziara hii ni sehemu ya juhudi za NHC katika kuhakikisha kuwa inatoa suluhisho la makazi bora kwa wananchi na kusimamia rasilimali za umma kwa ufanisi na uwazi.
Tags
Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Nyumba la Taifa
Habari
Shiri la Nyumba la Taifa (NHC)
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)