IRINGA-Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff amemtaka Mkandarasi China Henan International Cooperation (CHICO) kupitia mradi wa RISE kuongeza kasi ujenzi wa barabara ya Mtili-Ifwagi Km 14 na Wenda-Mgama Km 19 zinazojengwa kwa kiwango cha lami mkoani Iringa.
Ameyasema hayo alipokuwa katika ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa barabara hizo wilayani Mufindi na Iringa.
Mhandisi Seff amemtaka Mkandarasi CHICO kufanya kazi usiku na mchana ili kufikia lengo kwa mujibu wa mpango kazi na kumaliza kazi kwa muda uliopangwa kwenye mkataba.
Mradi wa RISE una lengo la kuboresha barabara za vijijini, kuongeza fursa za ajira na kujenga uwezo wa kitaasisi.
Mradi huo unatekelezwa katika mikoa ya Iringa, Tanga, Geita na Lindi kwa ujenzi wa barabara Km. 500 na kuondoa vikwazo pamoja na kufanya matengenezo ya kawaida ya barabara kwa kutumia wananchi wanaoishi kandokando ya barabara za wilaya nchini.