NBS yatumia teknolojia kusambaza matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi nchini

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Fedha, Mheshimiwa Dkt.Mwigulu Lameck Nchemba amesema, hadi mwezi Aprili 2024, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imeendelea kusambaza matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi 2022 kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Ameyasema hayo leo Juni 4, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Fedha kwa mwaka 2024/2025.

Dkt.Nchemba amefafanua kuwa,katika mwaka 2023/24, Ofisi ya Taifa ya Takwimu ilipanga kusambaza matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022.

Vile vile, kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi ya takwimu za sensa, kuendelea kuandaa taarifa za sensa za kisekta kulingana na ratiba.

Sambamba na kufanya tafiti za kitaalamu kuhusu watu wenye uwezo wa kufanya kazi, mapato na matumizi ya kaya binafsi, ajira, mapato na ustawi wa watoto katika jamii.

"Hadi mwezi Aprili 2024, Ofisi ya Taifa ya Takwimu imeendelea kusambaza matokeo ya Sensa kwa kutumia teknolojia ikiwemo tovuti, kanzidata na programu tumizi kupitia simu za kiganjani kwa lengo la kuwafikia wadau wengi iwezekanavyo.

"Aidha, uchambuzi wa kina, kuandaa kanzidata ya viashiria vya watu wenye ulemavu, utoaji wa elimu na mafunzo kuhusu matumizi ya matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 umeendelea kufanyika."

Dkt.Nchemba amesema, uchambuzi unaoendelea kwa sasa ni takwimu za ndoa na uzazi, elimu, hali ya umaskini kwa kutumia viashiria visivyotumia fedha (non-monetary items) na makadirio ya idadi ya watu kuanzia mwaka 2023 hadi mwaka 2063.

"Kazi ya uchambuzi wa viashiria vilivyoainishwa katika dodoso la sensa imekamilika kwa asilimia 80 kama ilivyoainishwa katika Mwongozo wa Taifa wa Uchambuzi wa Matokeo ya Sensa ya Mwaka 2022 na ule wa Umoja wa Mataifa."

Kadhalika, amesema utoaji wa mafunzo kuhusu matumizi ya matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 umefanyika kwa asasi za kiraia kupitia vyama vinavyowaunganisha, viongozi wa kimila na mabalozi wa Tanzania nje ya nchi.

Waziri Dkt.Nchemba amesema,kazi nyingine zilizotekelezwa ni pamoja na Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria wa Mwaka-TDHS/MIS (2022).

Utafiti ambao ulikamilika na matokeo kuzinduliwa Oktoba 28, 2023, Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi wa mwaka 2024 na Utafiti wa Ajira na Mapato wa Mwaka 2023 katika Sekta Rasmi nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news