NHIF na ZHSF waja na taarifa njema kuanzia Julai Mosi

DODOMA-Kuanzia Julai Mosi, 2024 wanachama wa Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF) wanatarajiwa kuanza kupata huduma za matibabu kupitia vituo vilivyosajiliwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya nchini (NHIF).
Hayo yamebainishwa leo Juni 28, 2024 jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa NHIF,Bw. Bernard Konga baada ya NHIF na ZHSF kuingia mkataba wa makubaliano na mashirikiano kwa ajili ya utoaji wa huduma za matibabu kwa wanachama wa mfuko huo.

Konga ndiye aliyeongoza makubaliano na mashirikiano hayo kwa upande wa NHIF huku ZHSF ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Bw. Yaasin Juma.

Amesema, mwaka 2023 Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ilianzisha Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF) kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya, uhakika na endelevu kwa wananchi na wakazi wote wa Zanzibar bila kuwa na kikwazo cha fedha pale wanapozihitaji.

Sambamba na kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali fedha za kutosha katika kugharamia huduma za afya.

"Katika kuhakikisha kuwa ZHSF inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar Na. 1/2023 na kwa kutambua uzoefu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), katika uendeshaji wa mfumo wa bima ya afya nchini,
"Julai Mosi, 2024 ZHSF itaanza rasmi majukumu yake kwa kuhudumia wanachama na wategemezi wake kupitia vituo vya kutolea huduma vilivyosajiliwa na NHIF Tanzania Bara.

Amesema, hatua hii inatokana na uzoefu, wigo mpana wa vituo vya kutolea huduma vilivyosajiliwa na NHIF nchi nzima.

Pia, amebainisha kuwa, kwa upande wa NHIF, hatua mbalimbali za maandalizi na utayari wa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa mashirikiano zimefanyika ili kuhakikisha wanachama hao wanapata huduma bila ya changamoto yoyote.

"Masuala hayo ni pamoja na kutoa taarifa kwa watoa huduma wote kuhusu suala hili na wako tayari kuwahudumia wanachama, ofisi zote za NHIF zilizoko katika mikoa vote ziko tayari na zimejipanga kutoa huduma na kutoa msaada utakapohitajika."

Ameongeza kuwa, mifumo ya utambuzi imeimarishwa zaidi ili kurahisisha utambuzi wa wanachama wanapofika katika vituo vya kutolea huduma.

Vilevile wamejipanga kufanya malipo kwa watoa huduma kwa wakati pindi wanachama hao watakapopata huduma za matibabu katika vituo husika.
Jambo lingine amesema, ni kuandaa ofisi kwa aiili watumishi wa ZHSF watakaokuwa wanahudumia wanachama kwa upande wa Tanzania Bara.

"Wanachama wa ZHSF watapata huduma kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya tiba nchini kama inayotumika kwa wanachama wa NHIF."

Miongoni mwa taratibu ambazo zitatumika, Konga amesema,wanachama na wategemezi wa ZHSF watatumia kadi ya uanachama ya ZHSF badala ya kadi ya NHIF.

Aidha,vituo vitatumia mifumo ya utambuzi inayotumiwa na NHIF katika kuhakiki uhalali wa wanufaika.

"Na kutumia mfumo wa rufaa katika kupata huduma ambapo mwanachama anaweza kuanzia ngazi ya hospitali ya wilaya ama ngazi ya chini kupata huduma husika."

Katika kuhakikisha wanachama wanapata huduma wanazohitaji, Konga amefafanua kuwa, ZHSF na NHIF zimejipanga kwa kuweka Maofisa Maalum kutoka ZHSF ambao watakuwa katika Ofisi za NHIF kwa ajili ya kushughulia changamoto zinazojitokeza hususan za kihuduma.

"Aidha, kwa sasa hospitali nyingi za NHIF zinayo madawati maalum ya watumishi wake ambao moja ya majukumu yao ni kutoa usaidizi kwa wanachama wanaokwama ama kukutana na changamoto katika kupata huduma za matibabu.

"Mfuko unawahakikishia wanachama wake upatikanaji wa huduma bora Za matibabu katika vituo vyote wa kutolea huduma vilivyosajiliwa na mfuko.

"Endapo mwanachama atapata changamoto awasiliane na Kituo cha Huduma kwa Wateja bure kwa namba 199,"amesisitiza Mkurugenzi Mkuu wa NHIF.

ZHSF

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu ZHSF, Bw. Yaasin Juma amesema,taasisi hiyo ya umma ilianza utekelezaji wa majukumu yake kwa kuanza na usajili wa wanachama wa sekta ya umma Julai,2023 na Oktoba, 2023 huduma za matibabu kwa vituo vilivyosajiliwa na ZHSF zilianza kutolewa rasmi kwa upande wa Zanzibar.

"Mwezi wa Machi, 2024 ZHSF ilianza usajili wa sekta binafsi na huku tukiandaa mikakati ya kuelekea katika usajili wa sekta isiyo rasmi na makundi mengine yasiyokuwa na uwezo kama ilivyoelekezwa katika Kifungu cha 2 cha Sheria ya Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar Na.1 ya 2023.

"Katika kipindi cha mpito cha kuwafikia wanachama wetu walioko Tanzania Bara, tulishirikiana na wenzetu wa NHIF ili kuweka utaratibu wa muda wa kuwawezesha wanachama hao kupata huduma za afya, ambapo ZHSF ilikua ikilipa michango ya wanachama hao NHIF. "Vilevile, ZHSF na NHIF zilikua zikishirikiana kwa wanachama wote ambao kabla ya kuanzishwa kwa ZHSF walikua ni wanachama wa NHIF ambapo hadi sasa NHIF inaendelea kuwapatia huduma wanachama hao kwa kutumia kadi za NHIF."

Amesema, kwa mujibu wa kifungu cha 27 cha Sheria Na.1 ya 2023, Mfuko umepewa uwezo wa kuwafikishia wanachama wake huduma za afya nje ya Zanzibar, ambapo kwa kuanzia ZHSF imeanza kuwafikia wanachama wake walioko Tanzania Bara."

Mkurugenzi Mkuu huyo amesema, tukio la leo linaakisi utekelezaji wa masharti ya sheria hiyo.

"Hivyo basi, mafanikio haya ya kufikia makubaliano na wenzetu wa NHIF ni ya kujivunia kwani yatawawezesha wanachama wetu kupata huduma za afya wakiwa Tanzania Bara kwa kutumia kadi za ZHSF.

"Tunategemea mashirika yetu kama ZIC, PBZ ambayo yanafanyakazi Tanzania Bara na wategemezi ambao wachangiaji wao wapo Zanzibar watafaidika na huduma hizo.

"Kuanzia mwezi wa Julai, 2024 watumishi ambao walikuwepo NHIF kutoka sekta ya umma watarudi rasmi ZHSF na wafanyakazi wote waliopo sekta binafsi wataanza kupata huduma ZHSF kuanzia tarehe 1 Septemba, 2024. Vilevile ZHSF itafungua ofisi Tanzania Bara ili kuratibu kwa ukaribu masuala yetu".

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news