Ni bajeti ya maendeleo vijijini na mijini, wabadhirifu kumulikwa

NA GODFREY NNKO

SERIKALI imeliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuidhinisha bajeti ya shilingi trilioni 49.35 kwa mwaka 2024/25 ili kwenda kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu.
Hayo yamesemwa Juni 13,2024 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt.Mwigulu Lameck Nchemba wakati akiwasilisha hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali.

Dkt.Nchemba amesema, baadhi ya maeneo mahsusi yatakayopewa kipaumbele ni pamoja na kukamilisha miradi ya kielelezo na ile ya kimkakati.

Pia,kuimarisha sekta za uzalishaji,kuimarisha rasilimali watu hususani katika sekta za huduma za jamii nchini.

Nyingine ni kuongeza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji wa sekta binafsi.

"Aidha, maeneo mengine ya muhimu katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2024/25 ni kugharamia mishahara ya watumishi wa umma, deni la serikali.

"Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2024,maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na maandalizi ya michuano ya mpira wa miguu ya mataifa ya Afrika (AFCON) ya mwaka 2027 ikiwa ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa viwanja."

Vile vile Waziri Dkt.Nchemba amesema, Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwenye mifumo ya uendeshaji wa shughuli zake ili kudhibiti matumizi ya fedha za umma.

"Hata hivyo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali amekuwa akitoa hoja zinazohusu matumizi ya fedha za umma.

"Nipende kulihakikishia Bunge lako Tukufu na watanzania wote kuwa, Serikali makini ya Chama Cha Mapinduzi itaendelea kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti, Sura 439.

"Sheria ya Fedha za Umma, Sura 348, Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290,Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura 410, na Sheria ya Matumizi ya Fedha za Umma ya Mwaka 2024."

Aidha, Mheshimiwa Dkt.Nchemba amesema, Serikali itaendelea kuhakikisha sheria hizo zinasimamiwa na kutekelezwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na kujibu hoja zilizotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na hoja za wakaguzi wa ndani.

"Na endapo itabainika Afisa Masuuli wa Fungu husika ameshindwa kutekeleza matakwa ya sheria hizo, hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa.

"Niendelee kuwasisitiza Maafisa Masuuli kuzingatia Waraka wa Mkuu wa Utumishi wa Umma Na. 2 wa mwaka 2021 kuhusu utaratibu wa kutumia magari, aina na stahili za magari kwa viongozi katika utumishi wa umma kwa lengo la kupunguza matumizi.

"Aidha, hatua nyingine zitakazochukuliwa ni pamoja na kupunguza safari za ndani na nje na kupunguza ukubwa wa uwakilishi kwenye mikutano ya ndani na nje ya nchi.

"Vilevile, niendelee kuwasisitiza Maafisa Masuuli wote kuendelea kufanya vikao na mikutano kwa njia ya mtandao na kupunguza matumizi ya karatasi."

Wakati huo huo, Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba amesema, Serikali inaendelea kuchukua hatua kwa taasisi za Serikali zinazokiuka taratibu za ununuzi ikiwemo kufanya ununuzi bila kupata ridhaa ya bodi za zabuni.

"Nitoe wito kwa taasisi zote za Serikali kufuata taratibu za ununuzi wa umma na kuhakikisha kuwa ununuzi wote unaidhinishwa na Bodi za Zabuni.

"Hii itaongeza uwazi na uwajibikaji katika mchakato wa ununuzi na hivyo, kudhibiti matumizi mabaya ya rasilimali za umma.

"Aidha, nawaelekeza Maafisa Masuuli kuendelea kutumia Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma katika ununuzi wa bidhaa, huduma na kandarasi pamoja na kuzingatia bei ya soko wakati wa ununuzi."

Mheshimiwa Dkt.Nchemba amesema, Serikali itaendelea kutekeleza Mkakati wa Kugharamia Miradi ya Maendeleo kwa Kutumia Vyanzo Mbadala (Alternative Project Financing-APF) ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kupunguza utegemezi wa bajeti ya Serikali Kuu.

Amesema, mfano halisi wa utekelezaji wa mkakati huo ni kufanikiwa kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga (TANGA UWASA) kutoa hatifungani ya kijani yenye thamani ya shilingi bilioni 53.1.

Pia amesema, Serikali itaendelea kutoa mafunzo katika mamlaka za Serikali za mitaa, sekta binafsi na taasisi za fedha kuhusu ugharamiaji wa miradi kwa njia mbadala ikiwemo utekelezaji wa miradi kwa ubia baina ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP).

"Mwaka 2023/24, Serikali ilianzisha vitengo vya ufuatiliaji na tathmini katika wizara na taasisi zake ili kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa majukumu ya taasisi husika.

"Nipende kuwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuviongezea nguvu vitengo hivyo kwa kuvipatia rasilimali watu, fedha na vitendea kazi ili kuhakikisha shughuli zinazotekelezwa zinaakisi thamani halisi ya fedha.

"Tukitekeleza hatua hizo za kudhibiti matumizi ya fedha za umma, tutaokoa fedha ambazo zitaweza kuelekezwa kwenye miradi itakayosaidia jamii kama vile ujenzi wa barabara, vituo vya afya, miundombinu ya maji na shule.

"Aidha, niwasihi viongozi wenzangu kuona umuhimu wa kusimamia matumizi ya fedha za umma ili kuweza kuleta maendeleo kwa wananchi.

"Na niwaonye wale wachache wanaotumia vibaya fedha za umma waache mara moja.Na wale watakaobainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao,"amesisitiza Waziri Dkt.Nchemba.

Fedha za Kigeni

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Dkt.Nchemba ameelekeza kuanzia Julai Mosi, 2024 wadau wote wa ndani,taasisi za umma, wafanyabiashara,asasi za kiraia,mashirika ya kimataifa na watu wote waliopo nchini Tanzania wenye tabia ya kuweka bei kwenye huduma au kuuza bidhaa kwa fedha za kigeni waache.

Waziri amewataka bei za bidhaa na huduma hizo zitangazwe na kulipwa kwa shilingi ya Tanzania.

“Endapo una fedha za kigeni unatakiwa kuzibadilisha kupitia benki au maduka halali ya kubadilishia fedha ndipo ufanye malipo kwa kutumia shilingi ya Tanzania.

"Naielekeza Benki Kuu pamoja na vyombo vingine vinavyohusika kuendelea kudhibiti suala hili.

"Kufuatilia kwa ukaribu ili kubaini wote wanaoendelea kufanya makosa hayo na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria, tunafanya kila malipo kwa fedha za kigeni, halafu shilingi ikishuka thamani tunajiuliza tumekosea wapi.

“Watanzania tunalikuza tatizo la upungufu wa dola kwa baadhi ya watu kudai malipo au kufanya malipo ya bidhaa na huduma zinazotolewa ndani kwa kutumia fedha za kigeni yaani dollarization.

"Tasisi ipo Tanzania na pengine hata taasisi ya Serikali inamuuzia huduma Mtanzania inamwambia alipe kwa dola, taasisi nyingine zinataka mtu alipe ada kwa dola, alipe kodi ya nyumba kwa dola, vibali vya kazi, leseni na kadhalika kwa dola.

“Tunawafanya Watanzania wahangaike kuitafuta fedha za kigeni kununua huduma zinazotolewa ndani ya nchi yao badala ya kuwafanya wageni wahangaike kuitafuta shilingi ya Tanzania wanapotaka huduma ndani ya nchi.

"Jambo hili linasababisha kuongezeka kwa mahitaji yasiyo ya lazima ya fedha za kigeni na kuwanyima fursa watu wanaohitaji fedha za kigeni kwa ajili ya kulipia bidhaa na huduma muhimu kutoka nje ya nchi.

"Kitendo cha kuuza bidhaa au huduma za ndani kwa kutumia fedha za kigeni ni kosa kwa mujibu wa kifungu cha 26 cha sheria ya Benki kuu ya mwaka 2006 ambacho kinabainisha kwamba shilingi ya Tanzania ndiyo fedha halali pekee kwa malipo ya ndani ya nchi"

“Aidha, nazielekeza taasisi zote za Serikali zinazotoza ushuru, ada na tozo mbalimbali kwa fedha za kigeni kurekebisha kanuni zao ili tozo hizo zilipwe kwa shilingi, hata mgeni akija na fedha za kigeni ni vyema akaibadilisha kuwa fedha ya kitanzania ili aweze kupata huduma."

Usafirishaji

Amesema, ili kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji nchini pamoja na kuwawezesha wananchi kutekeleza shughuli zao za kiuchumi na kijamii, Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea na ujenzi na ukarabati wa barabara kuu, barabara za mikoa na madaraja.

Ni kupitia TANROADS pamoja na barabara za mijini na vijijini kupitia TARURA.

"Ni dhahiri Mama hasemi tu, bali anatekeleza. Niwape mfano mmoja, utekelezaji wa ujenzi wa Daraja la Kigongo-Busisi lenye urefu wa kilomita 3 na barabara unganishi yenye urefu wa kilomita 1.66 kwa kiwango cha lami umefikia asilimia 88.0 na jumla ya shilingi bilioni 426.1 zimetumika.

"Mradi huu unatarajiwa kukamilika mwaka 2024/25. 26. Kwa kutambua kuwa barabara za vijijini ni maisha, uchumi na usalama kwa watanzania tulio wengi, Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuiongeza bajeti ya TARURA kutoka shilingi bilioni 710.31 mwaka 2022/23, shilingi bilioni 825.09 mwaka 2023/24 hadi kufikia shilingi bilioni 841.19 kwa mwaka 2024/25.

"Bajeti hii itawezesha TARURA kuendelea na ujenzi, matengenezo pamoja na ukarabati wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji wa vijijini na mijini.

"Hii nayo inatuambia nini Mheshimiwa Spika? Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatosha kuiongoza Tanzania."

Mapendekezo

Kupitia Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148 139, Waziri wa Fedha, Dkt.Nchemba amependekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Sura 148 kama ifuatavyo:

i. Kufanya marekebisho kwenye Kipengele cha 18 cha Sehemu ya Kwanza ya Jedwali la Msamaha ili kujumuisha magari pamoja na vifaa vinavyotumiwa na Jeshi la Wananchi (military and armed forces).

Lengo la hatua hii ni kuwezesha Jeshi la Wananchi kutekeleza majukumu yake ya ulinzi na usalama wa nchi.

Aidha, msamaha utatolewa baada ya kupata uthibitisho wa Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Ulinzi ili kuhakikisha msamaha husika unatumika kwa manufaa ya Jeshi la Wananchi na si vinginevyo;

ii. Kujumuisha wazalishaji na waunganishaji wa ndege nchini kwenye wigo wa msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani unaotolewa kwenye matengenezo kinga ya ndege (aircraft mantainance), uuzaji na ukodishaji wa ndege, injini za ndege na vifaa vyake vinavyouzwa nchini.

Lengo la hatua hii ni kufanya wazalishaji na waunganishaji wa ndege nchini kuwa shindani sokoni, kuvutia uwekezaji nchini, kuchochea ukuaji wa tasnia ya Anga pamoja na kuunga mkono juhudi za kuhamasisha Sekta ya Utalii

Hatua hii inatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 7.1;

iii:Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye madawa ya kutibu na kusafisha maji, dira za maji na huduma ya uondoshaji wa maji taka (sewage).

Msamaha utatolewa kwa Mamlaka za Maji baada ya kupata ridhaa ya Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Maji.

Lengo la hatua hii ni kufanikisha utoaji wa huduma ya maji safi na salama nchini.

Iv: Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye uingizwaji wa vifaa vya kiteknolojia kwa ajili ya kuwasaidia waamuzi (Video Assistant Referee equipment and accessories).

Lengo la hatua hii ni kuhakikisha nchi inapata vifaa muhimu vya michezo kwa kuzingatia kuwa, Tanzania ni moja ya nchi mwenyeji zitakazohusika katika maandalizi ya michuano ya fainali ya kuwania kombe la mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027 na hivyo kunufaika na ongezeko la akiba ya fedha za kigeni.

Pia, kukuza taswira ya nchi kimataifa na uwepo wa fursa kwa makampuni ya ndani kutangaza biashara zao.

Aidha, msamaha utatolewa baada ya vifaa hivyo kupata idhini ya Waziri mwenye dhamana ya masuala ya michezo ili kuhakikisha kuwa msamaha huo unatumika kama ilivyokusudiwa na si vinginevyo;

v.Kuweka takwa la marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT Refunds) kulipwa ndani ya siku 30 kutoka tarehe ya kuwasilishwa kwa maombi ya marejesho hayo.

Hatua hii inalenga kuchochea ulipaji kodi wa hiari na kuongeza uwajibikaji kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania.

Vi:Kujumuisha trekta lenye ekseli moja (single axle tractors/ power tiller) linalotambulika kwa HS Code 8701.10.00 kwenye wigo wa zana na vifaa vya kilimo vinavyopata msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani.

Marekebisho haya yanalenga kuakisi mawanda ya bidhaa zilizosamehewa pamoja na kuoanisha H.S Codes zilizomo kwenye kitabu cha Viwango vya Pamoja vya Ushuru cha Jumuiya ya Afrika Mashariki (East African Community Common 83 External Tariff) cha mwaka 2017 na zile zilizomo kwenye kitabu cha mwaka 2022;

vii. Kufanya marekebisho kwenye Sehemu ya Kwanza ya Jedwali la Misamaha ya Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa kuondoa baadhi ya vifaa vyenye matumizi mbadala kwenye wigo wa vifaa vya kilimo vinavyopata msamaha wa kodi.

Vifaa hivyo vinatambulika kwa HS Code 8201.10.00 (chepe); 8201.30.00 (sururu).

Lengo la hatua hii ni kuendana na azma ya Serikali ya kupunguza misamaha isiyo na tija kwa lengo la kulinda mapato ya Serikali na kupunguza matumizi yanayohusiana na utoaji wa misamaha ya kodi (tax expenditure).

Aidha, tathmini iliyofanywa imebaini kuwa, msamaha husika haujafikia malengo kutokana na vifaa hivyo kuwa na matumizi mbadala.Endelea hapa》》》

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news