Ni jukumu letu kulipa kodi kwa haki kuendana na sheria za nchi

NA GODFREY NNKO

SERIKALI kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuhakikisha inakusanya kodi zote nchini kwa mujibu wa sheria.

TRA imekuwa ikifanya hivyo, ili kuiwezesha Serikali kupata mapato ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ile ya kimkakati na huduma za kijamii.

Ni makusanyo yanayofanyika kupitia kodi inayolipwa moja kwa moja, na kodi inayolipwa kupitia kwenye bidhaa kwa maana ya kodi ya nyongeza ya thamani.

Ili kuweza kufanikisha hilo, kwa nyakati tofauti, viongozi wa juu serikalini wamekuwa wakiielekeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuendelea kukusanya kodi kwa weledi kwa kutafuta njia ya majadiliano na wafanyabiashara wanaokiuka taratibu badala ya kufunga biashara zao.

Pia, Serikali imekuwa ikiwataka wafanyabiashara kufanya biashara zao kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni zilizopo ili kuepusha misuguano isiyo ya lazima na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Vile vile, wananchi wamendelea kuhimizwa kuwa wazalendo kwa kulipa kodi stahiki na kwa wakati, kudai risiti halali kulingana na kiwango cha fedha walichotoa na wafanyabiashara kufanya matumizi sahihi ya mashine za kutolea risiti kwa njia ya kielekroniki (EFDs) pamoja na kutoa risiti halali kwa wateja wao.

Rais Dkt.Samia

Aprili 10, mwaka huu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Baraza la Eid El Fitri ambalo lilifanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam aliendelea kuhimiza ulipaji kodi kwa hiari.
Mheshimiwa Rais Dkt.Samia alitumia baraza hilo kufikisha ujumbe kwa Watanzania ili waweze kutambua umuhimu wa kulipa kodi sahihi na kwa wakati.

"Inasikitisha kuona kwamba baadhi ya wafanyabiashara wanatumia mbinu mbalimbali kukimbia kulipa kodi, hawatoi risiti, wanapouza au wakitoa risiti ni zenye upungufu.

"Na wanunuzi wa bidhaa nao, hawadai risiti wanaponunua bidhaa au huduma,naomba mniruhusu nilitumie jukwaa hili kusema kwamba, ulipaji wa kodi ni jambo la halali kidini.

"Mwenyenzi Mungu ametuwekea mfumo madhubuti wa kiuchumi, unaoeleza namna ambavyo Hazina za Serikali zinavyopaswa kukusanya kodi ili nchi ipate uwezo wa kuwahudumia wananchi wake.

"Hivyo basi, ni jukumu la kila mmoja wetu kupitia shughuli mbalimbali ambazo tunazifanya za kibiashara, kulipa kodi kwa haki kuendana na sheria za nchi.

"Hapa nieleze kwamba, nilikataa kodi za dhuluma ili tuendane na misingi ya haki,lakini inasikitisha kuona kwamba wafanyabiashara wetu, sasa wamegeuza tumekataa kodi za dhuluma kama Serikali, wafanyabiashara wanafanya dhuluma ya kodi.

"Wanadhulumu kulipa kodi, dhuluma ya kodi. Wanadhulumu mapato ambayo yangetumiwa kuhudumia wananchi."

Makamu wa Rais

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Philip Isdor Mpango akiwa mgeni rasmi katika kilele cha Maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi (Mei Mosi) ambayo kitaifa yalifanyika Mei Mosi, 2024 mkoani Arusha naye aliendelea kukumbushia umuhimu wa kulipa kodi.

"Napenda nichukue fursa hii, kutambua mchango mkubwa sana wa wafanyakazi katika ulipaji wa kodi,kimsingi wafanyakazi ni miongoni mwa walipaji wazuri wa kodi na mnayo kila sababu ya kujipongeza kwa mchango wenu adhimu kwa Taifa.

"Kupitia sherehe hizi za Mei Mosi, ninaomba niendelee kuyasii makundi mengine katika jamii yetu, kutimiza wajibu wao wa kisheria kulipa kodi kwa maendeleo ya Taifa.

"Ninapenda nitumie fursa hii pia kuwasihi wafanyakazi wote nchini kuwa mstari wa mbele katika kudai risiti kila wanaponunua bidhaa au huduma na wahakikishe risiti wanazopewa zimeandikwa gharama halisi.

"Kwa kufanya hivyo, siyo tu tutaiwezesha Serikali kupata mapato zaidi ya kuimarisha ustawi wa jamii ambayo wafanyakazi ni sehemu yake, bali pia itaipa Serikali wigo mpana zaidi wa kuboresha maslahi ya wafanyakazi,"anasisitiza Makamu wa Rais Dkt.Mpango.

Waziri wa Fedha

Kutokana na jitihada ambazo zinafanywa na Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt.Mwigulu Lameck Nchemba amesema, hadi Aprili 2024,TRA imekusanya jumla ya shilingi trilioni 21.3 sawa na ufanisi wa asilimia 96.9 ya lengo la Julai 2023 hadi Aprili 2024 na asilimia 79.8 ya lengo la mwaka.

Ameyasema hayo Juni 4, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Fedha kwa mwaka 2024/2025.

Dkt.Nchemba amesema, katika kuimarisha na kuboresha mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji wa mapato,mamlaka imeanza ujenzi wa Mfumo wa Usimamizi wa Kodi za Ndani (IDRAS) ambao ni mahsusi kwa usajili, ukadiriaji, ukusanyaji wa kodi na ufuatiliaji wa walipakodi.

"Mafanikio mengine yaliyopatikana ni kutekeleza mradi wa kuunganisha mifumo ya ndani na taasisi nyingine za serikali ikiwemo mfumo wa kuzalisha vitambulisho vya Taifa-NIDA na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).

"Na kuboresha moduli ya lango la huduma kwa mlipakodi na moduli ya uwasilishaji wa ritani za kieletroniki kwa mapato ya ndani."

Waziri Dkt.Nchemba amesema, hatua zilizochukuliwa kudhibiti uvujaji na upotevu wa mapato ni pamoja na kuanzisha divisheni mpya ya walipakodi wa kati na wadogo chini ya Idara ya Kodi za Ndani.

Pia, kuimarisha mifumo ya kubadilishana taarifa na wadau wa ndani na nje ya nchi, kuchukua hatua za kinidhamu na kisheria dhidi ya vitendo vinavyoashiria ukwepaji kodi.

Sambamba na kuendelea kuhamasisha wananchi kuhusu masuala ya kodi hususani umuhimu wa kudai na kutoa risiti za kielektroniki (EFD) na matumizi na uhakiki wa stempu za kielektroniki (ETS).

"Aidha, mamlaka imetoa elimu ya kodi kwa walipakodi kupitia njia mbalimbali ikiwemo semina, vipindi vya redio na televisheni, matangazo ya kodi, mikutano ya wadau wa kodi, kampeni, mitandao ya kijamii na vipeperushi."

Wakati huo huo, Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba amesema, hadi Aprili 2024, Bodi ya Rufani za Kodi imepokea mashauri ya kodi 437 ya kodi bishaniwa ya shilingi bilioni 3,456.5 na imesikiliza na kutolea uamuzi mashauri 388 ya kodi bishaniwa ya shilingi bilioni 2,780.1 na dola za Marekani 439,281.

Aidha, Baraza la Rufani za Kodi limesajili jumla ya mashauri 112 ya kodi bishaniwa ya shilingi bilioni 2,790 ambapo mashauri 64 ya kodi bishaniwa ya shilingi bilioni 137.9 yamesikilizwa na kutolewa maamuzi na mashauri 56 ya kodi bishaniwa ya shilingi bilioni 2,510 yako katika hatua mbalimbali za usikilizaji na kutolewa maamuzi.

Vilevile, Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi imepokea malalamiko 40, imesuluhisha malalamiko 22 na malalamiko 18 yapo katika hatua mbalimbali za usuluhishi.

"Kadhalika,taasisi imeanzisha mfumo wa kupokea malalamiko kwa njia ya simu (call center) ambapo mlalamikaji au mtoa taarifa anaweza kuwasilisha malalamiko kwa kupiga simu ya bure namba 0800111022."

Amesema,jitihada hizo zimewezesha ongezeko la mwamko wa wananchi na walipakodi kuwasilisha malalamiko yao kwa uhuru na uwazi.

"Ili kuhakikisha walipakodi wanakuwa na uelewa na kunufaika na huduma zinazotolewa, Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi imeendelea kujitangaza kupitia vyombo mbalimbali vya habari.

"Ikiwa ni pamoja na kufanya vikao na wahariri wa vyombo vya habari na vikundi vya wafanyabiashara katika Mkoa wa Dar es Salaam kuhusu uwepo wa ofisi, majukumu yake na namna ya kuwasilisha malalamiko."

Waziri Dkt.Mwigulu amesema, pia taasisi hiyo imeshiriki katika mikutano mbalimbali ya umoja wa wafanyabiashara katika mikoa ya Shinyanga, Kigoma, Mbeya, Mtwara, Lindi na Dar es Salaam kwa lengo la kutoa elimu ya usuluhishi wa masuala ya kodi.

Mwaka ujao

Waziri wa Fedha, Dkt.Mwigulu amesema, katika mwaka 2024/25, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inatarajia kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ya jumla ya shilingi trilioni 29.42.

Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 28.87 ni mapato ya kodi na shilingi bilioni 541.10 ni mapato yasiyo ya kodi.

Aidha, amesema mamlaka itaendelea kutekeleza mkakati wa kudhibiti biashara za magendo ili kupunguza mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali.

Vilevile, mamlaka inatarajia kupokea jumla ya shilingi bilioni 25.97 kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo kuimarisha na kuboresha mifumo ya usimamizi wa mapato ya Serikali, kununua vitendea kazi na kuboresha mazingira mahali pa kazi, hususani majengo ya ofisi.

Waziri Dkt.Nchemba amesema, katika mwaka 2024/25, Bodi ya Rufani za Kodi inatarajia kusajili, kusikiliza na kutolea maamuzi mashauri ya kodi yanayotokana na maamuzi ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania.

Pia, kuandaa Juzuu ya Taarifa za Sheria za Kodi Tanzania na kuhuisha Sheria ya Rufani za Kodi, Sura 408 pamoja na kanuni zake.

Vilevile, Baraza la Rufani za Kodi linatarajia kusajili, kusikiliza na kutolea maamuzi mashauri ya kodi yanayotokana na maamuzi ya Bodi ya Rufani za Kodi.

Kadhalika, amesema Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi inatarajia kutoa elimu kwa umma kuhusu majukumu ya taasisi.

Ikiwemo kupokea na kutatua malalamiko ya walipakodi, kukamilisha ujenzi wa mfumo wa kupokea na kuchakata malalamiko, kuratibu kutungwa kwa sheria mpya ya taasisi na kujenga uwezo kwa watumishi katika maeneo ya uendeshaji na usuluhishi wa malalamiko.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news