NA JAMES MWANAMYOTO
OR-TAMISEMI
NAIBU Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Elimu) Dkt. Charles Msonde amesema, mwalimu ni mtumishi mwenye hadhi kama walivyo watumishi wenginge hivyo ni lazima ajibiwe kwa staha na viongozi wote wakiwemo wakurugenzi wa halmashauri, maafisa elimu wa ngazi zote pamoja na watumishi wengine wa Serikali.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Elimu) Dkt. Charles Msonde akizungumza na Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Walimu waliopo Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu (hawapo pichani) wakati wa kikao kazi chake na maafisa hao.
Dkt. Msonde ametoa wito huo kwa nyakati tofauti kwa viongozi na watumishi wa umma nchini, wakati wa vikao kazi vyake na Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Walimu waliopo katika halmashauri za wilaya ya Kasulu, Kasulu Mji na Buhigwe.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Elimu) Dkt. Charles Msonde akizungumza na Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Walimu waliopo Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu (hawapo pichani) wakati wa kikao kazi chake na maafisa hao.
“Mwalimu akija na changamoto zake, ni wajibu wetu sisi tunayemuhudumia kumjibu kwa staha kama tunavyowajibu watumishi wengine tunaowathamini,” Dkt. Msonde amesisitiza.
Dkt. Msonde amesema, ukiwa wewe ndio afisa elimu au afisa taaluma kuna ubaya gani ukampokea na kumuhudumia vizuri mwalimu kwani hautopungukiwa na chochote na cheo chako utabaki nacho.
Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Walimu waliopo Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Elimu) Dkt. Charles Msonde (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi chao na Naibu Katibu Mkuu huyo.
Dkt. Msonde amefafanua kuwa, kupitia azimio la Tabora iliafikiwa kuwa, mwalimu ni lazima aishi kwa amani na wala asinyanyaswe au kunyanyasika ili aweze kutekeleza kikamilifu jukumu la kufundisha na kulea watoto ambalo alipewa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere ambaye alithamini na kutambua mchango wa walimu katika maendeleo ya taifa.
Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Walimu waliopo Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Elimu) Dkt. Charles Msonde (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi chao na Naibu Katibu Mkuu huyo.
“Tuliamini kwamba, viongozi wa elimu katika ngazi ya mkoa, halmashauri, kata na shule wakijenga utamaduni wa kupendana na kuheshimiana, ni wazi kuwa na wengine wataunga mkono kwa kuuishi utamaduni huo,” Dkt. Msonde amefafanua.
Afisa Elimu wa Mkoa wa Kigoma Bi. Paulina Ndigeza akitoa neno la shukrani kwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Elimu) Dkt. Charles Msonde (hayupo pichani) mara baada ya Naibu Katibu Mkuu huyo kufanya kikao kazi na Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Walimu waliopo Halmashauri za Wilaya ya Kasulu, Kasulu Mji na Buhigwe.
Dkt. Msonde amefanya vikao kazi na Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Walimu waliopo katika Halmashauri za Wilaya ya Kasulu, Kasulu Mji na Buhigwe, ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake mkoani Kigoma iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa maafisa hao.