Ni Sako kwa Bako, hatimaye Rais Dkt.Samia ametafuna mfupa mgumu wa Same kuhusu maji

NA FLORENCE LAWRENCE

KWA somo la Kiswahili, Mradi wa maji wa Same ni kama ‘Kitendawili kilichokuwa kimetegwa” na kimefanyiwa kazi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, ambaye hatimaye ametegua kitendawili hicho cha muda mrefu kuhusu huduma ya maji kwa wakazi wa Same ambao macho na masikio muda wote yalielekea katika mradi wa maji wa Same-Mwanga -Korogwe.
Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango hivi karibuni akishuhudia huduma ya majisafi katika makazi ya wananchi, maji hayo yanatoka katika mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe.

Mradi huu ndio tegemea kubwa kwa wakazi wengi wa eneo hili ambalo lina changamoto ya uhaba wa huduma ya maji. 

Sasa inaweza semwa, hilo ni fupa ambalo lilisumbua sana, lakini hivi sasa Rais Samia amelitafuna, kama biskuti na maji yanaingia katika matenki kabla ya kufikisha kwa wananchi.

Ni Dhahiri, ‘hayawi hayawi na sasa yamekuwa na mwenye macho haambiwi tazama’, Viongozi na wataalam wa Sekta ya Maji wamefanya kazi kwa saa 24 na huduma ya maji imewafikia wananchi kama ilivyoelekezwa na Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, ambaye muda wote amesisitiza kwa msemo “kumtua mama ndoo ya maji kichwani”. 

Na sasa kina mama wanaotegemea mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe wana kila sababu ya kufurahi na kujipongeza kwa huduma ya uhakika ya maji katika makazi yao.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewapongeza viongozi wa Wizara ya Maji kwa kusimamia na kufanikisha vema utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Same -Mwanga – Korogwe.

Ametoa pongezi hizo alipokagua mradi huo na kujionea wananchi wakianza kunufaika na maji kwa mara ya kwanza katika Mradi wa Maji wa Same – Mwanga – Korogwe ambao umefikia asilimia 95 ya utekelezaji. 

Pamoja na hayo ameipongeza Wizara ya Nishati kwa kufanikisha ujenzi wa kituo cha kupoozea Umeme cha kuhudumia mradi.

Pamoja na maji kuanza kutoka, ameiagiza Wizara ya Maji kuhakikisha vijiji vyote vinavyozunguka mradi huo vinanufaika na maji safi na salama yatokanayo na mradi huo ili waweze kutunza vyanzo vya maji na miundombinu ya mradi huo. 

Wataalam wa rasilimali za maji katika maandiko mbalimbali wanasisitiza utunzaji wa vyanzo, moja ya faida yake ni kuwa na miradi endelevu yam aji katika jamii.

Makamu wa Rais amewasihi wananchi wa Same na Mwanga kuanza kutumia vema maji ya mradi ili kuhifadhi mazingira ikiwemo kupanda miti katika maeneo yao. 

Aidha, amewataka viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro kuandaa malambo kwa ajili ya kunywesha mifugo ili kulinda mradi huo wa maji dhidi ya unyweshaji mifugo katika chanzo chake.

Pia amewahimiza wananchi wanaozunguka mradi wa maji wa Same – Mwanga – Korogwe kuhakikisha wanakuwa walinzi wa mradi huo ili uweze kudumu na kuwanufaisha kwa muda mrefu.

Kwa upande wake Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amewataka watendaji wa Sekta ya Maji kuhakikisha wanawaunganisha wananchi wa Mwanga na Same kupata huduma ya maji kwa wakati. 

Pia amewasihi watendaji katika sekta hiyo kuzingatia utoaji wa ankara sahihi kwa wananchi wakati Wizara ya Maji (ikiendelea na utaratibu wa kufanikisha Dira za maji za malipo ya kabla.

Kudhihirisha kuwa Serikali imefanikisha jambo hili, Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) awali, mapema mwezi Juni 2024 aliwasha pampu za kusukuma maji kwenda katika matanki ikiwamo Kivengere. 

Hizo zilikuwa dalili njema kwa wananchi kuwa sasa wakae mkao wa kula kwani maji mengi ya kutosha yanafikishwa na Serikali.

Kabla ya kuwasha pampu hizo, Aweso alijionea kazi iliyofanywa na wataalam katika mradi huo ikiwamo ulazaji wa mabomba na kuona utekelezaji wake kwa kushudia kukamilika kwa mifumo ya kutibu maji, jambo ambalo ni muhimu kabisa kwa usalama wa walaji wa huduma ya maji.

Ikumbukwe kwa Jiografia eneo hilo la Same lina hali ya ukavu, hasa eneo la tambarare. Hivyo huduma ya maji ni moja ya bidhaa muhimu kabisa kwa wananchi, kama tukiongelea suala la biashara, maji nayo ni bidhaa yenye uhitaji mkubwa kutokana na mazingira ya eneo.

Rais Samia alituma ujumbe mahsusi kupitia kwa Makamu wa Rais Mhe Dkt. Philip Mpango alielekeza kwa Wizara ya Maji kuhakikisha mwezi Juni 2024 wananchi wa Same - Mwanga wanapata huduma ya uhakika ya majisafi na salama. 

Hivyo, zigo hilo la kupambana katika mradi, usiku na mchana likabebwa na Waziri Aweso, kwa kuweka wataalam wa Wizara ya Maji kufanikisha maelekezo ya viongozi, na kuwafikia wananchi kwa huduma ya majisafi ya uhakika.

Moja ya aliyofanya Waziri Aweso kufanikisha hilo, ni kuwashirikisha wataalam wa Sekta ya Maji, mwanzo hadi mwisho wa kazi, na kuwapa morali ya kazi, kwa kutekeleza kazi za mradi kwa saa 24. 

Na yeye mwenyewe kuwepo eneo la ujenzi ili kuhakikisha kuwa ndoto ya kuwafikishia wananchi maji inafanikiwa, akisema “Baada ya dhiki ni faraja” na Wizara yake haiwezi kuwa kikwazo katika kufikisha huduma yam aji kwa wananchi, kwani kama ni mradi umechukua muda mrefu bila kuwa na matokeo katika jamii, sasa imefika mwisho n ani faraja kubwa kwa Serikali na wananchi wake.

Kabla ya mwendo wa kazi kwa usiku na mchana, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango alitembelea mradi wa maji wa Same - Mwanga - Korogwe na alisema mradi huo lazima ukamilike, na endapo sivyo ataacha kazi.

Nani kunufaika na mradi?

Mradi huo ambao umepangwa kunufaisha miji ya Same na Mwanga pamoja na vijiji 38 kwenye Wilaya ya Same na Mwanga na vijiji vitano katika Wilaya ya Korogwe, sasa umepata majawabu ukiwa zaidi ya asilimia 90 ya utekelezaji wake.

Mhe. Mpango alielekeza kwa watendaji wa Serikali pamoja na wakandarasi kuhakikisha wanafanya kazi usiku na mchana ili mradi uweze kukamilika kwa muda uliopangwa na wananchi waweze kupata huduma ya maji.

"Serikali imefanya kazi kubwa kuhakikisha huduma ya maji inamfikia kila Mtanzania, hivyo niwaombe mfanye kazi ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji ifikapo Juni 2024,” Mhe. Dkt. Mpango alisema, na hili limetimizwa kwa pampu kuwasha na kuanza kusukuma maji.

Akipokea maelekezo, Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso alimhakikishia Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Mpango kuwa Wizara ya Maji itaendelea na jitihada za kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa muda uliopangwa ili wananchi wapate huduma ya maji ipasavyo.

"Nikuhakikishie Mhe. Makamu wa Rais kuwa, Wizara ya Maji imejipanga na hivyo tunasimamia maagizo uliyotupa ili kuhakikisha utekelezaji wa mradi huu unakamilika," ameeleza Mhe. Aweso.

Serikali ya Awamu ya Sita inafanikisha kazi ya huduma ya maji katika Mradi wa maji Same Mwanga - Korogwe kwa gharama ya shilingi bilioni 262 na unatarajia kuwanufaisha wananchi zaidi ya 400,000. Huu ni moja kati ya miradi makubwa yam aji iliyofanikishwa na Serikali.

Tunaposema Rais Samia ametafuna ‘fupa’ la Same sio jambo la utani, huu ni ukweli na moyo wake wa dhati katika kumhudumia kila Mtanzania unapozungumzia suala la huduma ya maji yaani ‘kumtua mama ndoo ya maji kichwani’.

Mradi huo umesubiriwa kwa miaka 19 tangu ulipoahidiwa kwa mara ya kwanza, hivyo ni wakati wa kuhakikisha mradi huo unakamilika. Kutokana na hilo, Dkt. Mpango pamoja na kutaka watendaji wa Sekta ya Maji kuweka kambi katika mradi huo, nao uongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro ulipewa jukumu la kuhakikisha ulinzi wa mazingira na chanzo cha maji katika mradi huo ili kuwa endelevu.

Chanzo cha mradi ni kipi?

Chanzo cha maji kwa mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe ni bwawa la Nyumba ya Mungu lililopo wilayani Mwanga mkoa wa Kilimanjaro. 

Pamoja na matumizi mengine kwa maendeleo ya jamii, bwawa hilo linatumika kufua umeme unaotumika katika uzalishaji mali viwandani na majumbani.

Hivyo, kutumia uwekezaji huo wa serikali katika huduma ya maji nayo ni chemsha bongo ya kutumia maji mengi ya mvua na mafuriko kama fursa na sio laana katika jamii.

Mradi wa maji wa Same-Mwanga -Korogwe ulianza ukiwa na Wakandarasi watatu na chanzo cha maji cha mradi huo kinauwezo wa kuzalisha maji lita milioni 103. 

Kiwango hicho ni toshelevu kwa wanufaika wa mradi huo ambao wameusubiri kwa miaka kadhaa sasa, na faraja imebisha hodi nyumbani.

Uhalisia kuhusu maji

Maji ni muhimu kwa maisha na kudumisha mazingira, maji yanatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi wa nchi ya Tanzania. Ni wazi kuwa yanagusa nyanja zote za maisha ikiwemo nyumbani, kilimo, mifugo, uvuvi, viwanda, wanyamapori, nishati, michezo na burudani na shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii.

Kwa kuzingatia umuhimu wa maji kwa maisha ya watu na mazingira, Wizara ya Maji ina Maabara za Ubora wa maji katika kuhakikisha usalama wa maji, pia usimamizi wa rasilimali za maji, kwa manufaa ya wananchi na nchi jirani hususan maji ya kimataifa ambayo huvuka mipaka ya nchi zaidi ya moja. Matumizi yam aji ni muhimu yawe kwa usawa bila kuumiza eneo moja au sekta nyingine, na maji ya kimataifa. 

Hivyo, matumizi ya maji yanaangaliwa na utunzaji pamoja na kuendeleza vyanzo vyake ili viwe endelevu.

Kipaumbele cha Tanzania kuhusu maj

Hivi karibu, akiwasilisha mpango wa Wizara ya Maji 2024-2025 Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) alisema moja ya vipaumbele vya Wizara ya Maji ni kufikisha huduma yam aji katika vijiji ambavyo bado havijapata huduma hiyo.

Pia, kuendelea na maandalizi ya kuwa na Mtandao wa Taifa wa Maji (National Water Grid). Lengo la mtandao huo, ni kuwa na miundombinu ya kusafirisha maji kutoka kwenye vyanzo vya uhakika ikiwemo maziwa na mito na kuyapeleka kwenye maeneo yenye uhaba wa maji.

Alisema hadi sasa, Wizara ipo katika hatua za kumwajiri Mtaalam Mshauri kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na kuandaa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya kuajiri wataalam washauri watakaofanya usanifu wa kina ambapo nia ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali kubwa ya maji iliyopo na imeanza kutumia vyanzo vya maji vya uhakika mfano ni miradi ya kutoa maji Ziwa Victoria kwenda maeneo mbalimbali ikiwemo miji ya Kahama, Shinyanga, Tinde, Nzega, Tabora, Igunga, Shelui, Uyui, Kaliua na Urambo. Aidha, upembuzi yakinifu wa kutoa maji Ziwa Tanganyika na kuyapeleka katika mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa umekamilika na taratibu za kumpata mtaalam mshauri atakayefanya usanifu wa mradi zinaendelea.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news