NSSF yazidi kujiimarisha kwa ustawi bora wa wanachama

NA GODFREY NNKO

MWAKA 2022/23, Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ulisajili wanachama wapya 243,895 ikilinganishwa na wanachama wapya 233,643 walioandikishwa mwaka 2021/22 sawa na ongezeko la asilimia 4.4.

Katika kipindi hicho, wanachama wachangiaji wa mfuko walifikia 1,189,222 kutoka wanachama 1,039,183 mwaka 2021/22 sawa na ongezeko la asilimia 14.4.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Alexander Mkumbo ameyasema hayo Juni 13, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya uchumi wa nchi kwa mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2024/25.

Amesema,ongezeko hilo lilichangiwa na ukuaji wa shughuli za sekta binafsi pamoja na uwekezaji.

"Mwaka 2022/23, mfuko ulikuwa na wastaafu 28,820 ikilinganishwa na wastaafu 25,608 waliokuwepo mwaka 2021/22, sawa na ongezeko la asilimia 12.5."

Aidha, mafao yaliyolipwa kwa wanachama yaliongezeka kwa asilimia 12.0 na kufikia shillingi bilioni 738.61 mwaka 2022/23 ikilinganishwa na shilingi bilioni 659.77 mwaka 2021/22.

"Hii ilichangiwa na kuongezeka kwa maombi ya fao la ukosefu wa ajira na idadi ya wastaafu. Mwaka 2022/23, mapato halisi yatokanayo na uwekezaji wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii yaliongezeka kwa asilimia 20.5 na kufikia shilingi bilioni 380.63 ikilinganishwa na mapato ya shilingi bilioni 315.77 mwaka 2021/22.

"Ongezeko hilo lilichangiwa na uwekezaji uliofanywa na mfuko katika hatifungani za Serikali."

Aidha, thamani ya vitega uchumi vya mfuko iliongezeka kwa asilimia 21.0 na kufikia shilingi trilioni 6.880 mwaka 2022/23 kutoka shilingi trilioni 5.687 mwaka 2021/22.

Waziri Prof.Mkumbo amesema,hayo yalitokana na ongezeko la michango ya wanachama pamoja na uwekezaji uliofanywa na mfuko katika hatifungani za Serikali.

"Mwaka 2022/23, Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii ulikusanya michango kutoka kwa wanachama kiasi cha shilingi bilioni 1,719.25 ikilinganishwa na shilingi bilioni 1,419.71 zilizokusanywa mwaka 2021/22, sawa na ongezeko la asilimia 21.1.

"Ongezeko hilo lilichangiwa na ukuaji wa shughuli za sekta binafsi, maboresho ya mifumo ya ukaguzi na matumizi ya TEHAMA."

Kwa upande mwingine, thamani ya mfuko iliongezeka kwa asilimia 18.0 na kufikia shilingi trilioni 7.2 mwaka 2022/23 kutoka shilingi trilioni 6.1 mwaka 2021/22.

"Ongezeko hilo lilitokana na kukua kwa thamani ya uwekezaji wa mfuko na kuongezeka kwa michango ya wanachama."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news