DAR-Ofisi ya Msajili wa Hazina ipo katika hatua za mwisho za kuwa na mfumo thabiti wa kuripoti taarifa za kiutendaji za wakuu wa taasisi kwa wakati na za kuaminika ili kuwezesha kufanyika maamuzi sahihi kwa wakati kwa mamlaka za uteuzi.
Hayo yalisemwa Juni 11,2024 jijini Dar es Salaam na Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu wakati akizungumza katika hafla ya kupokea Gawio na Michango kutoka kwa Mashirika na taasisi za umma Ikulu jijini Dar es Salaam.
Pia alisema, katika kuimarisha utawala bora na tija ya mashirika ya umma, ofisi imezindua na kuanza kutumia mfumo wa kidijitali wa kufanya tathmini ya bodi, hali ambayo imewezesha kukamlisha tathmini kwa wakati na kwa mawanda tarajiwa.
Aidha, alisema ofisi imeanza kutumia vigezo vipya vya uendeshaji wa mashirika vilivyoingiwa kwa njia ya mikataba baina ya wenyeviti wa Bodi na Msajili wa Hazina.
"Vigezo hivi vimeboreshwa zaidi na vimezingatia mgawanyo wa kisekta na majukumu ya msingi ya taasisi, na tutaendelea kuboresha vigezo hivi mara kwa marana pia kwa kutegemea mrejesho kutoka taasisi zetu hizi ambao ndio wadau wetu."
Mchechu alisema, ofisi pia imefanikiwa kupitia mikataba mbalimbali ya kibiashara na pia kufanya mazungumzo na wabia wetu kwenye sekta nyeti za uchumi.
"Kwenye sekta ya madini kumekuwa na mazungumzo mbalimbali tukishirikiana na Wizara ya Madini na tumeweza kuongeza hisa za serikali katika baadhi ya Kampuni, Mathalani tumeongeza hisa za serikali katika Kampuni ya madini ya Sotta kutoka 16% hadi 20%, jambo litasaidia sana katika majadiliano ya mikataba mingine ambayo tupo katika mazungumzo."
Pia alisema, wamefanikiwa kukamilisha majadiliano na kuingia mikataba mipya ya wanahisa na makampuni kama NMB, NBC na MCCL ambapo kati ya mikataba mingi inayofanyiwa kazi, na kampuni ya MCCL imeweza hatimaye kupata faida mwaka huu na kutoa Gawio kwa wanahisa Mwaka huu baada ya kipindi cha miaka 10.
Kuhusu GAWIO, Mchechu alitoa rai kwa wale ambao wanadaiwa au hawajatoa kuhakikisha kuwa wanakamilisha malipo yao kabla ya mwisho wa Mwaka huu wa fedha.
Mchechu alisema, Serikali imepokea jumla ya shilingi 637,122,914,887.59 ikijumuisha gawio shilingi 278,868,961,122.85 kutoka katika mashirika ya biashara na michango shilingi 358,253,953,764.74 kutoka katika taasisi nyingine, makusanyo hayo ni kwa kipindi kinachoanzia Julai 2023 hadi mwezi Mei 2024.
Alisema, kwa kuwa mwaka wa fedha wa 2023/24 bado haujakamilika, makusanyo bado yanaendelea, na wanatarajia kufikisha kiasi cha shilingi bilioni 850.
"Jumla ya mashirika yaliyochangia katika kipindi hiki ni 145 ambalo ni ongezeko la mashirika 36 kutoka 109 ya mwaka jana.
"Aidha, mashirika 159 hayajachangia kabisa katika Mfuko Mkuu wa Serikali kwa mwaka huu. Idadi hii sio ndogo, hivyo tunatoa wito kuwa taasisi zote zibadilike na kuboresha utendaji wao wa kazi utakaowawezesha kuanza kuchangia ama kuongeza uchangiaji katika mfuko mkuu wa Serikali. Kuchangia katika mfuko mkuu wa serikali sio suala la kujitolea au fadhila kwa Serikali, bali ni wajibu wa lazima,"alisisitiza.
Mchechu alisema,miaka ya nyuma, kiasi kikubwa cha gawio kutoka katika mashirika ya biashara kilikuwa kinatoka katika mashirika ya umma ambapo kati ya mwaka 2019/20 hadi 2021/22 mashirika ya umma yalichangia kiasi cha shilingi bilioni 255.8, 161.6, na 207.2 mtawalia, huku kampuni ambazo serikali ina hisa chache zilichangia kiasi cha shilingi bilioni 44.3, 147.2 na 150.3 mtawalia.
Hata hivyo, Mchechu alisema mizania ya uchangiaji kwa sasa imebadilika kwa kiasi kikubwa ambapo asilimia kubwa ya gawio linatoka kwenye kampuni ambazo Serikali ina hisa chache.
Mathalani katika kipindi cha miaka miwili 2022/23 na 2023/24 gawio la mashirika ya umma yanayofanya biashara, ilikuwa shilingi bilioni 109.7 na 110.3 mtawalia, ambapo kampuni ambazo serikali ina hisa chache zilichangia kiasi cha shilingi bilioni 219 na bilioni 168 mtawalia katika kipindi hicho.
Mchechu alisema kwa mwaka huu, katika msimamo wa makampuni ya kibiashara yaliyofanya vizuri na kurejesha faida nzuri serikalini, nafasi kumi bora za juu zimeshikiliwa na makampuni ambayo tuna hisa chache
"Matokea haya kwetu yanaleta fikra mchanganyiko (mixed feelings) na ni wake up call kwetu kwa taasisi zetu za umma. Ni habari njema kwa kuwa inaonesha wazi uwezeshaji unaofanywa na serikali yako ya awamu ya sita katika kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya biashara yanafanikiwa kwa kampuni binafsi kufanya kazi nchini Tanzania na kupata faida."
Mchechu alisisitiza kwamba pamoja na kutoa gawio katika mfuko mkuu wa Serikali, mashirika yana faida pia katika maeneo mbalimbali ikiwemo kutoa ajira, kutoa huduma za msingi na wezeshi hata maeneo ambayo yasipata huduma kama kusingalikuwa na mashirika ya Umma, kubeba miradi ya maendeleo katika sekta zote za uchumi, kuchangia katika pato la taifa nk.
"Ni nia thabiti ya ofisi hii kuhakikisha kuwa faida hizi zinakuwa imara, endelevu na zinaendelea kuongezeka kila mara. "