NA DKT.MOHAMED O.MAGUO
JUNI 13, 2024 Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Tulia Ackson alitangaza kifo cha Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya kusaidia wanawake na vijana kujikwamua kiuchumi ya FUNGUA TRUST, Dkt.Shogo Richard Mlozi.
Dkt.Tulia Ackson alitoa taarifa hizo kabla ya kuanza kwa kikao cha 47 cha Mkutano wa Bunge la Bajeti.
Aidha,Dkt.Mlozi ambaye alichaguliwa kuiwakilisha Tanzania katika bunge hilo mwaka 2022 alikuwa anahudumu katika nafasi hiyo hadi 2027.
Lifuatalo ni shairi la kumlilia Dkt. Shogo Richard Mlozi aliyefariki katika Hospitali ya Mount Meru jijini Arusha.
Ikumbukwe Dkt. Shogo aliwahi kuwa mhadhiri na Mkuu wa Idara katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania katika Idara ya utalii na ukarimu na baadae akateuliwa kuwa Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii na baada ya muda kidogo akachaguliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Afrika ya Mashariki mpaka umauti ulipomkuta. Endelea;
KIITIKIO
Nyoyo'ze zasikitika, machozi hayakatiki
Ni kutwa kububujika, machoni hapakauki
Muumba wetu Rabuka, E-Mungu mwenye miliki
Mpokee Dokta. Shogo, OUT twamuombea.
1:OUT yote yalia
Nyoyo'zo zimezimia
Huzuni imewaingia
Dkt. Shogo kawaumiza
2:Utalii mtalamu
Mpole mtu rahimu
Heshima na ukarimu
Sifa'ze Dokta Shogo
3:Cheko lake tabasamu
Ni sifa'ye maalumu
Hata umpime damu
Shogo kajawa upendo
4:Uhadhiri ualimu
Shogo alizihudumu
Kuifundisha kaumu
Ya Huria Tanzania
5:Ta'mkumbuka dawamu
Mlozi mwenye nidhamu
Kwa Mungu wetu Rahimu
Peponi ataingia
6:Profesa Sedoyeka
Pole sana ya hakika
Mke wako kuondoka
Mwenyezi akupe nguvu
7:Na watoto kadhalika
Pole zetu ziwafika
Wazazi na marafika
Poleni sana msiba
8:Pole na kwako Spika
Na wote waheshimika
Wa Bunge la jumuika
Afrika ya Mashariki
KIITIKIO
Nyoyo'ze zasikitika, machozi hayakatiki
Ni kutwa kububujika, machoni hapakauki
Muumba wetu Rabuka, E-Mungu mwenye Miliki
Mpokee Dokta Shogo, OUT twamuombea
MTUNZI
Dkt.Mohamed Omary Maguo
Mshairi wa Kisasa
Mhadhiri Mwandamizi
Mkuu wa Itifaki
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania