NA LWAGA MWAMBANDE
WENGI wetu tunatambua kuwa, Bima ni mfumo wa kulipa kiasi cha fedha katika kampuni ya bima ili kujiinua au kujilinda na madhara ya tukio lolote baya litakalotokea katika kitu ulichokatia bima.
Kupitia mfumo huo wa kisheria ambao huwa unahusisha pande mbili kwa maana ya mtoa huduma na mkatabima, humwezesha mkatabima pindi anapopata tatizo kulingana na makubaliano ya pande mbili kupata fidia.
Ili kufanya makubaliano hayo yaweze kutendeka kwa haki, Serikali imekuwa msimamizi mkuu ambapo inawasimamia watoa huduma hizo kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), chini ya Sheria ya Bima Na.10 ya mwaka 2009.
TIRA ni taasisi ya Serikali ilioanzishwa ili kutekeleza majukumu ya kusimamia soko na kuendeleza biashara ya bima nchini na masuala yanayohusiana na bima kwa mujibu wa sheria ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania inahudumia kampuni za bima zilizosajiliwa, wadau wote na umma kwa ujumla wa bima kwa mujibu wa sheria.
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, bima si tu kwamba inakusaidia katika majanga ya kila siku, bali bima ya maisha ni jambo muhimu. Endelea;
1.Pata bima ya maisha, ondoa sintofahamu,
Ustawi wa maisha, ili uweze jikimu,
Watu umeorodhesha, mafao kwao yadumu,
Hebu wewe kata bima, faida kwako na kwao.
2.Kama umekata bima, miaka waifahamu,
Kisha ukapata homa, na uhai kutodumu,
Faida yote mazima, warithi wataishumu,
Hebu wewe kata bima, faida kwako na kwao.
3.Endapo muda wa bima, mkataji unadumu,
Malipo yote mazima, ni ya kwako yanadumu,
Faida mtu mzima, utatumia kwa zamu,
Hebu wewe kata bima, faida kwako na kwao.
4.Hiyo bima ya maisha, kwa mtoto ni elimu,
Mwenyewe wajichangisha, mtoto mtoto atahitimu,
Huwezi jihangaisha, kwamba ada iwe ngumu,
Hebu wewe kata bima, faida kwako na kwao.
5.Yuko shule ya msingi, ndiko apata elimu,
Azidi upiga mwingi, sekondari anatimu,
Gharama mbele ni nyingi, bima kwake ni muhimu,
Hebu wewe kata bima, faida kwako na kwao.
6.Bima ya miaka kumi, kwa ajili ya elimu,
Kuitoa haiumi, kidogokidogo dumu,
Kufikia hiyo kumi, jumla yake ni tamu,
Hebu wewe kata bima, faida kwako na kwao.
7.Itokee uko hai, mwana tapata elimu,
Na ukutoke uhai, ataipata elimu,
Kata bima kunywa chai, umefanya la muhimu,
Hebu wewe kata bima, faida kwako na kwao.
8.Endapo ukichangia, myaka mitatu kudumu,
Bima waweza tumia, dhamana iliyo tamu,
Mkopo jichukulia, mengine ukahudumu,
Hebu wewe kata bima, faida kwako na kwao.
9.Bima inapokomaa, sasa ni ya kwako zamu,
Mkao wa kula kukaa, kufaidika kwa zamu,
Miaka uliyokaa, hata hauifahamu,
Hebu wewe kata bima, faida kwako na kwao.
10.Faida za bima nyingi, kwako wewe mwanada
Kukata hiyo msingi, maisha yaweze dumu,
Wamefaidika wengi, kushuhudia wadumu,
Hebu wewe kata bima, faida kwako na kwao.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602