Pato Halisi la Taifa lazidi kuimarika

NA GODFREY NNKO

SERIKALI imesema, mwaka 2023, Pato halisi la Taifa lilifikia shilingi bilioni 148,399.76 kutoka shilingi bilioni 141,247.19 mwaka 2022, sawa na ukuaji wa asilimia 5.1 ikilinganishwa na asimilia 4.7 mwaka 2022.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Alexander Mkumbo ameyasema hayo leo Juni 13, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya uchumi wa nchi kwa mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2024/25.

Amesema,ukuaji huo ulichangiwa na jitihada mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali ikiwemo mikakati ya kukabiliana na athari za vita kati ya Ukraine na Urusi pamoja na uwekezaji wa kimkakati katika miundombinu ya nishati, maji, afya, elimu na usafirishaji.

Vile vile, kuongezeka kwa uzalishaji wa madini, hususani dhahabu na makaa ya mawe ikiwemo kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi iliyochachua shughuli za kiuchumi.

Waziri huyo amesema, kiwango cha ukuaji wa Pato la Taifa cha asilimia 5.1 mwaka 2023 kipo chini ya lengo la mwaka la asilimia 5.2.

Amesema, hiyo ilitokana na kupanda kwa gharama za uzalishaji katika baadhi ya sekta, mabadiliko ya tabianchi yaliyoathiri uzalishaji katika sekta ya kilimo kwa baadhi ya maeneo nchini na kuharibu miundombinu ikiwemo madaraja na barabara.

Sambamba na hatua zilizochukuliwa na nchi zilizoendelea katika kukabiliana na mfumuko wa bei zilizosababisha kuongezeka kwa gharama za mikopo kutoka masoko ya kimataifa ya fedha na hivyo kuathiri shughuli za uzalishaji.

Wakati huo huo, Waziri Prof.Mkumbo amesema,pamoja na mwelekeo mzuri wa ukuaji wa uchumi wa Tanzania katika kipindi cha miongo miwili iliyopita mambo matano yalichangia.

Mosi, amesema ukuaji wa uchumi umekuwa ukihusisha sekta chache na ambazo haziajiri watu wengi kutoka kaya maskini.

"Sekta zilizoongoza kwa ukuaji kwa mwaka 2023 ni pamoja na Sanaa kwa asilimia 17.7, fedha na bima kwa asilimia 12.2, madini kwa asilimia 11.3 na malazi na chakula kwa asilimia 8.3."

Amesema,sekta ambazo zilitarajiwa kuajiri watu wengi zilikua kwa kasi ndogo. Sekta hizo ni pamoja na kilimo kwa asilimia 4.2, viwanda kwa asilimia 4.3 na biashara kwa asilimia 4.2.

"Matokeo ya hali hii ni kwamba ukuaji wa uchumi umekuwa hauendani na kasi ya kupunguza umaskini kwa kiwango cha kuridhisha."

Pili, Waziri huyo amesema, ukuaji wa uchumi nchini umekuwa ukitegemea uwekezaji wa umma katika miundombinu na sekta binafsi haijaonekana kuchukua nafasi yake kikamilifu katika kuchochea ukuaji wa uchumi kama ilivyotarajiwa.

Waziri Prof.Mkumbo amefafanua kuwa, uwekezaji kupitia sekta binafsi ndio unaotarajiwa kuchochea ajira na uzalishaji. Jambo la tatu, amesema mauzo ya bidhaa nje ya nchi yameendelea kutegemea bidhaa ambazo hazijaongezwa thamani.

Kwa mfano, Waziri Prof.Mkumbo amesema, wakati uzalishaji viwandani ulitarajiwa kuchangia asilimia 24 ya mauzo ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi ifikapo mwaka 2025 mchango wa sekta hii kwa wastani wa miaka mitano (2019-2023) ulikuwa asilimia 17.1 pekee ukilinganisha na asilimia 16.9 mwaka 2019/20.

"Hii inamaanisha kuwa mauzo haya hayajachangia vya kutosha katika kuzalisha ajira."

Nne, Mheshimiwa Waziri Prof.Mkumbo amesema, nchi yetu bado inanunua zaidi kutoka nje kuliko kiwango tunachouza.

"Hivyo, bado tuna urari mkubwa katika biashara. Kwa mfano, thamani ya mauzo ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi kwa mwaka 2023 ilikuwa dola za Kimarekani bilioni 13.7 ukilinganisha na thamani ya manunuzi ya bidhaa ambazo Tanzania iliagiza kutoka nje ya nchi ya dola za Kimarekani bilioni 8.2.

"Hii ndiyo kusema nchi yetu bado inatumia fedha nyingi za kigeni kuagiza bidhaa ambazo zingeweza kuzalishwa nchini."

Kuhusu jambo la tano, Waziro Prof.Mkumbo amesema, uchumi umekuwa ukikua kwa kasi zaidi katika maeneo ya mijini kuliko vijijini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news