DAR-Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) ipo katika hatua za mwisho za kupokea maoni ya Kanuni za Rufaa za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2024 ili kuiwezesha Sheria ya Ununuzi Umma ya Mwaka 2023 kutekelezeka kwa ufanisi, ambapo pamoja na mambo mengine, Kanuni hizi zitatoa wigo mpana wa kuwasilisha malalamiko na rufaa.


Pamoja na mambo mengine, Dkt. Luhende ameongeza kuwa Sheria mpya ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 imeboresha masuala mbalimbali ikiwepo kupunguzwa kwa muda wa kushughulikia malalamiko na rufaa zinazotokana na michakato ya Ununuzi wa Umma.

Kwa upande wake, Kamishina wa Sera ya Ununuzi wa Umma, Wizara ya Fedha, Dkt. Frederick Mwakibinga amesema mabadiliko ya Sheria ya Ununuzi yamekuwa yakifanyika mara kwa mara kwa lengo la kupunguza muda, kuongeza uwazi na usawa katika shughuli za ununuzi wa umma, kuongeza ushindani na kupunguza mianya ya rushwa.
“Sote tumesikia kuwa muda wa kushughulikia malalamiko na rufaa umepunguzwa na shughuli zote za ununuzi wa Umma zinafanyika kwa njia Kieletroniki na PPAA ipo katika mchakato wa kukamilisha Kanuni za Rufaa za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2024 ambapo baada ya kukamilika zitasaidia kuboresha Sekta ya Ununuzi wa umma,” amesema Dkt. Mwakibinga.

Katika kikao hicho, Wakili wa kujitegemea, Bw. James Kasusura ameipongeza PPAA kwa kazi nzuri ya kusimamia mabadiliko ya Kanuni za Rufaa za Ununuzi wa Umma ikiwa ni pamoja na muda wa kutoa maamuzi katika mashauri yanayowasilishwa katika Mamlaka hiyo.
“Tunategemea kuboresha muda, kuongeza zaidi uwazi katika tendering, na uwazi katika mfumo na watu wavione na kuvitekeleza,” alisema Bw. Kasusura.
Mwaka 2004, Serikali iliifuta Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 3 ya Mwaka 2001 kutokana na upungufu uliokuwepo katika Sheria hiyo na kutunga Sheria Na. 21 ya mwaka 2004 ambayo ilitumika hadi mwaka 2011. Aidha, Serikali iliifuta Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 7 ya Mwaka 2011 na kutunga Sheria ya Ununuzi wa Umma Na.10 ya Mwaka 2023 ili kukidhi mahitaji ya sasa ambayo yalishindwa kutekelezwa na Sheria ile ya 2011.

Tags
Habari
Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA)
Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali
PPAA Tanzania
Wizara ya Fedha Tanzania