DAR-Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Prof. Elifas Bisanda, ameishikuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuboresha miundombinu mbalimbali ya chuo hiki ili kiweze kuwa karibu zaidi na jamii na kushiriki moja kwa moja katika kuleta maendeleo nchini.

“Katika kipindi cha hivi karibuni, serikali imekuwa ikituangalia kwa karibu sana. Tumepata haya magari manne haijawahi kutokea, bado tuna majengo saba ya maabara za kikanda yatakayoanza kujengwa hivi karibuni chini ya Mradi wa HEET halikadhalika serikali kupitia fedha za maendeleo inajenga Kituo cha Uratibu cha Pemba,"amesema Prof. Bisanda.
Aidha, Prof. Bisanda, amesisitiza matumizi sahihi ya magari hayo na utunzaji mzuri ili yaweze kudumu na yaweze kusaidia chuo kutimiza malengo yaliyokusudiwa. Pia, amewakumbusha watumishi wote kufanya kazi kwa ushirikiano ili kufanikisha malengo ya utekelezaji wa Mradi wa HEET ili uweze kamilika kwa wakati na mafanikio makubwa.
Wakati huo huo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anyesimamia Taaluma, Utafiti na Huduma za Ushauri wa Kitaalam, Prof. Alex Makulilo, ameendelea kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kukiwezesha chuo hiki.
Amesema pia, magari yaliyopatikana yatatumika kusaidia shughuli za utekelezaji wa Mradi wa HEET ambao unajenga maabara saba za Sayansi katika vituo saba vya mikoa ya Arusha, Kigoma, Mtwara, Mwanza, Morogoro, Pwani na Njombe, hivyo yatarahisisha usimamizi wa mradi huo.
Akihitimisha, Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Huduma za Mikoa na Teknolojia za Kujifunzia, Prof. Leonard Fweja, amewakumbusha watumishi wote kufanya kazi kwa bidii ili kuendelea kuijengea serikali imani kwa Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania ili iendelee kuwekeza miradi mbalimbali katika chuo hiki.
