Prof.Bisanda awapa kongole wakuu wa idara OUT

DAR-Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Elifas Bisanda, amewapongeza wakuu wa idara wa chuo hiki na kusema kuwa wanasaidia kwa kiwango kikubwa maendeleo ya chuo hiki hususani katika utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).
Prof. Bisanda, ametoa pongezi hizo wakati akifungua kikao kazi cha Kamati Tendaji cha siku mbili kinachofanyika Juni 20, 2024 na Juni 21, 2024 ambapo kamati hiyo inakutana na Wakuu wa idara wa chuo hiki kupeana mrejesho wa maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa HEET kinachofanyika katika kituo cha mikutano cha APC Mbweni jijini Dar es salaam.
“Wakuu wa idara ni wadau muhimu katika uendeshaji wa chuo hiki, wanajua mambo mengi juu ya chuo hiki. Tumewaita kwa sababu maalum kabisa ili muweze kujua nini kinaendelea katika mradi huu.” Amesisitiza Prof. Bisanda.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayesimamia Taaluma, Utafiti na Huduma za Ushauri wa Kitaalam, Prof. Alex Makulilo, amesema umuhimu wa wakuu wa idara ni wa kipekee ndiyo maana mapendekezo mengi katika mradi huu yanaanzia kwao hivyo wamewawaita ili wakae pamoja waweze kujitathmini kuona wametoka wapi na wanakwenda wapi kimkakati kwa kuangalia rasilimali zilizotolewa na Mradi wa HEET.

“Tumeona kuna umuhimu wa kukaa na wadau ili kuweza kujadili mandeleo ya mradi. Tutaangalia namna gani tunasonga mbele na tutajadili pia changamoto ambazo inawezekana zimejitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi ili kukamilisha utekelezaji wa mradi huu kwa ufanisi,” amesema Prof. Makulilo.

Akiwasilisha katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Endelezi ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dkt. Jacob Leopold, amesema program ya msingi (OFP) inayotolewa na chuo hiki kupitia udhamini wa Mradi wa HEET katika masomo ya Sayansi, Hisabati, Uhandisi na TEHAMA kwa wasichana walioshindwa kuendelea elimu ya juu kutokana na changamoto za umasikini, ujauzito au ukatili wa kijinsia, inaendelea vyema.
Ambapo amesema, wanafunzi wa kike 193 kati ya 203 wapo kambini katika Chuo cha Ualimu cha Singida kilichopo katika Manispaa ya Singida ambapo wanatarajia kumaliza mitihani yao ya mwisho Juni 24, 2024 ili kuhitimisha mwaka wao wa mafunzo hayo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news