PSSSF yazidi kuchanja mbuga

NA GODFREY NNKO

SERIKALI imesema, mwaka 2022/23, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma - (PSSSF) ulisajili wanachama wapya 47,851 ikilinganishwa na wanachama 19,910 kulingana na taarifa ya takwimu zilizokaguliwa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali mwaka 2021/22.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Alexander Mkumbo ameyasema hayo Juni 13, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya uchumi wa nchi kwa mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2024/25

Aidha, amesema wanachama wachangiaji wa mfuko walifikia 729,346 mwaka 2022/23 kutoka wanachama 717,943 mwaka 2021/22.

"Katika kipindi hicho, mfuko ulikusanya shilingi trilioni 1.67 kutokana na michango ya wanachama ikilinganishwa na shilingi trilioni 1.52 mwaka 2021/22.

"Hii ilitokana na kuongezeka kwa wanachama na kiwango cha mishahara kulikotokana na kupandishwa kwa madaraja na nyongeza kidato kwa watumishi wa umma."

Pia amesema,mfuko ulilipa mafao yenye thamani ya shilingi trilioni 1.56 mwaka 2022/23 ikilinganishwa na shilingi trilioni 1.69 zilizolipwa mwaka 2021/22, sawa na upungufu wa asilimia 7.7.

Amesema, hii ilitokana na mabadiliko ya Kanuni ya Mafao iliyoanza kutumika Julai 2022 na kupungua kwa idadi ya wanachama wanaostahili kulipwa mafao mbalimbali.

Vile vile, amesema mwaka 2022/23, thamani ya uwekezaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma ilifikia shilingi trilioni 7.90 kutoka shilingi trilioni 7.48 mwaka 2021/22.

Aidha, mapato ya mfuko yatokanayo na uwekezaji yaliongezeka kwa asilimia 16.7 na kufikia shilingi bilioni 685.44 mwaka 2022/23 ikilinganishwa na shilingi bilioni 44 587.56 mwaka 2021/22.

Kwa upande mwingine, thamani ya mfuko ilikuwa shilingi bilioni 8,102.34 mwaka 2022/23 ikilinganishwa na shilingi bilioni 7,415.7 mwaka 2021/22, sawa na ongezeko la asilimia 9.3.

"Hii ilitokana na kupungua kwa gharama za uendeshaji na kuongezeka kwa uwekezaji na mapato yatokanayo na uwekezaji."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news