NA DIRAMAKINI
HOFU imezidi kuongezeka kwamba, pengine Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Malawi, Mheshimiwa Dkt. Saulos Chilima amefariki katika ajali baada ya ndege ya jeshi kutoweka katika Msitu wa Chikangawa.
Msitu huo ambao unafahamika kwa jina lingine la Viphya Plantations unapatikana wilayani Mzimba ambapo hifadhi yake ilianza tangu mwaka 1948.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo, ndege hiyo ilitarajiwa kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mzuzu asubuhi ya leo Juni 10,2024.
Imeelezwa kuwa,Mheshimiwa Chilima alikuwa ndani ya ndege hiyo ya Jeshi la Ulinzi la Malawi kuhudhuria maziko ya Wakili Ralph Kasambara.
Hata hivyo, ndege hiyo ilishindwa kutua katika uwanja huo kutokana na hali mbaya ya hewa.
Serikali imethibitisha kuwa, mamlaka za mawasiliano zimepoteza mawasiliano na eneo hilo tangu saa 10 asubuhi.
“Ofisi ya Rais na Baraza la Mawaziri inapenda kuutaarifu umma kwa ujumla kuwa Ndege ya Jeshi la Ulinzi la Malawi iliyoondoka Lilongwe leo Jumatatu tarehe 10 Juni 2024 saa 09:17, ikiwa imembeba Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Saulos Klaus Chilima, na wengine tisa, ilishindwa kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mzuzu saa 10:02.
“Juhudi zote za mamlaka ya anga kufanya mawasiliano na ndege tangu ilipotoka kwenye rada zimeshindikana hadi sasa.
"Kwa hivyo, Kamanda wa Jeshi la Ulinzi la Malawi, Jenerali Valentino Phiri, amemjulisha Mheshimiwa Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera kuhusu tukio hilo,"Katibu wa Rais na Baraza la Mawaziri, Collen Zimba amesema katika taarifa yake.
Wakati huo huo, serikali pia imethibitisha kuwa Rais Lazarus Chakwera amesitisha safari yake ya Bahamas kutokana na tukio hilo.
"Rais Chakwera ameghairi kuondoka kuelekea Bahamas na kuagiza vyombo vyote vya mkoa na kitaifa kufanya operesheni ya haraka ya uokoaji ili kujua mahali ilipo ndege hiyo," ameongeza Zimba.
Aidha,vyanzo vingine vimesema kuwa simu ya Chilima ilipatikana mara ya mwisho saa 10:30 asubuhi ya leo.