Rais Dkt.Chakwera amteua Waziri wa Maliasili Dkt.Usi kuwa Makamu wa Rais wa Malawi

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Malawi, Mheshimiwa Dkt.Lazarus McCarthy Chakwera amemteua Dkt.Michael Bizwick Usi kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Malawi.
Uteuzi huo ameufanya kulingana na mamlaka aliyopewa na Katiba ya Jamhuri ya Malawi kifungu cha 84.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Juni 20,2024 na Katibu wa Rais na Baraza la Mawaziri, Colleen Zamba.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mheshimiwa Rais Dkt.Chakwera atamuapisha Dkt.Usi kesho saa 9:00 alasiri jijini Lilongwe.

Dkt.Usi kabla ya uteuzi huo alikuwa Waziri wa Maliasili na Mabadiliko ya Tabianchi wa Jamhuri ya Malawi.

Uteuzi wake umefanyika kuziba nafasi ya hayati Dkt.Saulos Klaus Chilima ambaye alifariki hivi karibuni katika ajali ya helikopta ya jeshi.

Helkopta aliyokuwa akisafiria Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Malawi,Mheshimiwa Dkt.Chilima ilipoteza mawasiliano ya rada Juni 10,2024 majira ya saa 3 asubuhi kwa saa za huko, ilipokuwa ikijiandaa kutua huko Mazuzu Kaskazini mwa Malawi.

Wadhibiti wa ndege walikuwa wamemshauri rubani kurejea Lilongwe, mji mkuu wa nchi hiyo, lakini alama za ndege hiyo zilipotea na baadaye ikapatikana ikiwa imeanguka msituni karibu na Mazuzu.

Vikosi vya uokoaji vilitatizika kutafuta mabaki hayo kutokana na uoto mnene. Aidha, Juni 11,2024 Rais wa Malawi, Mheshimiwa Dkt. Chakwera wakati akihutubia taifa alisema kwamba kila mtu aliyekuwa ndani ya ndege hiyo amefariki. Dkt.Chilima alizikwa Juni 17,2024.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news