DAR-Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Doto Biteko amekutana na Naibu Waziri wa Nishati wa Marekani Mhe. David Turk kuzungumzia masuala mbalimbali ikiwemo uwekezaji katika Sekta ya Nishati nchini.
Mkutano huo umefanyika Juni 12, 2024 jijini Dar es Salaam na kubainisha maeneo kadhaa ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika vyanzo mbadala vya nishati.Dkt. Biteko amesema mazungumzo ya pande hizo mbili yanajikita katika misingi thabiti na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan yanayolenga kuifungua nchi katika sekta mbalimbali.
"Kwanza mazungumzo haya yanatokana na maono ya Rais wetu ambaye siku zote anasisitiza kuboreshwa kwa diplomasia ya kiuchumi na hili limewezesha kuifungua nchi katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na mazungumzo na ugeni wa namna hii," amesema na kuongeza kuwa
Ziara ya Naibu Waziri wa Nishati wa Marekani pamoja na ujumbe wake unaangazia pia uwekezaji katika sekta ya madini kama vile madini ya Nikel na Graphite ambayo yanatumika katika uzalishaji wa nishati.
Aidha, Dkt. Biteko amebainisha maeneo kadhaa ya kimkakati yanayoiwezesha Tanzania kuwa kivutio cha uwekezaji ambayo ni pamoja na utulivu wa kisiasa, fursa na vivutio anuai vya uwekezaji, mifumo thabiti ya kisheria, vigezo vya kijiografia vinavyoifanya Tanzania kuwa kiunganishi na nchi nyingine za mashariki, magaharibi na Kusini mwa Afrika, ukarimu wa Watanzania pamoja na maliasili zilizopo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati wa Marekani Mhe. David Turk amesema ujio wao unajikita katika ushirikiano katika mawanda mbalimbali na kuongeza thamani ya bidhaa mbalimabli yakiwemo madini yanayotumika kuzalisha nishati.
Mhe. Turk amesema, Uwekezeji katika sekta hizo utawezesha kubadilishana uwezo na uzoefu miongoni mwa wataalam kutoka nchi zote husika, Ushirikiano huo pia unaelezwa katika kuongeza fursa za ajira miongoni mwa watu kutoka nchi washirika na hivyo kuchochea maendeleo.
Tanzania iko katika mpango wa kimkakati wa kutafuta na kuanzisha vyanzo vipya vya nishati tofuati na nishati inayotokana na nguvu ya maji. Vyanzo hivyo ni pamoja, umeme jua, upepo, Jotoardhi na Tungamotaka.
Mazungumzo hayo pia yamehudhuriwa na Balozi wa Marekani nchini, Dkt. Michael Buttle Sr. maafisa waandamizi kutoka Mareakani pamoja na Wakuu wa Taasisi na Wawakilishi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati.