Rais Dkt.Samia ampongeza Askofu Wolfgang Pisa

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan amempongeza Mhashamu Askofu Wolfgang Pisa, Askofu wa Jimbo Katoliki Lindi kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).

Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ametoa pongezi hizo leo Juni 23,2024 kupitia kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii.
"Pongezi za dhati kwa Mhashamu Askofu Wolfgang Pisa, Askofu wa Jimbo Katoliki Lindi kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).

"Kuchaguliwa kwako katika nafasi hii ya uchungaji kwa Kanisa Katoliki nchini ni matokeo ya imani na matarajio ya Kanisa kwa utumishi wako.

"Nanukuu maneno mawili toka katika Biblia Takatifu kwenye Injili ya Yohana 19:28, “...Naona kiu” ambayo pia uliyachagua kuwa kaulimbiu yako ya Uaskofu.

"Katika utumishi huu nakuombea kiu ya kuendelea kufanya kazi ya kujenga Kanisa kwenye misingi ya upendo, haki, kweli, kujali masikini, umoja, amani, mshikamano, utu na kuhudumia jamii na Watanzania kwa ujumla, ndani na nje ya Kanisa Katoliki.

"Nakutakia kila la kheri. Mwenyezi Mungu akushike mkono na kukuongoza,"amefafanua kwa kina Mheshimiwa Rais Dkt.Samia.

Hivi karibuni Kanisa Katoliki limepata viongozi wapya, baada ya viongozi wa awali kumaliza muda wao.

Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga amemaliza muda wake wa miaka sita kama Rais wa TEC, akisaidiwa na Makamu wa Rais Askofu Flavian Kassala na Katibu Mkuu Padre Dkt.Charles Kitima.

Viongozi wapya waliochaguliwa ni Rais, Askofu Wolfgang Pisa kutoka Jimbo Katoliki Lindi, Makamu wa Rais, Askofu Eusebius Nzigilwa kutoka Jimbo Katoliki Mpanda huku Dkt.Charles Kitima akiendelea na wadhifa wake wa Katibu Mkuu ndani ya baraza hilo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news