Rais Dkt.Samia awaweka viporo viongozi hawa wababe

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema, bado kuna wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wanaoendeleza ubabe wakati wa utekelezaji wa majukumu katika maeneo yao.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea Taarifa ya Kamati ya Kuunda Mkakati wa Utekelezaji wa Mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai kutoka kwa Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu Mhe. Balozi Ombeni Sefue. Hafla ya upokeaji wa Taarifa hiyo imefanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 15 Juni, 2024.

Kutokana na hali hiyo, Mheshimiwa Dkt.Samia amewataka viongozi hao wazingatie taratibu za kazi na waheshimu mipaka yao ya kazi.

Ameyasema hayo leo Juni 15,2024 Ikulu Chamwino jijini Dodoma wakati akiwa kwenye hafla ya kupokea Taarifa ya Kamati ya Kuunda Mkakati wa Utekelezaji wa Mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi pamoja na wageni mbalimbali mara baada ya kupokea Taarifa ya Kamati ya Kuunda Mkakati wa Utekelezaji wa Mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai, Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 15 Juni, 2024.

"Linatakiwa kuwa jambo la kihistoria, Waraka Namba 1 wa 2023 wa Katibu Mkuu Kiongozi kwa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya unaelekeza na kusisitiza uzingatiaji wa sheria na kanuni katika utekelezaji wa mamlaka yao ya ukamataji uende ukatekelezwe vema.

"Pamoja na waraka ule, ambao umetolewa mapema mwaka jana, bado kuna wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wanaendelea ubabe kule maeneo waliko."
Viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla ya kupokea Taarifa ya Kamati ya Kuunda Mkakati wa Utekelezaji wa Mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai, Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 15 Juni, 2024.

“Nikimnukuu Makamu Mwenyekiti wakati ananipa briefing anasema wakati wa kikao chao na wakuu wa wilaya mmoja alithubutu kusimama na kusema ‘Mimi ni Mwakilishi wa Rais hapa kwa hiyo lolote lilipo huku ni la kwangu, hata nikisikia Mahakama imeamua sivyo Mimi nitatengua’,

"Sasa nadhani bado hatujakaa vizuri, kwa hiyo aidha elimu zaidi inahitajika au kuna usugu wa aina fulani ambao unahitaji kushughulikiwa.
"Kwa hiyo niseme kwamba waraka ule uzingatiwe na ukafanye kazi vizuri, lazima kila mmoja ajue taratibu za kazi na mipaka yake, twendeni kwa mipaka yetu.”

Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amezitaka taasisi zote vikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama nchini kuhakikisha ifikapo Desemba 31, mwaka huu mifumo yao ya utoaji haki ikiwemo haki jinai iwe inasomana.Viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla ya kupokea Taarifa ya Kamati ya Kuunda Mkakati wa Utekelezaji wa Mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai, Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 15 Juni, 2024.

Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amesema, lengo la kufanya hivyo ni ili kusaidia wananchi kupata haki zao bila kuchelewa na kwa wakati.

"Suala la mifumo yya TEHAMA naendelea kulisisitiza lifanyiwe kazi, kwa upande wetu.

"Upande wa Serikali niliweka tarehe ya kukamilisha taasisi zenu ziwe zinasomana, nayo ni Desemba kwa hiyo ni imani yangu kwamba upande wa taasisi za haki jinai mtakwenda kufuata ratiba hii."

Amesema kwamba, wajibu wa kuimarisha haki za raia kama zilivyoelekezwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 (Sura 1 sehemu ya 3) si suala la hiari bali la kufanyiwa kazi ipasavyo.

"Sote tunalazimika kusimama upande wa haki, suala la haki halina mbadala na ndio maana tunachukua hatua hizi tunazochukua."
Mheshimiwa Rais Dkt. Samia amesema, ili kufanikisha suala zima la kuleta mabadiliko katika utendaji wa taasisi za haki jinai kama Jeshi la Polisi, Magereza, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupamba na Dawa za Kulevya (DCEA) na nyinginezo lazima wahusika wafanye mabadiliko ya kifikra na kimtazamo na hawapaswi kuishi kwa mazoea.

Pia amesema kuwa, mambo yaliyokuwa yakimkereketa kuhusu hali ya haki jinai nchini sasa yanakwenda kufanyiwa kazi.
"Ndugu zangu, faraja yangu ni kwamba, yale yaliyokuwa yakinikereketa moyoni sasa yanachukua sura mpya ya mabadiliko katika kutenda haki ndani ya nchi yetu."

Vile vile amesema, Serikali imedhamiria kwa dhati kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai na tayari baadhi ya mapendekezo hayo yameanza kutekelezwa.

"Katika Bajeti ya Mwaka 2024/25 inayokamilishwa kwa kujadiliwa na wabunge, utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai ni moja ya vipaumbele katika ya wizara zetu na hasa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye hafla ya kupokea Taarifa ya Kamati ya Kuunda Mkakati wa Utekelezaji wa Mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma tarehe 15 Juni, 2024.

"Kipaumbele cha kwanza cha Wizara ya Katiba na Sheria ni kutunga Sera ya Taifa ya Haki Jinai. Hii inaonesha kwamba Serikali imedhamiria kwa dhati kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai na kutumia mapendekezo ya tume kuleta mageuzi chanya kwenye mfumo wa haki jinai."

Awali, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Balozi Ombeni Sefue amesema,wamegundua baadhi ya watendaji katika taasisi za haki jinai ni wagumu katika kupokea mabadiliko na kuyaishi.
Amesema, wakati tume hiyo ikikusanya maoni ya wananchi juu ya mambo mbalimbali juu ya haki jinai, malalamiko ya watuhumiwa kuteswa yameanza kushughulikiwa ikiwa ni pamoja na Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma kuweka kanuni za kuongoza uchukuaji wa maelezo kwa njia ya kielektroniki ili kuongeza kasi ya usikilizwaji wa mashauri ya watuhumiwa.

"Mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai yanagusa maeneo mengi na yanaashiria mabadiliko makubwa sana ya kiutendaji katika taasisi za haki jinai.

"Ni kawaida kwa binadamu kuhofu mabadiliko jambo ambalo ni kihatarishi kikubwa katika kuyafanya kuwa sehemu ya utamaduni.

"Inawezekana wako wanaoamini huu moto wa mabadiliko utapoa na hatimaye kuzimika, tunaomba hali hiyo isitokee."
Kutokana na hatua hiyo, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ameipongeza Mahakama ya Tanzania chini ya Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma kwa utayari wa kupokea na kufanyia kazi mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai.

"Kwa upande mwingine pongezi zangu nyingi sana ni kwa Jaji Mkuu wa Tanzania.

"Upande wa Mahakama kazi kubwa imefanywa kama ambavyo Makamu Mwenyekiti wa Kamati (Balozi Sefue) alivyoeleza.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko, Spika wa Bunge Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma, Viongozi wengine kwenye picha ya pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Kuunda Mkakati wa Utekelezaji wa Mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 15 Juni, 2024.

"Mheshimiwa Jaji Mkuu hongera sana na niwahakikishie kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono jitihada zenu."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news