Rais Dkt.Samia kushiriki uapisho wa Rais mteule Ramaphosa kesho

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kusafiri leo Juni 18,2024 kuelekea nchini Afrika Kusini kwa ziara ya kikazi ya siku moja.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiteta Rais wa Afrika Kusini, Mhe. Cyril Ramaphosa mjini Pretoria Machi 16, 2023 alipofanya ziara ya kiserikali nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Sharifa Nyanga, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ataondoka leo jioni.

Mheshimiwa Dkt.Samia akiwa nchini humo atashiriki hafla ya kuapishwa Rais mteule, Matamela Cyril Ramaphosa ambaye ataapishwa kesho Juni 19,2024.

Uapisho huo unafanyika ikiwa ni kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 30, Chama cha African National Congress (ANC) kimepoteza wingi wake bungeni na kulazimisha kutafuta muungano.

ANC kilifikia makubaliano na Chama cha Democratic Alliance na kumpa aliye madarakani kura zinazohitajika kuunda Serikali ijayo.

Juni 15, 2024 Bunge la Afrika Kusini lilitangaza ushindi wa Ramaphosa na kupata muhula wake wa pili.

“Bunge katika kikao chake cha kwanza cha Bunge la 7 leo limemchagua Mheshimiwa Cyril Ramaphosa kuwa Rais Mteule wa Jamhuri ya Afrika Kusini. Amechaguliwa tena kuhudumu kwa muhula wa pili wa Rais," ilieleza taarifa iliyotolewa na Bunge.

Rais aliye madarakani alichaguliwa kwa kura 283 dhidi ya wapiganaji wa siasa kali za mrengo wa kushoto wa Economic Freedom Fighters (EFF),Julius Malema ambaye alishinda kura 44.

Tanzania na SA

Uhusiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Afrika Kusini una historia ndefu, hivyo pande zote zimeendelea kudumisha udugu wao wa kihistoria.

Afrika Kusini inatambua mchango wa kijeshi, kijamii na vifaa kwa wapigania Uhuru wake uliotolewa na Tanzania wakati wa siku za kiza za ukandamizaji nchini humo.

Kuanzia miaka ya mwanzo ya 1960 hadi Afrika Kusini ilipopata Uhuru, Tanzania ilikuwa nyumbani kwa wapigania Uhuru wa Afrika Kusini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news