NA GODFREY NNKO
RAIS wa Jamhuri ya Tunisia,Mheshimiwa Kais Saied amemfuta kazi Waziri wa Mambo ya Dini nchini humo,Ibrahim Chaibi baada ya raia 49 wa Tunisia kufariki dunia wakati wa ibada ya kila mwaka ya Hija huko Macca nchini Saudi Arabia.
Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Kidini, Ibrahim Chaibi. (Picha na TN).
Mheshimiwa Chaibi alikutana na maamuzi hayo magumu kutoka kwa Rais huyo Juni 21,2024.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari kutoka ndani na nje ya Tunisia, Waziri huyo alidaiwa kuzembea katika usimamizi wake wa mahujaji ambao walikuwa Saudi Arabia.
Aidha, ilidaiwa Watunisia wengi waliokufa walikuwa wamesafiri kwenda Saudi Arabia kama watalii na sio mahujaji.
Kutokana na changamoto hiyo, Watunisia hao hawakuweza kupata usaidizi wa haraka.
Hayo yanajiri ikiwa Saudi Arabia imekuwa na joto kali wakati wa Hija, iliyoanza Ijumaa iliyopita na kumalizika Jumatano.
Taifa hilo la Afrika Kaskazini limekuwa likipitia katika kipindi kigumu ikiwemo kisiasa hali ambayo imechochea mawaziri wengi kufutwa kazi.
Mathalani, mwaka jana Kais Saied alimfuta kazi Waziri wa Mambo ya Nje,Othman Jerandi katika mazingira ya mvutano wa kisiasa nchini humo.
Wengine waliofutwa kazi ni Waziri wa Biashara, Madini na Nishati,Neila Nouira Gonji, Waziri wa Kilimo,Mohamed Ilyes,Waziri wa Elimu,Fathi Selaouti na wengineo.(NA/DIRAMAKINI).