Rais Putin,Kim Jong Un wafikia makubaliano ya uwaguse wanuke

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Urusi, Vladimir Putin amesaini makubaliano ya ushirikiano wa kimkakati wa kina na kiongozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Korea Kaskazini,Kim Jong Un ambapo kuna kifungu cha ulinzi kinachosisitiza gusa kati ya mataifa hayo mawili uone cha moto.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya ndani na nje kutoka mataifa hayo mawili, makubaliano hayo yamefikiwa Juni 19,2024 wakati wa ziara ya Rais Putin mjini Pyongyang.

Makubaliano hayo ya ulinzi wa pande zote, yanatajwa kuwa ni moja ya hatua muhimu zaidi za Urusi barani Asia kwa miaka ambayo Kim amesema ni muungano muhimu.

Urusi na Korea Kaskazini zinajiimarisha wakati ambao Marekani na washirika wake wa Asia wanajaribu kupima ni kwa kiasi gani Urusi inaweza kuongeza uungaji mkono kwa nchi pekee iliyojaribu silaha za nyuklia katika karne hii.

Katika ziara yake ya kwanza Pyongyang tangu Julai 2000, Putin ameonesha wazi kuzidisha uhusiano wa Urusi na Korea Kaskazini.

Vilevile ni katika kipindi ambacho uungaji mkono unaoongezeka wa nchi za Magharibi kwa Ukraine,Putin anasema Moscow inaweza kuendeleza ushirikiano wa kijeshi na kiufundi zaidi Pyongyang.

"Mkataba wa kina wa ushirikiano uliotiwa saini leo unatoa, pamoja na mambo mengine, kwa usaidizi wa pande zote katika tukio la uchokozi dhidi ya mmoja wa washiriki wa makubaliano haya,"Rais Putin amebainisha.

Pia, amesema uwasilishaji wa silaha za hali ya juu na za masafa marefu za nchi za Magharibi ikiwa ni pamoja na wapiganaji wa F-16 kwenda Ukraine kwa ajili ya mashambulizi dhidi ya Urusi ulikiuka makubaliano.

"Kuhusiana na hili, Urusi haijizuii yenyewe maendeleo ya ushirikiano wa kijeshi na kiufundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea."

Naye Kim aliipongeza Urusi kwa kufanya kile alichokiita kama hatua muhimu ya kimkakati ya kuunga mkono Korea Kaskazini, ambayo ilianzishwa mwaka 1948 kwa kuungwa mkono na Umoja wa Kisovieti.

Wataalamu wa masuala ya kiusalama, wanautaja mkataba huo ambao haujawekwa wazi kama msingi wa kuimarisha mikakati ya kiusalama na kiuchumi kwa Urusi huko Asia.

Ikizingatiwa kuwa, Marekani imejiimarisha zaidi katika ukanda huo huku Jamhuri ya Korea ikiwa mshirika wake muhimu.

Mkazo huo unakuja katika kipindi ambacho bado Jamhuri ya Kidemokrasia ya Korea Kaskazini na Jamhuri ya Korea zimeendelea kuvutana mara kwa mara,mivutano ambayo ni ya miaka nenda rudi tangu pande hizo zipigane.

Historia inaonesha vita vya Korea vilikuwa vita vya kijeshi kati ya Korea Kaskazini na Kusini vilivyoanza Juni 25, 1950 hadi Julai 27, 1953.

Kaskazini ilivamia Kusini Juni 25, 1950, katika jitihada za kuunganisha nchi chini ya utawala wa Kikomunisti.

Aidha, Umoja wa Mataifa, ukiongozwa na Marekani uliingilia kati kwa niaba ya Korea Kusini, na muungano wa majeshi ya Umoja wa Mataifa hasa kutoka Marekani, walipigana dhidi ya majeshi ya Korea Kaskazini na China.

Vita hivyo vilikuwa na mapigano makali, huku kukiwa na hasara kubwa kwa pande zote mbili.

Usitishaji mapigano ulitangazwa Julai 27, 1953, na eneo lisilo na jeshi lilianzishwa kando ya 38 maarufu kama Demilitarized Zone (DMZ), ambalo bado linatumika kama mpaka kati ya Korea Kaskazini na Kusini hadi leo.

Vita vya Korea vilisababisha vifo vya mamilioni ya watu na kuiacha Rasi ya Korea ikiwa imegawanyika na kuandamwa sana kijeshi.

Ingawa Korea Kaskazini ina mkataba wa ulinzi na China, haina ushirikiano wa kijeshi na Beijing kama ilivyoendelea na Urusi katika mwaka uliopita.

Korea Kaskazini pia ilitia saini mkataba wa mwaka 1961 na Umoja wa Kisovieti ambao ulijumuisha ahadi za kusaidiana endapo shambulio litatokea.(NA/DIRAMAKINI).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news