DAR-Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Filipe Jacinto Nyusi atawasili nchini Julai 01, 2024 kwa ziara ya Kitaifa hadi julai 04, 2024 kufuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Atakapowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Rais Nyusi atapokelewa na viongozi waandamizi wa Serikali na mapokezi rasmi yatafanyika Ikulu jijini Dar Es Salaam Julai 02, 2024.
Akiongea na waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba alisema pamoja na mambo mengine, Rais Nyusi atakuwa Mgeni Rasmi katika hafla ya ufunguzi wa Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar Es Salaam maarufu, Sabasaba siku ya tarehe 03 Julai, 2024.
Mhe. Waziri Makamba alieleza kuwa ziara hiyo ya Rais Nyusi nchini itakuwa ziara ya mwisho kama kiongozi wa nchi kutokana na kumaliza mihula miwili ya uongozi wake mwezi Oktoba 2024. Hivyo, ziara hiyo ataitumia kumuaga Rais Samia na Watanzania kwa ujumla.
Waziri Makamba alisema Tanzania na Msumbiji zina uhusiano mzuri ambao ulianza miaka mingi iliyopita.
Alieleza kuwa chama tawala cha nchi hiyo (FRELIMO) kilianzishwa nchini na kiongozi wake wa kwanza, Hayati Eduardo Mondlane aliuawa na kuzikwa hapa nchini mwaka 1969.
Uhusiano huo uliendelea kwa Rais wa kwanza wa Tanzania, Hayati Julius Kambarage Nyerere kutoa mchango mkubwa katika harakati za kutafuta uhuru hadi ulipopatikana mwaka 1975.
Uhusiano uliendelea kuimarika na hadi ilipofikia mwaka 1977 nchi mbili hizi zilisaini Makubaliano ya kuanzisha Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC). Tangu kuanzshiwa kwa Tume hiyo, mikutano 15 ya JPCs imefanyika.
Kupitia mikutano hii, nchi mbili zimeweza kukubaliana kushirikiana katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ulinzi na usalama, uhamiaji, biashara, uwekezaji, utalii, kilimo na uchukuzi.
Aidha, Waziri Makamba alisema Tanzania imekuwa mstari wa mbele kuisaidia Msumbiji kukabiliana na changamoto za kiusalama. Alitolea mfano wa Tanzania kuwa moja kati ya nchi 11 za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zilizochangia vikosi vya kulinda amani nchini Msumbiji kufuatia mashambulizi ya vikundi vya kigaidi Kaskazini mwa nchi hiyo, hasa katika majimbo ya Cabo Delgado, Niassa na Nampula.
Rais Samia na Mgeni wake, Rais Nyusi watashiriki mazungumzo ya faragha na rasmi ambayo yanatarajiwa kujikita katika kukuza biashara, uwekezaji, ulinzi na usalama. Viongozi hao pia watashuhudia uwekaji saini wa makubaliano mbalimbali ya ushirikiano katika maeneo ya ulinzi, elimu na afya kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari Julai 02, 2024.
Rais Nyusi ataondoka nchini Julai 04, 2024 kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Aman Abeid Karume baada ya kumaliza ziara binafsi mjini Zanzibar.