NA GODFREY NNKO
RASILIMALI za Kampuni ya Uwekezaji wa Pamoja (UTT AMIS) zimeendelea kuongezeka ambapo hadi Aprili 2024 zilifikia zaidi ya shilingi trilioni 2 kutoka zaidi ya shilingi trilioni 1 huku elimu ikiwa msingi wa mafanikio hayo.
Hayo yamesemwa leo Juni 4, 2024 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt.Mwigulu Lameck Nchemba wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Fedha kwa mwaka 2024/2025.
Amesema, katika mwaka 2023/24 kampuni hiyo ilipanga kuongeza rasilimali za mifuko kwa kiwango cha asilimia 15.
Pia,kuongeza idadi ya wawekezaji kwa asilimia tano na kuhamasisha taasisi za Serikali, mifuko ya hifadhi za jamii, mashirika na vikundi mbalimbali vya kijamii kama vile SACCOS kujiunga na mifuko ya UTT AMIS.
"Hadi Aprili 2024, rasilimali za mifuko ziliongezeka hadi shilingi bilioni 2,012.8 kutoka shilingi bilioni 1,535.8 Juni 30, 2023, sawa na ongezeko la asilimia 31.1.
"Na idadi ya wawekezaji kwenye mifuko ya uwekezaji wa pamoja iliongezeka kwa asilimia 19.2. Sababu za kuvuka malengo ya 2023/24 ni kuongezeka kwa uelewa wa wananchi kuhusu faida ya uwekezaji wa pamoja.
"Na matumizi ya teknolojia katika utoaji huduma na ongezeko la mawakala waliosajiliwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam,"amesema Waziri Dkt.Mwigulu.