RC Makongoro Nyerere awauma sikio watoa huduma ndogo za fedha Rukwa

NA EVA NGOWI

MKUU wa Mkoa wa Rukwa, Bw. Charles Makongoro Nyerere amewataka watoa huduma ndogondogo za fedha mkoani kwake wasajili huduma zao za kifedha kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2018, na kuwaelekeza watoe elimu kwa wateja wao kabla ya kuwakopesha.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Bw. Charles Makongoro Nyerere, aliyeketi akiwa katika picha ya pamoja na Timu ya utoaji Elimu ya Fedha mara baada ya kumalizika kwa mkutano na waandishi wa Habari uliofanyiaka Ukumbi Mdogo wa Mikutano wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Wilaya ya Sumbawanga Mjini.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha, Rukwa).

Bw. Charles Makongoro Nyerere ametoa maagizo hayo wakati wa kikao na Waandishi wa Habari katika Ukumbi Mdogo wa Mikutano wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Wilaya ya Sumbawanga Mjini.

“Ndugu wanahabari; watoa huduma ndogo za fedha ni watu muhimu katika mkoa wetu wa Rukwa na Taifa kwa ujumla. Pamoja na umuhimu huo naagiza kuwa watoa huduma ndogondogo za fedha wote mkoani Rukwa wasajiliwe kwa mujibu wa sheria,”amesema Bw. Makongoro.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Bw. Charles Makongoro Nyerere, akiongea na waandishi wa Habari (hawamo pichani) kuhusu umuhimu wa usajili na utoaji elimu ya fedha kwa watoa huduma Ndogo za fedha katika Ukumbi Mdogo wa Mikutano wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Wilaya ya Sumbawanga Mjini.

Bw. Makongoro alisema kuwa sambamba na zoezi la kusajili vikundi vidogovidogo vya huduma ndogo za fedha, ni vyema pia kwa watoa mikopo kutoa elimu kwa wanaowakopesha na kuwapa muda wa kuelewa mikataba kabla ya kuwapa mkopo.

“Mtoa huduma za kifedha toa elimu kwa yule unayetaka kumkopesha kuhusu huduma yako kabla ya kumkopesha. Na hili liende sambamba na wanaokopeshwa kupewa muda wa kutosha kusoma mikataba yao na kuielewa vizuri kabla ya kumkopesha, usimshtukize ule mkataba mpe muda ausome auelewe ndio umkopeshe,"amesisitiza Bw. Makongoro.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Bw. Charles Makongoro Nyerere (kushoto) akipokea kitabu cha nyenzo ya kufundishia Elimu ya Fedha kutoka kwa Afisa Mkuu Mwandamizi kutoka Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Bw. Salim Kimaro (kulia) katika Ukumbi Mdogo wa Mikutano wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Wilaya ya Sumbawanga Mjini.

Vile vile alitoa rai kwa Wakuu wa Wilaya wote wa Mkoa wa Rukwa kuwa wahakikishe wanasimamia maelekezo yake kuanzia ngazi ya Vijiji, Kata, Tarafa pamoja na Halmashauri zote.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Bw. Charles Makongoro Nyerere, alihitimisha kwa kuwaomba wananchi wote wa Mkoa wa Rukwa kutoa ushirikiano ili kuwabaini wale wote wanaotoa huduma za fedha kinyume na utaratibu wa kisheria ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Timu ya Wataalamu ya utoaji wa Elimu ya Fedha Pamoja na baadhi ya Waandishi wa Habari wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Bw. Charles Makongoro Nyerere (hayumo pichani) wakati wa mkutano na waandishi hao katika Ukumbi Mdogo wa Mikutano wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Wilaya ya Sumbawanga Mjini.

Aidha, aliwashukuru wataalam kutoka Wizara ya Fedha kwa kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa mkoa wake katika Wilaya na Halmashauri zake zote.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news