RC Mtanda afungua maadhimisho ya Kimataifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya duniani

NA GODFREY NNKO

MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Mheshimiwa Said Mtanda amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo Serikali anayoiongoza inavyochukua jitihada mbalimbali kukabiliana na dawa za kulevya nchini.
Ameyasema hayo leo Juni 28,2024 katika Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza wakati akifungua Maadhimisho ya Kimataifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani.

"Nipende sana kumshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo Serikali yake inachukua jitihada nyingi kutekeleza Ilani ya Uchaguzi Ibara ya 245 (2020-2025) inayoielekeza Serikali yake kuchukua hatua kadha wa kadha katika kupambana na uzalishaji, usambazaji, uuzaji na utumiaji wa dawa za kulevya."

Sambamba na hilo, RC Mtanda amesema ni utekelezaji pia wa Azimio la Bunge la Mwaka 2022 na matakwa ya Itifaki na Mikataba ya Kikanda na Kimataifa kwa namna ambavyo Serikali imekuwa ikitekeleza mikataba hiyo katika vita dhidi ya dawa za kulevya.
Wakati huo huo, RC Mtanda amempongeza Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupamba na Dawa za Kulevya nchini (DCEA),Aretas Lyimo kwa kazi nzuri anayoifanya.

Pia ameipongeza DCEA kwa kazi nzuri katika kudhibiti uuzaji, usambazaji na utumiaji wa dawa za kulevya nchini.

"Kwa namna ya kipekee nikushukuru na kukupongeza Kamishna Jenerali kwa kuridhia Mkoa wa Mwanza kuwa mwenyeji wa Maadhimisho haya ya Kitaifa kwa mwaka huu.
"Ujio wenu na mamlaka yako, unachagiza shughuli mbalimbali za kiuchumi, lakini pia kuuchangamsha mji wetu na jiji letu la Mwanza.

"Asanteni sana kwa kuja, kauli mbiu ya maadhimisho haya ni ''Wekeza kwenye Kinga na Tiba, Kudhibiti Dawa za Kulevya''.

"Ndugu zangu wananchi wenzangu kaulimbiu ya mwaka huu pamoja na mambo mengine inasisitiza umuhimu wa elimu kwa jamii ili iweze kufahamu madhara ya dawa za kulevya.
Kushirikisha jamii katika kutatua changamoto zinazotokana na dawa za kulevya pamoja na kuhimiza tafiti mbalimbali za kisayansi.

Zenye lengo la kubainisha kiiini cha matatizo ya namna hii au dawa za kulevya na kutafuta njia za kuondokana na dawa za kulevya."

Ameeleza kuwa, tatizo la dawa za kulevya duniani linaendelea kuongezeka ambapo kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuzuia Dawa za Kulevya na Uhalifu ((UNODC) kwa mwaka 2023 matumizi ya dawa za kulevya yaliongezeka kwa asilimia 24.

"Ikilinganishwa na mwaka 2010, aidha inakadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni 296 duniani wanatumia dawa za kulevya ambapo,ambapo kati ya watu hao, milioni 39.5 ni waraibu.
"Yaani, waathirika wa dawa za kulevya. Matumizi ya dawa za kulevya pamoja na athari nyingine yanachangia sana maambukizi ya UKIMWI,homa ya ini na magonjwa mbalimbali ya ngono.

Matumizi ya dawa za kulevya, yanaathiri uwezo wa kimwili, kifkra na wakati mwingine watumiaji wa dawa za kulevya wanakuwa wana mchango mdogo katika maendeleo ya Taifa letu, lakini pia katika uchumi wao binafsi, familia zao na Taifa kwa ujumla.

Lakini, madhara makubwa pia ya matumizi ya dawa za kulevya ni vifo vinavyotokana na athari za dawa za kulevya."

Amesema kuwa, taarifa ya hali za dawa za kulevya nchini kwa mwaka 2022, zinabainisha tatizo la dawa za kulevya, kwani waraibu wa dawa hizo na vilevi vingine imeongezeka.
"Kutoka watu 166,266 mwaka 2020 hadi 854,135 kwa mwaka 2022 ambapo asilimia 78 ni vijana wenye umri wa kufanya kazi kati ya miaka 15 hadi miaka 35.

Waraibu waliosajiliwa katika vituo 16 vya tiba ya Methadone kwa ajili ya uraibu wa Heroin ni watu 16,460. Lakini, pia waraibu hawa ni wanawake na wanaume.

Waraibu wanaopata huduma katika nyumba za upataji nafuu, yaani Sober House ni 56, kwa hiyo mnaweza mkaona ukubwa wa tatizo hili."

Kamishna Jenerali

Kwa upande wake, Kamishna Jenerali Aretas Lyimo amesema, dawa za kulevya ni vita vya kidunia ambavyo vinahitaji ushirikiano wa pamoja ili kuvishinda.
"Mataifa yote kulingana na mikataba mbalimbali tuliyoingia ya Kimataifa kupitia Shirika la UNODC ambalo ndilo linalohusika na kuratibu shughuli zote za mapambano dhidi ya dawa za kulevya duniani, mataifa yote yametakiwa katika kipindi cha mwezi wa sita kuhakikisha kwamba yanaadhimisha maadhimisho ya kupiga vita dawa za kulevya duniani.
"Na sisi,Tanzania katika kuungana na mataifa hayo tumechagua siku ya tarehe 30 iwe ndiyo kilele cha kupiga vita dawa za kulevya duniani.Na leo, tarehe ni uzinduzi wa Wiki ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news